MUUAJI MWENYE BARAKOA - 42 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 MUUAJI MWENYE BARAKOA - 42

sultanuwezotz.blogspot.com 


Vurugu ndani ya jengo lile la mama Burudani ziliendelea huku kila mhusika akiwa ni Catherine. Waliingia kila kona kuhakikisha anapatikana ili ashughulikiwe lakini hawakuweza kumpata. Baada ya kila kona kutomuona walirudi mpaka kwenye chumba cha Bettina na kumkuta kitandani akiwa anachati.

"Acha kujichatisha hapo Kima wewe, hivi unawezaje kucheza na akili zetu?" Aliuliza mmoja wao.

"Hivi Naomi unaringia nini lakini? Umewazoazoa hao Misukule wenzako na kuja kunipigia kelele humu au mnafikiri na mimi ni Msukule mwenzenu?" Bettina alimuuliza Naomi dada wa kigauni kifupi.

"Hivi mnamsikia huyu ninyi?" Naomi aliuliza akiwa amemvaa mwilini Bettina na kuanza kupigana pale kitandani.

"Hebu acheni bwana mnafanya nini? Anahusikaje Betty hapa?" Mmoja wao alikuja na kuwaamlia huku wengine wakishangilia.

"Hujui kama huyu ndiyo aliyemficha Catherine?" Naomi alimjibu huku akiwa kawekwa chini na Betty akipokea kichapo. Na wakati makelele yakiwa yameshika kasi Catherine alijitokeza kutoka chooni.

"Naombeni muache kupigana wenyewe kwa wenyewe Betty hana kosa mwenye kosa ni mimi hivyo njooni kwangu." Walimgeukia wakamkamata na kumuangusha chini na kuanza kumshambulia kwa mingumi ambayo ilikuwa haichagui sehemu ya kutua, cha ajabu Catherine hakujibu mashambulizi badala yake alikuwa anajaribu kujinasua kutoka mikononi mwa Viswaswadu visivyo na namba.

" Hebu acheni mtamuua jamani hivi mna nini?" Betty aliingilia kati kuamulia ugomvi ule.

"Ina kuuma ee? Mtu wa ajabu sana wewe yaani apigwe mtu mwingine uumie wewe." Alijibiwa huku akisukumwa chini na kuangukia kwenye mguu wa mbele wa kitanda. Kupoteza fahamu kwa Betty pale chini kulimuinua Catherine kama Mbogo na kumpiga kichwa Naomi ambaye alikwenda kuwaangukia wenzake na kumsogelea Betty.

" Mnaona mlichokifanya hapa?" Catherine aliwauliza akijaribu kumuinua.

"Wewe ndiyo chanzo cha haya yote unafikiri bila wewe kungetokea ugomvi?"

"Unasemaje Naomi?" Aliinuka na kumtandika ngumi ya mdomo ambayo ilimpeleka mpaka chini huku akitokwa damu kama kala nyama mbichi.

Alirudi chini na kumbeba Betty na kumlaza kitandani ambapo alianza kumfanyia huduma ya kwanza. Ngumi ile iliwafanya wenzao kutoka mbio mle chumbani bila hata kutoa msaada kwa Naomi. Dakika kadhaa Betty alizinduka na kujikuta kitandani.

"Unajisikiaje mdogo wangu?" Catherine alimuuliza.

"Eneo hili la sikio la kulia ndio lenye maumivu makali." Betty alimjibu akionesha sehemu ya juu kidogo ya sikio.

"Simu yako iko wapi tuombe msaada kwa Madam Carolyn?"

"Hakuna haja dada nitakuwa sawa tu, wacha ninywe dawa za kutuliza maumivu kama hali itakuwa tofauti kesho nitakwenda hospital." Alimjibu akijaribu kuinuka.

"Unakwenda wapi?"

" Nataka nichukue dawa kwenye droo ya 'dressing table'.

"We tulia tu acha nikuletee." Catherine alimtuliza na kwenda kumchukulia na baada ya kugeuka hakumuona Naomi naye alikimbia.

Alimletea dawa kisha alimuaga na kutoka mpaka nje japo hakufanikiwa kumkuta Naomi koridoni hivyo alirudi tena kwa Naomi.

"Niazime simu yako mara moja."

"Ila usimpigie mama tafadhali isije kuleta matatizo bure na mimi sipendi hilo litokee dada."

"Hapana ninataka kuongea na kaka yangu nyumbani." Alimjibu akiipokea. Aliingiza namba fulani na kuipiga, ilipoanza kuita alitoka nje ya chumba cha Betty na kuelekea mpaka kwenye chumba chake.

"Catherine hapa Martin." Alijitambulisha mara baada ya kuona simu imepokewa lakini mtu haongei.

"Oohh my sister, ndiyo nini kupotea hewani?" Martin aliuliza.

"Mdogo wangu nikikwambia niliko na kile kilichonitokea utacheka badala ya kunionea huruma." Catherine alimjibu.

"Kivipi dada?" Alimuuliza tena.

"Muda si rafiki naomba unijuze mmefikia wapi kwenye kazi ya kumsaka yule mtoto Jennifer?"

" Huku ni majanga tu dada yangu hivi ninavyoongea niko mafichoni na Awadh."

"Mafichoni?"

"Ndiyo."

"Kilichowakuta?"

"Kuna siku niliwaambia waongozane na vijana wangu kwenda kufanya tukio la utekaji sehemu moja hivi."

"Enhh nini kikawakuta Martin usiniambie wamekamatwa."

"Mmhh sijui hata nisemeje ili uweze kunielewa lakini kwa kifupi huko hawakuweza kufanikisha kwani ramani yao ilivuja mapema na kujikuta wako katikati ya walinda usalama."


"Oogh my God, Martin kwanini uliwapeleka vijana wangu huko wakati unajua fika hawana uzoefu na shughuli zako?" Catherine alimuuliza kwa ghadhabu.

"Naomba unisamehe tu kwa hilo dada yangu."

"Itasaidia nini samahani yako? Hebu niambie wako wapi kwa sasa?"

"Walikamatwa wote japo kuwa Seynabou na Jumbe walitupigia simu kuwa wametoroka kwa kuruka kwenye gari lakini hawakusema wako wapi mbaya zaidi gari zangu zote mbili ziko mikononi mwao na taarifa iliyopo ni kwamba wanamsaka mmiliki wa hayo magari wakisema yamehusika kwa kiasi kikubwa kwenye matukio ya utekaji."

" Umezipata wapi hizo taarifa wewe?" Catherine alimuuliza.

" Kuna rafiki yangu ambaye ni Afisa wa Jeshi la Polisi alinitaka kuondoka nchini kwa kuwa hali ni mbaya kwani nasakwa kwa udi na uvumba huku taarifa zikisema tukio lilifanyika japo vijana wangu wanadai waliotewa kabla ya kulifanikisha hivyo nimejificha hapa Nigeria lakini bado nafuatilia kujua kama nimepigwa au la." Majibu ya Martin yalimchanganya tu Catherine ambaye aliamua kumkatia simu na kumpigia Seynabou na kama bahati vile alimpata.

" Catherine hapa naongea."

"Jamani dada uko wapi?"

"Ni stori ndefu nikipata utulivu mzuri nitakuelezeni kilichonikuta huku."

"Mbona unanitisha dada?"

"Usitishike mdogo wangu, kwanza hebu niambie uko wapi?"

"Mmh tuko nchini Niger tulikuja kukusaka lakini taarifa ya siku mbili zilizopita ambayo tuliishuhudia kwenye televisheni ilitupa hofu na kujikuta tukitafuta pori la kujificha."

"Kivipi?"

"Tulilishuhudia gari lako likiwa limeungua na kubakia mabati tu huku taarifa likisema mmiliki wa gari hilo alijitoa mhanga kwa kutaka kulipua Kambi ya Jeshi la Ukombozi."

"Ilisemaje taarifa hiyo?" Catherine aliuliza akivuta usikivu zaidi.

"Ndiyo hivyo dada walisema kuwa gaidi huyo hakuweza kufanikiwa kwani gari lililipuka kabla ya kuifikia Kambi,sikutaka kuendelea kuitazama hiyo taarifa nikamwambia Jumbe tutafute njia nyingine ya maisha kwa kuwa tuliyekuwa tukimfuata ameshakufa japo Jumbe alipingana na taarifa hiyo akasema ni mpango wako tu ila haukuwa wewe." Seynabou alifafanua.

" Hebu ipuuzieni hiyo taarifa japo gari ni langu kweli mengine tutaongea hebu niambieni mlipo na wenzenu wako wapi?"

" Bado tuko hapa hapa Niger kwenye kijiji fulani hivi kinaitwa Nailoti niko na Jumbe hao wengine hatujui waliko, kilichotufikisha huku kuna tukio la mamilioni ya dollars tulilifanya lakini Martin tulimtengenezea filamu ambayo aliiamini na kajificha huko Nigeria akiwa na Awadh ila mpango mzima tutakusimulia, Martin katutumikisha sana bila malipo yoyote yale kwa kipindi hiki ambacho wewe uko mbali nasi hivyo tulifanya uamuzi mgumu na muda wowote Awadh ataungana nasi ila Adoyee usaliti ulimponza."

"Alifanya nini Adoyee?"

"Hakutaka tuondoke na mzigo kwa kushirikiana na vijana wa Martin hivyo tuliwapa haki yao kisha Awadh akatuamuru tutoroke na begi la hela ili yeye amfuate Martin akamalizane naye kisha ataungana nasi."

"Mbona mnanichanganya maana nimeongea na Martin kasema wao wamejificha kwa kuhofia kukamatwa na Polisi na yuko Awadh na kasema ninyi mlikamatwa kabla ya kufanikiwa?"

"Kadanganya dada hataki ujue kuna nini kinaendelea na katupania sana kwani mmoja wa vijana wake alifanikiwa kutoroka na wala hayuko na Awadh."

"Mhhh basi tuwasiliane kesho nikinunua simu hii msiipige nimeiazima tu." Catherine alimaliza na kukata simu. Alichokutana nacho alichoka mpaka akajilaumu aliyaanza ya nini kuwapigia simu wakina Seynabou. Aliinuka na kuelekea chumbani kwa Betty ili amrejeshee simu yake, akiwa anaukaribia mlango wa Betty alimuona Herieth akiufungua mlango wa chumba chake hivyo aliamua kunyata maana alikuwa hajamuona aliangalia huku na kule kuhakikisha anakuwa salama na baada ya kuufikia mlango wa Herieth alichungulia ndani kupitia tundu la ufunguo wa kitasa.

"Unafanya nini hapo wewe?" Sauti hiyo ilimfanya aduaye kidogo kwani hakutarajia kabisa.

"Mmh nilikuwa naangalia kama amerudi Herieth aniazime simu yake."

"Ndiyo uchungulie hivyo kwani hiyo swichi ya kengele hujaiona?"

" Ugeni mama yangu nilijua ni swichi ya taa tu."

"Acha ushamba bonyeza hiyo." Mama Burudani alimwambia Catherine na kuondoka lakini hakujua kama anafuatiliwa nyuma na Catherine ambaye hakuona sababu ya kumgongea Herieth wakati mhusika ni mama Burudani hivyo alinyata kuhakikisha hampotezi mama huyo mpaka pale alipomshuhudia akiingia ndani. Aliongeza mwendo na kuufikia mlango wa mama Burudani na kuvuta pumzi kwa nguvu huku akiiangalia mikono yake. Kisha alipeleka mkono kwenye swichi ya kengele ya ndani kwa mama Burudani lakini aliurudisha mkono baada ya kusikia mnyato wa mtu na haraka alijificha upande wa pili wa korido na kuchungulia alikotoka kuona ni nani huyo aliyekuwa akija.

"Shiiiit huyu mwanaharamu kafuata nini tena?" Alijisemesha mwenyewe baada ya kumuona Herieth akibonyeza swichi ya mlangoni kwa mama Burudani. Hivyo aliona akaona liwalo na liwe kama mbayi na iwe akamfuata pasipo kumuona kabla hajafanikiwa kuingia ndani baada ya mlango kufunguliwa alimziba mdomo huku akiikusanya mikono ya Herieth nyuma.

"Tunaweza kuingia wote."

"Hebu niache nani wewe?"

"Naitwa Mzimu."

"Mzimu??"

"Ingia ndani wewe acha maswali yako."

"Catherine!!!" Alishangaa baada ya kumuona ni Catherine.

"Kuna nini?" Mama Burudani aliuliza lakini bahati mbaya hakukutana na jibu la swali lake bali alikutana na teke moja takatifu la tumbo lililompeleka chini na kuangukia ndani akipiga kelele, Catherine alimsukumia Herieth ndani pia kisha akaingia na kuufunga mlango kwa ndani.

"We binti umepatwa na nini ulikuwa mlangoni kwa Herieth na sasa kwangu kuna nini?" Mama Burudani aliongea akijivuta nyuma.

"Catherine umekuaje?" Herieth naye aliuliza akijaribu kusimama lakini Catherine alimpa msaada wa kusimama naye akajiachia akijua kuna mazuri. Kabla hajakaa sawa alikutana na mtama murua uliompeleka chini na kumuangukia mama Burudani ambaye jina lake halisi ni Carolyn Othello.

"Mimi siyo yule Catherine mliyemuona mchana akiwa mpole na mnyenyekevu kiasi cha kupigwa hivi na Machangudoa wenzenu muda mfupi uliopita, mimi ni Catherine Mkono wa Mauti ambaye huwa nikinyoosha mkono huwa haurudi nyuma kifupi mimi ni Mzimu usiokamatika na yeyote."

" Unataka nini kwetu?" Herieth aliuliza akimwaga machozi kama chemchem.

" Vizuri Herieth, nikitakacho kwenu mnakifahamu vizuri lakini acha niwaambie, nahitaji cheki na keshi."

"What do you mean mother.... ky?" Madam Carolyn akiwa amemkamata mguu na kuung'ata alimuuliza.

"Unanitusi mimi wewe Changudoa mzoefu?" Alimuinua na kumpiga ngumi ya pua iliyopelekea kuanza kumwaga damu mfululizo kitu kilichomuogofya Herieth aliyekuwa akijivuta nyuma kuhofia kufanyiwa kitu mbaya na Catherine.

"Wewe hapo kusanya simu zenu weka hapa." Akimnyooshea mkono. "Na wewe hapo fanya kama nilivyokuambia haraka." Aliwaambia mama Burudani (Carolyn Othello) ambaye pua na mdomo vilikuwa havitambuliki kutokana na kutapakaa damu aliyokuwa akiisambaza kwa mkono wake maana hata uwezo wa kuchukua kitambaa hakuwa nao.

"Nimeeleweka?" Alimuuliza tena Carolyn ambaye aliitikia kwa kichwa na kujivuta mpaka karibu na droo ya kitanda.

"Unataka kufanya nini hapo?"

"Humu kuna keshi nimeihifadhi huwa siweki benki hela zangu."

"Nipe funguo hapa unataka kuleta jeuri yako kwangu?"

"Funguo hiyo hapo kwenye simu."

"Una maanisha nini?"

" Simu yangu ndiyo funguo ya droo yangu."

"Na kwanini ulikuwa unaisogelea ulitaka kuifungua na nini?" Catherine alimuuliza akiipekua simu yake.

"Kuchanganyikiwa tu nisamehe bure."

"Toa 'password' yako." Alimsogezea simu.

"Andika Big Mama kwa herufi kubwa itafunguka." Alimuelekeza kisha Catherine akafanya hivyo itafunguka na moja kwa moja akaikuta app yenye jina 'my bed' na kuifungua akakutana na sehemu inayoonesha ufunguo akaigusa ikafunguka kisha ikahitajika 'password' akamgeukia tena mama Burudani.

" Password yake ni ipi?"

"Weka imoji ya kipanya."

"Iko wapi?" Catherine alimuuliza baada ya kukutana na namba namba tu hivyo akajua anadanganywa.


JE NI NINI KITATOKEA KATIKA JUMBA LA MAMA BURUDANI?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO #storytelling #story #storytime #stories

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post