IMETOSHA MAMA MKWE - 39
sultanuwezotz.blogspot.com
Kweli hizi simu zina wazimu aisee yaani masaa zaidi ya mawili lakini utafikiri nimetumia dakika kumi tano tu na ninachojiuliza hivi na wao waliotengeneza simu wanatumia kama sisi au ndiyo kulaza bongo zetu na wao kusonga mbele kiuchumi. Baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa ndani ya Jirafu nilifunga mlango na kuingia zangu kulala. Kutokana na akili kuchoshwa na mionzi ya simu nilipojiegesha tu kitandani nilikuja shituka ni saa moja asubuhi na penyewe ni baada ya mama kuniamsha.
Mwanangu Thobias aliruhusiwa kutoka Hospitali akiwa kakaa siku nne za kupata matibabu akiwa na afya tele. Pia Jofrey na ndugu zake walifika nyumbani kama walivyoahidi na kukamilisha taratibu zote za kuniposa na baadaye tulifunga ndoa mkoani Rukwa mimi na mchumba wangu Jofrey na kisha tulianza masomo yetu ndani ya chuo cha ualimu St. Aggrey Mbeya. Japo safari ilikuwa ni ngumu sana kimasomo na kimahusiano lakini tulisonga mpaka pale ambapo tulifanikiwa kuhitimu Kozi yetu ya Ualimu. Kama unavyojua kwa kipindi hiki ajira ni tatizo hivyo baada ya kuhitimu tulibaki mtaani kwa miaka miwili huku tukiwa tunafanya biashara ndogo ndogo ndani ya jiji la Mbeya ambazo tulizianza toka tuko chuoni mimi nikijihusisha na biashara ya utoaji na utumaji pesa (Mpesa, na mitandao mingine) huku mume wangu akiuza nguo za mitumba akiwa ndani ya soko la SIDO Mwanjelwa na yote hii ilikuwa ni kwa msaada wa Mdogo wangu Rachel. Tulipambana sana mpaka pale ambapo serikali ilipotangaza ajira na sisi kama bahati vile tukawa miongoni mwao huku mume wangu akipangwa mkoani Tabora na mimi nikienda mkoani Njombe. Hapo ndipo safari mpya ya maisha na ajira yakianza huku kila mmoja akiwa mkoa mwingine. Wazazi wangu walinisaidia kwenye baadhi ya vitu kabla ya kuelekea mkoani Njombe ambako nilipangwa katika wilaya Wanging'ombe ndani ya mji mdogo wa Ilembula.
"Mke wangu unaendeleaje na majukumu?" Aliniuliza mume wangu Jofrey siku moja jioni nikiwa njiani kutoka kazini kuelekea nyumbani.
"Mungu anasaidia naendelea vizuri japo changamoto hazikosekani." Nilimjibu.
"Mhh mbona ni kama vile unahema sana uko njiani nini?" Aliniuliza baada ya kuona naongea kwa tabu kidogo.
"Ndiyo niko njiani na kibarabara nilichopita kina kimuinuko kiasi."
"Oohh pole sana basi fika kwanza nyumbani kuna jambo nataka tulizungumze."
"Okey sawa mume wangu." Nilimjibu lakini wakati huo nilikuwa niko ndani ya duka la jirani yangu kwa ajili ya kununua mahitaji kidogo. Nilitoka dukani hapo na kuikamata njia inayoelekea nyumbani lakini mara nikasimamishwa na bibi mmoja ambaye sikuwahi kumuona hata siku eneo lile na sehemu nyingine yoyote ile kifupi ilikuwa ni sura ngeni machoni pangu.
"Ndiyo bibi shikamoo!!" Nilimsalimia bibi huyu.
"Marhaba mjukuu wangu, hujambo?"
"Sijambo bibi naomba nikusikilize maana nina haraka kidogo." Nilimjibu.
"Mwalimu mbona una haraka hivyo unajua nimekusimamishia nini?" Aliniuliza na kujikuta naishiwa pozi.
"Samahani bibi yangu nimekosa."
"Bila shaka hujawahi kuniona popote pale japo mimi ninakufahamu vizuri sana, ila tuachane na hayo inawezekana ukanipuuzia kwa maneno yangu."
"Kwanini nipuuze bibi yangu mbona nimekuomba msamaha?"
"Ndiyo umeomba lakini nikiuangalia moyo wako nauona bado umesinyaa hivyo naona nisikucheleweshe sana mimi shida yangu ni kukuomba hata kamia tano tu ili kagaloni haka kakaingie tuulanzi pale kwa mzee Mwilave." Yaani nilichoka baada ya kuambiwa shida yake bibi huyu ambaye nilijua sijui ana jambo gani kwa namna ambavyo alinisimamisha.
" Bibi yaani mbwembwe zote hizo kumbe shida yako ilikuwa shilingi mia tano tu ya ulanzi? Usinifanyie hivyo bibi yangu." Nilimjibu.
"Ni hivyo tu mjukuu wangu ila kama utaniongeza pia nitashukuru." Alinijibu huku mimi nikiwa nimekwazika sana lakini nifanyaje imeshatokea hivyo nilifungua pochi yangu na kutoa noti ya shilingi elfu moja na kumkabidhi.
"Nakushukuru sana mjukuu wangu na samahani sana kwa kukuchukulia muda wako na kuanzia leo mimi ni rafiki yako umenisaidia leo kesho huwezi jua itakuwa ni zamu ya nani." Alinishukuru akiubusu mkono wangu.
"Sawa bibi naomba nikuache kuna mtu namuwahi nyumbani."
" Wewe nenda tu na mimi ngoja niwahi foleni kwa mzee Mwilave."
" Sawa bibi." Nilimjibu kisha tuliachana yeye akiishia huko kwa mzee Mwilave na mimi kiguu na njia kuelekea nyumbani, nilipofika tu kabla ya kufanya chochote kile niliona nimpigie kabisa simu mume wangu mengine yafuate.
" Umeshafika nyumbani?" Aliniuliza.
"Ndiyo nimefika muda huu kuna sehemu nilipata mara moja."
"Kuna sehemu ulipita?" Alipata wasiwasi kama kawaida yake.
"Umeanza mambo yako kwa hiyo unataka kusema nini?" Ilibidi nimbadilikie maana namfahamu vizuri mwanaume huyu.
"Si ni kawaida yako Tina nikigusa kwenye ukweli tu unakuwa mkali kwa hiyo unataka niwe nakaa kimya wakati nina uhakika kale kakijana ka siku ile kwenye mahafali pale chuoni hakajaacha kukufuatilia." Kauli hiyo ilinifanya nipandwe na hasira kiasi cha kumkatia simu ni mtu gani asiyekua kila siku tuhuma tu maana kama ni suala la Salehe Mabena tulishalizungumza na kulimaliza kwani nilishamweleza kuwa mtu huyo alikuwa akinitaka kwa lengo la kunioa lakini nilipomwambia kuwa nina mchumba na ambaye kwa sasa ni mume wangu, namshukuru Mungu katika hilo alinielewa na kuniomba tubaki marafiki. Sikuona tatizo nilikubali na baadaye niliwakutanisha na Jofrey wakabadilishana mpaka namba za simu sasa hizo shutuma anazoniletea tena zinatoka wapi? Nilichukia sana na hapo hapo nikainuka na kuelekea bafuni kuoga maana nilishavurugwa tayari na mtu asiyekuwa muelewa. Lakini kabla sijatoka chumbani kuelekea bafuni simu iliita lakini niliipotezea kwani nilijua si mwingine bali ni Jofrey hivyo nikachukua zangu maji kwenye kindoo na kuingia bafuni ambako niliweza kuoga maji ya baridi ambayo yaliweza kunichangamsha mwili na kisha nilirudi ndani.
Nilipoingia nilikutana na simu ikiita na baada ya kuiangalia niliiona namba ya Jofrey nilitaka kuipotezea lakini nikaona niipokee.
"Kwanini ulinikatia simu?" Aliniuliza nilipoipokea simu.
"Unauliza swali?"
"Ndiyo nauliza na ninahitaji jibu."
"Nisikilize wewe mwanaume kama hauna la kuongea na mimi nitakukatia simu sasa hivi ohhoo." Nilimjibu.
"Haya bwana naomba tuachane na hayo maana wewe huujuagi hata utani." Aliona ajitetee sasa baada ya kuona nimemkazia.
"Utani gani huo?"
"Nisamehe bwana."
"Nimeshakusamehe tayari wewe ongea kile ulichotaka kunieleza."
"Nashukuru kama umenisamehe mke wangu sasa kuna kitu naomba unisaidie mke wangu."
"Kitu gani hicho Jofrey?" Nilimuuliza.
"Nafikiri unakumbuka siku kadhaa nyuma nilikwambia tatizo la mama kule kijijini."
"Ndiyo nakumbuka kuna nini?" Nilimtupia swali.
"Ni hivi juzi tu kundi la watu limemfuata wakitaka kumuua."
"Kumuua? Kwa kosa gani?" Nilimuuliza.
"Wanamshutumu kuwa ni mchawi sijui kuna mama gani pale mtaani kwake walirushiana matusi ya nguoni na yenye vitisho, kilichotokea ni kuwa yule mama kafariki akiwa anajifungua hivyo zigo lote limekwenda kwa mama."
"Unajua nini mume wangu?"
"Ndiyo mke wangu." Aliitikia.
"Mimi nilishakueleza mambo ambayo nilifanyiwa na mama yako mkubwa Bi Kiziwa pale Mbeya lakini wewe hukuniamini ukasema nina chuki na mama yako ambaye hujawahi kusikia kama ana tabia hizo nilikuomba msamaha leo yako wapi? Mama yako naye amekutana na kisanga, kwa hiyo unataka kusema nini?"Nilimuuliza swali.
" Mke wangu kwanza unatakiwa kuelewa kuwa hukumu tangulizi jazifai katika jamii hivyo kukubaliana na mambo yanayozungumzwa kwa chuki tu siyo vizuri hata kidogo na pia unatakiwa kukumbuka kuwa yule ni mama yangu...." Alishaanza kupandisha mashetani yake hivyo nikaona nimtulize.
" Mume wangu sijazungumza kwa ubaya na kama nimekosea naomba unisamehe halikuwa kusudio langu."
" Nimekusikia lakini wakati mwingine unatakiwa kuwa makini na maneno yako."
" Nimekuelewa mume wangu kipenzi." Niliendelea kujishusha ili ajione mshindi.
"Nilichokuwa ninataka kukuomba ni juu ya suala la mwanangu Marygoleth."
"Kafanya nini?" Nilimuuliza maana nilianza kuhisi kipi anataka kuzungumza. Marygoleth ni mtoto wake Jofrey ambaye alizaa na msichana wake wa utotoni huko kwao Sumbawanga na kwa sasa alikuwa akiishi na mama yake Jofrey baada ya mama wa mtoto kutorokea jijini Dar es Salaam.
"Nilikuwa nakuomba umchukue ukae naye wewe asije patwa na tatizo lolote lile maana kama mama ameshabatizwa jina la mchawi unafikiri nini kitatokea?" Aliniuliza.
" Mimi sijui na kwanza halinihusu hata kidogo kwani shangazi zake si wapo kwanini asipelekwe huko uniletee mimi ili baadaye nionekane namnyanyasa."
"Mama Thobias naomba unisikilize kwanza." Alinituliza.
"Unataka kusema nini?"
"Mimi ni nani kwako?" Aliniuliza.
"Ni mume wangu."
"Sasa kama ni mume wako kwanini hutaki kunielewa?"
"Suala siyo kukuelewa, kuna mambo ya kukuelewa na kuna mengine hapana kwa hilo ongea na ndugu zako lakini siyo mimi naomba unisamehe sana mume wangu." Nilimjibu pasipo kupepesa macho. Na ni kama vile alichukia hivi kwani aliamua kukata simu. Na mimi sikujali hilo nilitoka sebuleni kuendelea na shughuli zangu leo nikae na mtoto wake ili kesho nionekane namnyanyasa aa wapi. Nilichukua jiko na kuweka mkaa kisha nikachukua kijembe na kwenda kuomba moto kwa jirani yangu mama Raymond.
"Mama Raymond."
"Karibu mwalimu."
"Asante dada yangu pole na majukumu."
"Yanakwenda mwalimu si unajua tena ukilemaa tu familia yako itaishia kuwa ya wazururaji tu mtaani hivyo ni lazima wazazi tuwajibike wakati bado tu hai."
"Ni kweli kabisa dada yangu nakumbuka mama yangu siku moja aliniambia kuwa ukikosea malezi kwa mtoto hilo doa mpaka kaburini."
"Alikuwa sahihi kabisa katika hilo."
"Ndiyo hivyo dada yangu."
"Mbona na kijembe mkononi?" Aliniuliza.
"Nahitaji moto."
"Yaani ukakoleze muda huu halafu upike saa ngapi?" Aliniuliza.
"Ni maandalizi ya usiku mchana sisi tunakula shuleni."
"Unaonaje ule tu hapa maana mimi chakula nimepika kingi halafu kama ujuavyo Raymond kasafiri kwenda Morogoro kwa baba yake hivyo niko mwenyewe tu hapa."
"Kwa hiyo tumekutana mabachela leo?" Nilimuuliza.
"Kama kawaida hivyo mabuzi leo ruksa." Mama Raymond aliongea kwa kujiachia kabisa.
"Kabisaa?" Nilimuuliza.
"Mwalimu kwani tatizo liko wapi katika hili?" Majibu yake yaliniacha hoi nikajikuta nikiomba tu anipe moto nikajipigie mwenyewe chakula masuala ya mabuzi akuu.
JE NINI KITAENDELEA TINA ATAUKWEPA MTEGO WA MAMA RAYMOND?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.
#SULTANUWEZO