NITAKUUA MWENYEWE - 49
sultanuwezotz.blogspot.com
Ndani ya Hospitali ya Makambi iliyo ndani ya mji wa Windhoek madaktari walikuwa kwenye kikao kizito juu ya wagonjwa watatu ambao ni Jackline, Jessica na Jasmine ambao mpaka wakati huo walikuwa bado hawajazinduka pamoja na juhudi zao zote za kuwahudumia. Mkurugenzi mkuu wa Hospitali hiyo ya Makambi bwana Hans Murray aliamua kufanya maamuzi mazito juu ya hili.
"Kwanza niwapongeze kwa juhudi zenu zote mlizozionesha kwa hawa wagonjwa tulioletewa kutoka Namport kuanzia siku ya kwanza mpaka leo hii tunapowajadili, kitu kimoja ninataka kukifanya juu yao kwani naliona kama jaribu kwetu na iwapo hatutalishinda jaribu hili tutaupoteza umaarufu wetu na Brand yetu itashuka na kupotea kabisa wataalamu wangu hivyo katika kuliona hili nimeamua kuwaleta Madaktari Bingwa kutoka Ujerumani ambao wamebobea zaidi kwenye mfumo mzima wa mwanadamu huenda watatusaidia kubaini tatizo linalowakabili." Alifafanua Mkurugenzi.
Wakati kikao hicho kikiendelea baina ya madaktari na Mkurugenzi wao mara aliingia Nesi wa zamu kwenye chumba cha wakina Jackline na kuleta taarifa ambayo ilipelekea kusimama kwa kikao hicho huku kila mmoja akishika njia kuelekea chumbani kwa wakina Jackline na katika hilo mpaka Mkurugenzi bwana Hans Murray akishika njia mbio mbio kuelekea huko chumbani.
"Jamani ni kweli huyu hapa kafumbua macho."
Daktari mmoja aliongea kwa mshangao baada ya kumkuta Jackline akiwa kafumbua macho yake huku akiangalia huku na kule bila shaka mazingira yalimchanganya kidogo.
"Wataalamu nawaombeni tupungue kidogo ili kutoa nafasi kwa mgonjwa kutuliza akili yake kwani hapa bado anayashangaa mazingira hivyo uwingi wetu ndiyo unamchanganya kabisa, nafikiri abakie daktari husika na nesi mmoja wengine tukaendelee na majukumu mengine."
Mr Hans Murray aliwaomba wafanyakazi wake kupungua mle ndani ili kumpa nafasi Jackline ya kujenga kumbukumbu vizuri ya matukio ya nyuma kisha naye aliondoka.
" Bila shaka leo kutakuwa na taarifa nzuri kutoka kwako kaka Hans."
Daktari Abbas Mukesh aliongea baada ya kuipokea simu ya rafiki yake daktari na Mkurugenzi mkuu wa Makambi Hospital bwana Hans Murray.
"Naweza sema hivyo rafiki yangu huwezi amini dakika kumi zilizopita mgonjwa mmoja yule ambaye ni mwembamba kafumbua macho tayari ikiwa ni kama dakika kadhaa tukiwa kwenye majadiliano ya kuongeza nguvu kwa kuleta wataalamu wengine kutoka Ujerumani kwa gharama zetu ili kuilinda Brand yetu tuliyoitengeneza kwa muda mrefu."
"Brother unachokiongea ni kweli au umeamua tu leo kunijaza?"
Daktari Abbas Mukesh aliuliza baada ya kukaa kimya kwa muda akimsikiliza tu daktari Hans Murray.
"Nataniana sana na wewe Abbas lakini kwenye kumbukumbu zako unaweza kuniambia ni lini niliwahi kukutania mida ya kazi?"
"Kwa hilo nikiri halijawahi tokea kaka." Daktari Abbas alikiri.
"Sasa iweje leo niuvae ujasiri huu wa kuinua simu na kukupigia kisha kukueleza taarifa za uongo?"
"Kulingana na jambo lenyewe lilivyochukua muda mrefu nilianza kupoteza matumaini ya kupona kwao na ndiyo maana ulivyonieleza tu nikajua unanidanganya,nisamehe bure kaka."
"Aaah achana na hizo dogo lakini weka akilini kuanzia sasa kuwa mgonjwa wa kwanza keshaamka tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awatendee miujiza na hawa wengine wazinduke usingizini."
"Nashukuru sana kwa taarifa hizi ambazo naweza kusema ni spesho kwangu kwa siku ya leo, kesho mapema nitakuwa hapo kwa lolote litakaloendelea tujulishane kaka wala usichoke."
"Tulikubaliana toka awali na itakuwa hivyo mpaka mwisho mdogo wangu daktari Abbas."
"Mungu akubariki wewe na timu yako ya Madaktari kaka."
"Na wewe pia iwe hivyo."
"Shukrani sana."
Baada ya simu kukatwa daktari Hans aliingia ofisini kwake akaketi kitini kwake na kuipandisha miguu yake juu ya meza akiwa anaigongagonga mikono yake aliyoikunja mdomoni, kama haitoshi ni kama alikumbuka kitu aliinuka na kutoka nje ya ofisi yake na kuelekea kule kwenye kile chumba walicho wakina Jackline.
"Samahani kaka wewe ni nani na hapa ni wapi?"
Ni swali alilolikuta likitoka kinywani mwa Jackline akimuuliza daktari yule aliyekuwa akimuhudumia. Ilibidi abakie pale pale mlangoni ili asikie mgonjwa wao yuko katika hali gani ya utambuzi.
"Naitwa Daktari Ramadhan na yule pale mezani ni nesi anaitwa Mariam." Daktari Ramadhan alijitambulisha.
"Daktari, Nesi..." Alirudia tena kutaja tambulisho hizo akiwa kama anakumbuka kitu hivi.
"Ndiyo sisi ni wahudumu wa hospitali hii ya Makambi."
Aliongeza Nesi Mariam aliyekuwa akimuandalia maji ya glucose.
"Nilifikaje fikaje hapa hospitali rafiki zangu Jasmine na Jessica wako wapi?" Jackline aliuliza.
"Pumzika kwanza dada yangu ukiwa sawa kila kitu utakifahamu."
Daktari Ramadhan alimjibu hivyo baada ya kumuangalia bosi wake aliyetoa ishara ya kutomwambia kitu kwanza.
"Daktari unafikiri mimi ninaumwa? Siumwi hata kidogo bali nilizimia tu baada ya kuvuta hewa yenye sumu, kwanza Robinson na wenzake wako wapi? Kwa akili zenu utashangaa kuona mmewaachia."
Jackline alipoona kama vile anataka kufichwa ukweli aliwahakikishia kuwa yeye si mgonjwa na kitendo cha kulitaja jina hilo pamoja na sumu ndipo wakahisi inawezekana ulikuwa ni ugomvi wa kimapenzi.
" Nakuomba kunywa maji haya kisha pumzika kwanza..... " Nesi Mariam alimuomba Jackline.
"Kitu kimoja tu ili nitulie nahitaji kukifahamu kutoka kwenu Jasmine na Jessica wako hai? Na wakina Robinson wamekamatwa?"
"Dada yangu hao ndugu zako ni wazima kabisa na hao wengine wako chini ya vyombo vya dola."
Baada ya kusikia hayo kutoka kwa Nesi Mariam, Jackline alipokea ile glasi ya maji akanywa na kisha akamrudishia Nesi kilichofuata alijigeuza na kulala.
Walimfunika vizuri kisha wakaviendea vitanda vya Jasmine na Jessica vilivyokuwa vimezungushwa mapazia ya rangi kuangalia kama kuna mabadiliko kwenye hali zao.
"Huyo tayari yuko vizuri kwani kwa kitendo cha kulikumbuka tukio la mwisho ni ushahidi tosha kwetu kuwa yuko vizuri, cha kufanya ni kumfanyia mpango wa lishe kisha tutapata utambulisho wao hapo kesho."
Daktari Hans alizungumza hayo baada ya kuingia kwenye vitanda walivyolazwa wakina Jessica na Jasmine ambako hata Jackline naye alikuwa huko lakini baada ya mabadiliko hayo alitolewa.
" Mkuu tunaweza kuzungumza kidogo? "
Daktari Ramadhan alimuomba bosi wake daktari Hans Murray. Aliomba wakati huo Nesi Mariam alikuwa akiwafunika vizuri wagonjwa wake.
"Daktari Ramadhan bila shaka tunaweza tu kama ni hapa au nje ni wewe tu."
Daktari Hans Murray alimkubalia Daktari Ramadhan hivyo walitoka nje ya chumba hicho na kuelekea kwenye bustani ya maua ya Hospitali hiyo na kuketi kwa mazungumzo.
"Naomba nikusikilize Mtaalam wangu."
"Nashukuru sana bosi, kuna wazo ambalo nimelipata tukiwa mle ndani."
"Wazo gani hilo Rama?"
"Ni juu ya yule binti kwa namna nilivyomuona nimebaini kuwa kuna magumu mengi ambayo kayapitia hivyo nikaona niongee na wewe uweze kuongea na mzee yule aliyewaleta ikiwezekana tumpeleke kwenye Kituo chetu cha Saikolojia na Utimamu wa Akili ili tuweze kuwajenga." Daktari Ramadhan alimweleza bosi wake wazo lake.
" Nashukuru kwa kuliona hilo hivyo ngoja nifanye mpango wa kuwasiliana na rafiki yangu aliyewaleta huku bwana Abbas Mukesh yeye itakuwa rahisi zaidi kuongea na mzee Jerome Whistle akifanikiwa kuhusu Kituo haina shida ni chetu kile lakini wakati huo huo unatakiwa kujua kuwa mwenye maamuzi ya mwisho ni mhusika mwenyewe alikubali sawa lakini pia akikataa ni haki yake."
Daktari na Mkurugenzi mkuu wa Makambi hospitali bwana Hans Murray alikubaliana na Daktari Ramadhan lakini alitoa tahadhari pia.
Upande wa Jackline akiwa kajilaza pale kitandani mara mtiririko wa matukio ulianza kupita kichwani kwake kitu kilichomfanya kupiga kelele ambazo ni kama ziliamsha tukio ambalo halikutarajiwa na madaktari wote kiasi cha kubakia midomo wazi.
"Nasema haiwezekaniiiiii hata kidogo tunarudi tena ulingoni, wanajeshi wangu amkeeeeeniiiiiiiii..............!"
"Samahani dada tafadhali, pumzika hujapona vizuri."
Nesi Mariam alimuomba Jackline ajipumzishe baada ya kumkuta akipiga makelele.
"Bora umekuja Nesi kabla ya yote nieleze hii hospitali iko wapi?" Jackline alitokwa na swali.
"Hii ni hospitali ya Makambi iliyoko Windhoek....."
"Ina maana hapa ni Namibia? Mungu wangu nimefikaje hapa mimi?"
" Uliletwa na mzee mmoja hivi anaitwa mzee Jerome akiwatoa hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE bila shaka huyo anafahamu mlifika vipi hapa nchini."
"Santanaaaaaaaaaaaaa.......................!!! Am back jiandae."
"Saa...samahani dada yangu nimekusikia ukiyataja taja majina kadhaa mara Robinson mara Santana hawa ni wakina nani?" Nesi Mariam alimuuliza Jackline baada ya kuona akitaja jina Santana kwa hasira zaidi.
"Tuko wapiiiiiiiiiiiii........."
Sauti zilitoka kule walikokuwa wakina Jasmine. Nesi Mariam alichanganyikiwa akajikuta badala ya kwenda zinakotoka zile kelele yeye alitoka mbio kuelekea ofisini kwa Dakika wa kitengo huku nyuma akabakia Jackline ambaye naye alizisikia zile kelele na hivyo alishuka pale kitandani na kuelekea kule kwenye mapazia.
"Jasmine, Jessica na ninyi mko mahali hapa? Tumefikaje hapa?" Jackline aliongea akiwa kawakumbatia wenzake ambao alijua katengana nao.
"Melissa yuko wapi? Na vipi kuhusu wakina Robinson na mzee Bruno Gautier?" Jessica aliuliza swali akiwaangalia wenzake.
"Jessica achana na maswali hayo kifupi hapa hatuko Brazil tena nimeambiwa na Nesi...."
"Subiri kwanza Jackline unasema hatuko Brazil tuko wapi sasa?" Jasmine alijikuta akiuliza.
"Hapa tuko Windhoek Namibia." Jackline alijibu.
"Namibiaaaa !!!!!" Walijikuta wakiuliza kwa pamoja.
"Sikilizeni mwenzenu mpaka muda huu nimefanikiwa kuwahadaa hivyo na ninyi fanyeni hivyo ili tubaini lengo lao sawa?"
Jackline aliwaambia hivyo wenzake ambao hawakuelewa alimaanisha nini.
"Waooo kama zali vile wamezinduka wote sasa na hili litapelekea hospitali yetu kujipatia umaarufu."
Daktari Ramadhan alizungumza baada ya kuwakuta wakina Jasmine nao wamezinduka.
"Samahani daktari leo jumangapi?" Jasmine aliuliza swali.
"Leo ni Juma......" Kabla hajamalizia sentensi yake alijikuta akitemewa mate usoni na Jessica.
"Si niliwaambia kuwa noo...., sorry kumbe haukuwa wewe nilishasahau kuwa niliongea na Mkurugenzi mwenyewe."
Daktari Ramadhan alijikuta akitokwa na maneno yasiyo na utaratibu.
"Dokta mbona sikuelewi? Unasema hukuongea na mimi kitu gani?" Nesi Mariam alimuuliza.
"Okay, okay namaanisha kuwa niliongea na Mkurugenzi kuwa hawa wagonjwa tutatakiwa kuwapeleka kwenye Kituo maalum cha Saikolojia kwa ajili ya kuwajenga Kisaikolojia hawako vizuri kiakili si umeona walichokifanya?"
Wakati Daktari Ramadhan akiongea hayo wakina Jackline wenyewe walikonyezana kama ishara ya kuanza kuishinda baadhi ya mitihani.
" Samahani daktari unaweza kutupeleka Gereji?" Jackline alimuuliza daktari Ramadhan.
" Gereji?? "
" Ndiyo...!!! "
" Kufanya nini huko Gereji tena?" Aliuliza Nesi Mariam.
"Hamuoni mwenzetu hapa mguu wake umewekwa rangi nyeupe hivyo inatakiwa akafanyiwe usafi na marekebisho."
Jackline alijibu na kuwafanya wale wahudumu kujivuta pembeni kidogo ili watete.
"Daktari hivi unawaelewa vizuri hawa wagonjwa?" Nesi Mariam alimuuliza daktari Ramadhan.
"Mhh hata sina la kuongea hebu twende kwa bosi kwanza na pia itafute namba ya yule mzee mweleze kuwa watu wake tayari wamezinduka ila hawako sawa kiakili." Sawa Daktari.
"Simnaona huu mchezo? Mmeuelewa maana yake?" Jackline aliwauliza wenzake.
"Wala mimi sijaelewa hata moja." Jasmine alijibu.
"Mimi ndiyo kabisaaa sijamuelewa." Jessica naye alijibu.
"Ni hivi jamani kama nilivyowaambia kuwa huku tuko Namibia na hapa ni hospitali, kama mnakumbuka tukio la mwisho lilikuwa ni lile la pale kwa Melissa lililofanywa na wakina Robinson ambalo lilipelekea sisi kupoteza fahamu zetu hivyo hamuwezi kujua iwapo ni mchezo wa Santana huu hivyo hapa tunatakiwa kuondoka haraka sana ila kwa muda huu ambao bado hali zetu haziko sawa maigizo yawe ni asilimia mia moja." Jackline aliwafafanulia.
" Okeeeey Hapo nimekuelewa dada yake."
Jessica alimjibu.
" Tuko pamoja tunatakiwa tusiwape nafasi ya kutujua undani wetu."
Jasmine naye aliungana nao.
Mara waliwasikia Madaktari wakija mle ndani hivyo kila mmoja alikimbilia kitanda chake.
JE NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
#SULTANUWEZO