MUUAJI MWENYE BARAKOA - 30 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 30

sultanuwezotz.blogspot.com 


Catherine akaona ashuke kwenye gari na kujificha ili ajue askari huyu anamfuatilia kwa lengo gani. Alifunga mlango baada ya kushuka kisha akaingia uvunguni mwa gari na kutulia kimya akimsubiri adui yake huyo ambaye alifika na kusimamisha pikipiki yake kisha haraka akalisogelea gari na kuchungulia ndani ya gari ambapo hakuona mtu ikabidi aufungue lakini haukufunguka aliangaza huku na kule lakini hakuona mtu, akaegemea gari la Catherine na kutoa simu yake ambayo aliipiga.

"Mkuu huyu mwanamke kaacha gari hapa lakini yeye hayupo sijui ameingia wapi?" Alitoa taarifa kwa mtu huyo aliyemuita mkuu huku Catherine akifuatilia kile kilichokuwa kinazungumzwa na askari huyo.

"Unajua nini mkuu kumeanza kupambazuka na mimi nina mishe zangu za kifamilia hivyo ili niendelee kumfuatilia mtu wako hakikisha unaongeza unene wa fuko tofauti na hapo itakuwa ngumu." Askari huyu aliendelea kujieleza.

"Mmhh kwa hiyo huyu siyo Askari kama alivyojitambulisha kwangu eee!!" Catherine alishangaa mara baada ya kuyasikia mazungumzo ya mtu huyo hivyo akatoka uvunguni mwa gari na kutokea upande wa pili na kuanza kumnyatia pale aliposimama.

"Unatuma sasa hivi? Hayo ndiyo mambo wacha na mimi niendelee kumtia presha." Alimaliza kuongea na simu akakivutavuta kitasa cha mlango kwa mara nyingine lakini hali ikawa vile vile akiwa anajiandaa kugeuka upande wa pili alikutana na ngumi ya shavu iliyompeleka mpaka chini akataka kuinuka kukabiliana na Catherine lakini akawa amechelewa kwani alijikuta akichezea ngumi zisizo na idadi pale pale chini kiasi cha kujikuta anaona giza machoni japo kulikuwa na giza bado.

"Bwana Afande naomba utambulisho wako kabla sijafungua bucha hapa." Catherine alimwambia akiwa kamuoneshea bastola pale chini alipolala.

"Kama ambavyo nilikwambia mimi ni Askari Doria wa eneo hili nikitokea kituo namba 279." Alimjibu.

"Nipe simu yako."

"Ya nini tena dada? Mbona nimejibu swali lako." Alimjibu akiingiza mkono mfukoni kutoa simu.

"Nakusikitikia kijana kwa kuingia kwenye anga zangu unajua nini? Mara nyingi wanaoingia huwa hawatoki salama hivyo anza kusali yasikukute haya ninayokuwazia." Catherine alimwambia akiikagua simu ya askari huyo na kwa kuwa mwanga wa simu ulimmulika machoni Askari uchwara akaona nafasi ndiyo hiyo aliinuka na kutoka mbio, Catherine akatoka mbio kumfukuzia. Waliingia mitaani huku Catherine akimtaka ajisalimishe kabla hajamfyatulia risasi lakini kijana huyo hakuwa tayari kujitoa kafala aliendelea kujaribu bahati yake na baada ya kuona Catherine anamkaribia alianza kupiga kelele za mwizi ambazo ni kama zilimtia wazimu Catherine akamfyatulia risasi kama mbili za mgongoni kisha akaachana naye na kurudi mbio kwenye gari lakini kabla ya kuingia kwenye gari aliichukua pikipiki na kuisukumia korongoni kisha akarudi na kuingia kwenye gari na kuondoka.

"Mjomba hayupo mbali na mimi na ndiyo maana kamhonga huyu askari asiye na maadili ya kazi kunifuatilia nikokwenda au kunichelewesha safari yangu na hapa nina mashaka kuna sehemu anakwenda."Akiwa anafikiria haya akapata wazo la kuangalia kama simu yake ina ujumbe wowote kutoka kwa rafiki yake Uriah.

" Haya ndiyo mambo." Alijikuta akiongea kwa sauti baada ya kuuona ujumbe ambao ulikuwa na namba ambayo aliomba aitafute. Hapo hapo aliingiza kwenye 'app' ambayo huitumia kunasia mawasiliano na 'location' ya mtu anayemhitaji akiwa kalisimamisha gari na muda huo kulishapambazuka.

"Mmh anaondoka hapa Nigeria?" Alijikuta akijiuliza swali baada ya kuiona namba ile ikiwa mpakani mwa Nigeria na nchi ya Niger.

"Huyu anaelekea Niger na kwa inavyoonekana ameshaiingiza namba yangu kwenye mfumo wake wa ufuatiliaji ndiyo maana imekuwa rahisi kunitumia mtu." Aliongea akiitoa laini ile na kuweka laini ya mtandao mwingine ambayo mjomba wake hajawahi kuwa nayo na baada ya kuona iko sawa alikaa sawa kwenye usukani akawasha gari na kuondoka.

" Mzee Malick nimeona umahiri wako sasa tuicheze pamoja staili ya samba." Aliongea Catherine. Na kwa kuwa kulishakucha akaona apitie kwenye Cafe moja ambayo aliiona eneo lile.

"Ngoja nipate kifungua kinywa kwanza ili mwili upate nguvu kabla ya kuelekea huko niendako." Catheline alijisemesha akiingia 'Princeton Cafe' ambapo alikwenda mpaka sehemu maalum ya kuegesha magari na kulipaki gari lake akashuka na kuingia ndani ambamo kwa muda huo hakukuwa na watu wengi sana hivyo alichagua meza moja ambayo haikuwa na mtu akaketi na kumuita mhudumu aliyekuwa akifanya usafi wa baadhi ya meza.

"Ndiyo dada naomba nikuhudumie tafadhali." Mhudumu huyo alimwambia baada ya kumfikia.

"Habari yako lakini." Catherine alimsalimia.

"Safi tu dada."

"Nimeona unakuja hata salamu utafikiri tumelala pamoja?" Catherine alimwambia mhudumu huyo ambaye alifika bila hata salamu.

"Naomba unisamehe dada yangu ni kujisahau tu wala siyo kawaida yangu." Alimjibu.

"Usijali nimekusamehe mdogo wangu najua changamoto mnazopitia kwenye shughuli hizi. Naomba uniletee supu ya kuku." Catherine aliagiza.

"Sawa dada yangu." Mhudumu huyo alijibu na kutaka kuondoka lakini Catherine alimshika mkono.

"Samahani mdogo wangu jina lako nani?" Mhudumu yule alimtazama kwa woga kutokana na alivyomchambua awali na kisha alijitambulisha.

"Naitwa Aminata Flamingo." Alijitambulisha.

"Waoo nafurahi kukufahamu mdogo wangu unaweza kuniletea agizo langu."

"Okay sawa." Aminata alimjibu na kuondoka. Catherine akiwa pale anasubiria supu aliyoagiza mara macho yake yakatua kwenye Luninga ambayo ilikuwa humo Cafe.

"Habari zilizotufikia hivi punde ni kwamba Mgonjwa ambaye alishambuliwa hivi karibuni ndani ya Hoteli ya Virgo amefariki dunia mapema leo, taarifa hii imetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi na kuongeza kuwa wameanza kufanya jitihada za kuwatafuta ndugu wa marehemu ambayo mpaka sasa hakuna ambaye alijitokeza. Endelea kuwa karibu na televisheni yako ili kujua kinachoendelea katika tukio hili.... " Taarifa hii ilimfanya Catherine kuduwaa kwa muda kisha aliangaza mle ndani kama kuna mtu ambaye anamuangalia na baada ya kuona hakuna alitoa simu yake na kuandika kitu fulani kisha akairudisha tena mfukoni.

" Karibu dada." Aminata alimkaribisha baada ya kuiweka mezani.

"Nashukuru Aminata."

"Maji ya vuguvugu ya kunawa yale pale." Aminata alimuonesha Catherine ambaye aliinuka na kwenda kunawa. Baada ya kunawa alirejea na kuketi akaanza kupata kifungua kinywa huku macho yake yakiwakagua waliokuwa wakiingia mle ndani kwa wizi ili kuangalia usalama wake.

" Siyo hivyo wewe taarifa ya jana inasema kuwa mtu aliyehusika na Mauaji hayo alionekana kwenye chumba cha usalama lakini akiwa kwenye sura mbili tofauti." Waliingia wakibishana wasichana watatu ambao walikuwa wakiizungumzia habari ile na kumfanya Catherine kutoinua shingo yake lakini akiwa ameyatega vizuri masikio yake.

" Hebu acheni hizo habari ndugu zangu msije sombwa kwenda huko kulisaidia jeshi la Polisi shauri yenu." Mmoja wao aliwatahadharisha wenzake.

"Tatizo lako Tahya ni muoga sana wewe yaani mimi mwenzenu wala sina hofu yoyote ile na walichokikosea ni kutokutoa picha ya muuaji yaani wangerogwa tu kuitoa na nilivyochacha hivi mbona ningehakikisha nakuwa mtu wa kwanza kumnasa." Alijinasibu mmoja wao ambaye Catherine alimtolea macho msichana huyo na bila shaka haikuwa kwa wema hata kidogo. Na baada ya kumaliza tu aliinuka na kumfuata Aminata pale kaunta na kumlipa hela yake kisha akaaga na kutoka nje ambako moja kwa moja alielekea kwenye gari akawasha na kuondoka zake.

"Ni habari njema sana kwangu hizi nafikiri moyo wangu utakuwa sawa nitakapomkamata Malick Bolenge na hatimaye Mchungaji Rodney Hauser ambao ndiyo walioyashikilia maumivu ya moyo wangu wenye kisasi." Akiwa umbali wa kama kilometa arobaini hivi akaona msululu mkubwa wa magari makubwa kwa madogo kitu ambacho kilimpa hofu na kumfanya kupunguza kasi na baadaye akasimama.

" Kinga ni bora kuliko kinga wacha nichukue tahadhari mapema." Alijisemesha akilichukua wigi lake na kulivaa kisha akachukua kioo kidogo ambacho hutembea nacho garini na kuanza kujiseti vizuri kisha akachukua miwani na kuivaa, alipojiridhisha yuko vizuri akaondoa gari na kuendelea na safari. Baada ya kufika eneo lile alisimamishwa na Askari wa kike ambaye alikuja na kuchungulia na baada ya kumuona ni mwanamke alimruhusu bila shaka walikuwa wakiwasimamisha wanaume tu kutokana na kundi lililokuwa chini pale hakukuwa na mwanamke hata mmoja. Alipita na kuendelea na safari yake huku macho yake akiyaibia pembeni kuangalia kinachoendelea pale. Alipokunja kona na kuanza kupandisha mlima aliona asimame kwanza hivyo aliipaki kando kidogo kisha akaenda mbele na kuegemea gari kisha akampigia simu Awadh.

"Habari Madam." Alimsalimu baada ya kupokea simu.

"Nashukuru niko salama japo Vizingiti ni vingi sana navivuka kibishi hivyo hivyo ila Malick kanishtukia ameikimbia Nigeria."

"Pole sana, sasa kaelekea wapi?" Awadh alimuuliza.

"Kwa ninavyomuona kwenye king'amuzi changu hapa anaelekea Niger."

"Niger? Sasa unafanyaje?" Awadh alimuuliza tena.

"Nitamnasa tu ninyi endeleeni kumshikilia huyo panya mpaka nitakapo rejea."

"Bila shaka Madam sisi tunakuombea ufanikishe lengo lako."

"Wala usijali huyu pimbi wa kijani keshaiaga dunia akiwa bado anaipenda."

"Nani huyo?" Awadh alimuuliza.

"Si huyu msaidizi wa Malick niliyemuotea na kumpa somo pale Hotelini." Catherine alimjibu.

"Amekufa?"

"Kitambo Awadh." Catherine alimjibu na kumtakia asubuhi njema kisha alikata simu ili kuipokea simu ya rafiki yake Uriah aliyekuwa akimpigia.

"Unasemaje mdogo wangu?" Catherine alimuuliza.

"Ndiyo naamka muda huu uchovu wa kutosha, uko wapi muda huu au ndiyo tayari umeanza kumsaka adui yako." Uriah alijibu.

"Kama mganga vile hivi ndiyo nautafuta mpaka wa Niger."

"Mpaka wa Niger? Usiniambie unaelekea Niger dada." Uriah alimuuliza.

"Ndiyo hivyo mdogo wangu naelekea huko huyu panya anakimbilia huko hivyo nimeona nimfuate huko huko nikampe zawadi yake ambayo ninaamini ataifurahia sana akiipata." Catherine alimjibu.

"Mmh mimi sina hata cha kuongeza kwenye hilo ila kuwa makini mijitu kama hiyo inakuwaga siyo mizuri." Uriah alimpa tahadhari.

"Nitajitahidi kuwa makini mdogo wangu." Catherine alimjibu akiingia garini baada ya kuisikia gari nyingine ikiunguruma nyuma yake.

"Basi safari njema dada." Uriah alimuaga na Catherine alikata simu na kuiweka kwenye 'dashboard' kisha mikono ikaukamata usukani na macho yake yakiwa kwenye 'site mirror' kabla ya kuingia barabarani na baada ya kuona kuna usalama aliingia na kuendelea na safari. Asubuhi hii kwenye mlima huu kulikuwa na baridi kali huku kukiwa na ukungu kwa mbali lakini haukuwa na madhara kwa Catherine kushindwa kuendelea na safari. Baada ya kuumaliza mlima ule alikutana na mji mdogo ambao ulijulikana kama Kabyakh kutokana na maandishi ya 'Karibu Kabyakh' yalivyosomeka kwenye bango kubwa alilolisoma Catherine. Aliangaza kuona kama anaweza kuona kituo chochote cha mafuta aongeze kwa kuwa hakuwa na uhakika baada ya pale kama anaweza kukutana na mji mbele na kama bahati vile aliweza kukiona.

"Afadhali maana hiki kimlima kimenikombea mafuta yangu." Aliongea akikata kona kuingia pale kituo cha mafuta. Aliliingiza gari mpaka kwenye moja ya pampu ya mafuta na kusimama kisha akaja mhudumu ambaye alimpa maelekezo yaliyomfanya aende kufungua mfuniko wa tenki la gari na kuweka mafuta. Akiwa anaufungua mkanda ili akae vizuri yule mhudumu alikuja akapewa hela yake.

"Samahani kaka naweza kuegesha gari langu hapa kituoni kwako ili nisinzie kidogo?" Alimuuliza kijana aliyemhudumia.

"Kaliegeshe karibu na 'Supermarket' pale kuna 'parking' yenye nafasi." Alimjibu.

"Nashukuru sana kaka yangu."

"Bila shaka." Kijana huyo alimjibu na Catherine akafanya kama alivyoelekezwa na baada ya kufika pale akalipaki vizuri na kukivuta kiti vizuri ili kimrahisishie kujilaza kwa nyuma lakini kwa mbali akamuona mtu kama Malick akiingia kwenye gari lililokuwa mwishoni mwa yale yaliyosimama pale nje akitokea viliko vyoo.

"Siyo mzee Malick Bolenge yule? Hapana sikubali."


UNADHANI HAPO CATHERINE ATAENDELEA KULALA?


UNGANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KILICHOTOKEA KILICHOTOKEA KWENYE SAFARI HII.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post