NITAKUUA MWENYEWE - 36
sultanuwezotz.blogspot.com
"Wewe sikia ukifika Rio Branco tia nanga sawa?"
Jasmine alimweleza nahodha wa ile boti waliyemteka baada ya kuwaua wenzake.
"Nimekupata madam." Alijibu nahodha.
"Hivi tukiingia mjini breki ya kwanza ni wapi?" Aliuliza Jessica.
"Punguza presha dogo breki ya kwanza ni kwa yule bulicheka aliyetoroshwa na Robinson." Alijibu Jackline.
"Duniani kuna maeneo mazuri mpaka raha cheki namna mandhari ya mto huu yalivyo?"
Jessica aliwaonesha nje wenzake wakati boti ikiendelea kuchana mawambi na muda huo tayari ilikuwa ni alfajiri mwanga kuashiria jua linakaribia kuchomoza ulitokea.
"Dada zangu tumefika Rio Branco tayari."
Aliwajulisha nahodha. Ikabidi wayaangalie kwanza mazingira ya nje yalivyo, waliporidhika kuwa ni rafiki walitoka huku Jackline akifanya umafia mwingine.
"Utatusamehe brother ni lazima ufe, paa pa pa paaa....."
Alimtwanga risasi yule nahodha kwa kutumia bastola yake yenye kiwambo kisha waliteremka lakini wakati Jackline akikatisha kwenye moja ya vyumba vya ile boti alikutana na kitu kilichomtoa macho.
"Hili begi lina nini?" Alijiuliza huku akilifuata ili kujua ni la nini mbona lilikuwa limejaa sana. Alilifungua zipu na kuangalia ndani lina kitu gani.
"Ooh my gosh, mihela yote hii waliitoa wapi hawa wanaharamu au ndiyo biashara zao haramu na za binadamu?"
Aliinuka na kuwaita wenzake ambao walikuwa nje tayari.
"Twenzetu Jackline kuna nini tena huko? Jasmine aliuliza baada ya kusikia Jackline akiwaita.
" Njooni muone maajabu ya Mungu."
"Maajabu gani tena hayo bwana?"
Jessica aliuliza huku akipigiza mguu chini kuashiria kutofurahishwa na kitendo kile cha Jackline kuwarudisha botini tena.
Waliingia kwenye boti na kumkuta Jackline akiwa kalilalia begi na alipowaona tu alichomoa mabunda kiasi ya dola na kuwarushia wenzake.
"Hureeeeeeeeeeeee........" Alipiga kelele.
"Umezitoa wapi hela zote hizi Jackline?"
Jasmine alimuuliza baada ya kudaka kibunda kimojawapo baada ya kurushiwa na Jackline.
"Mungu wetu ni wa huruma jamani baada ya shida zote tulizopitia kaamua kututunuku kabla hata kazi yetu haijamalizika."
"Kweli kabisa Jackline hivi madola yote haya tutayafanyia nini eti?" Jessica aliuliza.
"Jamani mengine tutajadili baada ya kutoka huku mtoni ila tu cha msingi tuipekue hii boti tunaweza kupata kitu cha kutusaidia kwenye oparesheni yetu." Jackline aliwaelekeza wenzake.
Basi walianza kuifanyia ukaguzi ile boti mara moja ili kuona kuna nini ndani yake. Walipoikagua kwenye kila kona ya boti na cha kufurahisha walikutana na kisanduku kingine kidogo ambacho ndani yake hakikufahamika mara moja kilikuwa na nini kutokana na uzito wake.
"Jamani mimi nimezikuta hizi silaha tu."
Jessica aliwaambia wenzake ambao muda huo walikuwa nje huku Jackline akiwa kalibeba mgongoni lile begi lenye midola na Jasmine akiwa kakishika kile kisanduku.
"Okay, twendeni sasa muda si rafiki kwetu."
Jackline aliwaambia wenzake kisha wakaondoka eneo hilo ambalo halikuwa na watu wengi sana kwa muda huo. Walishika njia kupandisha juu ya kilima kilichokuwa karibu na mto ule.
"Hebu subirini kidogo jamani."
Jackline aliwaambia wenzake na kuiacha barabara na kulifuata jiwe moja kubwa na kujificha kisha akawapa ishara na wenzake wafanye hivyo hivyo ni baada ya kushtuka kuwa kulikuwa na mtu alikuwa akiwafuatilia kwa nyuma akijificha ficha. Na wenzake wakafanya hivyo na kweli alitokea kijana mmoja akiwa na kisu mkononi na kufika eneo lile ambalo alikuwa akiwavizia wakina Jackline ambao nao walikuwa wakimvizia hivyo wakatengeneza cheni ya kuviziana.
"Usigeuke nyuma tulia hivyo hivyo huku kisu ukikiacha kikutane na ardhi." Ilikuwa ni sauti ya Jackline ambaye alikuwa nyuma ya kijana aliyekuwa akiwavizia. Alitii amri mara baada kitu cha baridi kugusa kisogo chake na kuachia kisu ambacho kilibebwa na Jessica.
" Twambie wewe ni nani? Na kwanini unatufuatilia sisi?"
Jackline alimuuliza huyo kijana baada ya kunyoosha mikono juu kusalimu amri.
"Mimi ni mlala hoi tu wa hapa Rio Branco mara nyingi huja huku kuvizia watu wanaosafiri kwa njia ya boti na kuwapora vitu vyao."
"Kwa hiyo lilikuwa ndiyo lengo lako kwetu pia?" Jasmine alimuuliza.
"Ndiyo dada ila naombeni mnisamehe msiniue...."
Kabla hajamalizia sentensi yake alikutana na Jessica aliyemvamia na kuanza kumpa kichapo kitakatifu.
"Sirudii tena ndugu zangu naombeni msamaha." Alijitetea baada ya kuiva kwa kichapo cha Jessica.
"Simama juu haraka." Jackline alimuamuru asimame.
"Kijana mzuri kumbe una mambo ya kijinga jinga tu muone, si kila unayemuona ni wa kumchezea tu utakufa siku si zako mjinga wewe."
Jackline aliongea hayo huku akimsindikiza na teke la tumbo lililompeleka chini tena yule kijana.
"Nimekoma dada zangu ni shida tu ndiyo zinanifanya kuingia kwenye kazi za hatari kama hizi."
"Mshenzi wewe una shida gani?" Jasmine alimuuliza.
"Mimi naishi na mama yangu ambaye ana miaka mitatu sasa hospitali kalazwa akitibiwa Ugonjwa wa kansa ya damu hivyo kutokana tulijikuta tukiuza nyumba yetu, magari na mashamba kugharamia matibabu ya mama ambapo hatujafanikiwa mpaka sasa na mbaya zaidi baba aliamua kukimbia na kuelekea kusikojulikana mpaka leo."
" Aliondoka lini baba yako?" Jackline aliuliza.
" Mwaka jana na hivyo mimi ndiyo niliyebakia kumuhudumia mama na makazi yangu yako kwenye makorido ya hospital aliyolazwa mama ya St. MARIA HOSPITAL."
Maneno yale ya yule kijana yaliwagusa wakina Jackline na kujikuta wakimwinua huku wakifuta machozi yao.
" Jina lako nani?" Jackline alimuuliza.
" Naitwa Roberto Stanley."
"Pole sana Roberto tuko tayari kukusaidia katika hili kikubwa tuhakikishie kuwa hutarudia kufanya matukio mabaya ambayo yatapelekea kutengana na mama yako ambaye ataendelea kubaki hospitali huku na wewe ukienda kuishi kaburini." Jackline aliongea hayo huku akimfuta vumbi.
" Sitarudia tena dada zangu."
Kilifuata ilikuwa ni kuongozana naye mpaka mjini kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kwenda St. Maria Hospital kumuona mama yake Roberto.
***
"Umeona sasa mzee Bruno wako wapi? Wako wapiiiii? Nilikwambia siyo watu wazuri wale na kwa vyovyote vile yule kijana ni shushushu wao."
Santana aliwaka baada ya kukutana na Ngome ikiwasabahi tu.
"Ninyi ndiyo mnafahamu walikofichama hawa Mbwa?"
Mzee Bruno Gautier alichafukwa baada ya kuwakosa wabaya wake hivyo kuamua kuwatia adabu walinzi wake ambao aliamini nao waliungana kutaka kumpindua na kumpora Mali zake.
"Mzee utatuua tu lakini sisi hatujui lolote lile juu ya hao wasichana kama unavyoona wametufunga hapa toka saa mbili usiku mpaka sasa na hatujui kilichotokea baada ya kuzinduka." Mmoja wao alijitetea.
"Tena wewe ndiyo unyamaze huna lolote askari mzima unakuwa muogaoga kama nini?"
"Kwa kitendo cha vijana wangu kuuwawa kinyama hivi nasema mzee Bruno utalipa na yule kenge wako tuliyemuacha kwenye ndege." Santana aliunguruma kwa hasira ya kuwapoteza watu wake.
"Lakini Santana hili si la kuliendea haraka tunatakiwa kutafakari wametowekaje hapa na pia ukumbuke wakati haya yanatokea yule Robinson hakuwepo huku tulikuwa naye sisi na pale hana hata mchoro wa simu sasa yeye anahusika vipi? Yule ndiye atakuwa msaada kwetu katika kuwanasa wenzake kikubwa tumjengee uaminifu na ikiwezekana tumpe kitengo cha kusimamia kwenye moja ya miradi yetu kisha tumpe Uhuru wa kwenda popote ndani ya nchi nakuhakikishia atawaleta wenzake bila hata kuambiwa."
"Unataka kusema tumuaminishe kuwa sisi na yeye tumekuwa wamoja na tusioneshe ishara yoyote ya kuwatafuta wenzake?"
"Tuko pamoja sasa Santana umenielewa vizuri."
"Ikitokea tofauti itakuwaje?"
"Fanya maamuzi unayoweza juu yangu mimi."
"Kweli mzee Bruno Gautier? Nitakuchinja hadharani."
"Bila shaka kabisa kijana wangu."
"OK tuseme nimekuelewa na kwa upande wa serikali nilishaongea nao kiutu uzima na kuwaambia Sakata hili waniachie mwenyewe nitalimaliza na wamenielewa hivyo kwa sasa hata wakienda popote hawatakamatwa."
"Kweli Santana?"
"Nakueleza hivyo najua katika hili watajisahau na kujiona wako huru na hapo mimi nitawadaka kwa kutumia kidole changu cha mwisho."
Walikubaliana na kisha waliwasamehe wale walinzi na kuwaondoa kwenye milingoti ya mateso na kuwataka kuwa makini wakati mwingine na hapo hapo king'ora kililia na kwa kila aliyekisikia aliacha shughuli zake na kukimbia kuelekea eneo la makutano kusikia kilichojiri.
"Nisikilizeni nyinyi watu msiokuwa na uhuru kwenye chochote mnachokifanya, kuanzia leo sheria zinabadilika kama mlijua uko bozo umefika kwenu mlikuwa mnajidanganya tu zaidi zaidi sheria ndiyo zinakwenda kuwa ngumu zaidi na waliokuwa wanawapa kiburi wameondoka tayari na kama mlijua hapa kuna mateso kwanini hamkwenda nao? Walinzi wapya wa mgodini sogeeni hapa." Walisogea kama alivyotaka mzee Bruno Gautier.
" Kuanzia kesho kazi ni ya kufukua mawe kule na masuala ya chakula ni mara moja tu kwa siku na chenyewe ni jioni pekee kwa wale dhaifu dhaifu watakuwa wakichomwa moto kila siku ili kupunguza idadi ya watu tegemezi hapa kwani hili siyo eneo la msaada."
"Tumekupata mkuu."
"Siyo tu kusema tumekupata mkuu tu hapa halafu hakuna kinachofanyika na labda niseme hivi kwa kilichotokea ndani ya siku hizi ngapi kikijirudia sitaona tabu kuileta ndege ya sumu."
Santana aliongeza kwa kuweka vitisho zaidi kwa wote waliokuwa pale. Lakini wakati hayo yakiendelea simu ya mzee Santana iliita na alipoangalia mpigaji ni nani alibaini ni mke wake hivyo aliipokea.
" Mke wangu kipenzi umeamkaje?"
" Nimeamka salama mume wangu vipi wewe huko umeamkaje?"
"Mke wangu bwana nimeamkaje tena kwani nimelala basi ilikuwa ni mwendo wa oparesheni tu."
"Pole sana mume wangu yatakuwa sawa naamini hivyo, sasa hapa nyumbani kuna wageni wamefika na kujitambulisha kuwa wao ni wafanyabiashara wenzako wanataka kukuona ndiyo nikawaambia ngoja nikujulishe."
"Wafanyabiashara wenzangu?" Mzee Bruno Gautier aliuliza.
"Ndiyo mzee Bruno Gautier au umetusahau?"
Aliongea Jackline baada ya kumpokonya simu mke wa mzee Bruno.
"Mbona siwakumbuki?"
"Mzee nilikueleza tokea mwanzo kuwa usilete jeuri kwani uko chini ya himaya yangu nafikiri sasa maana yangu umeijua mzee Bruno Gautier ha ha ha ha ha ha ha..."
"Buuu Shiiiiiiii.... t watoto haramu sana ninyi na mmelaaniwa toka siku mliyozaliwa mmefikaje kwa mke wangu kipenzi?"
"Ha ha ha mzee Bruno tumefika kwa miguu yetu na ukileta kujua kichwa chake utakikuta mlangoni."
"Sasa mnataka nini?"
"Well well mzee Bruno ni hivi yale mahitaji ya mwanzo tumeyafuta ila tuna manahitaji mapya kutoka kwako."
Jackline aliendelea kumchanganya mzee Bruno.
"Nayasikiliza sasa."
Alijibu mzee Bruno na muda huo Santana alikuwa pembeni akimuangalia tu mzee Bruno.
"Mke wako tutaondoka naye muda huu mpaka sehemu ambayo hutaijua mpaka utekeleze yale ninayokwenda kukueleza hapa nayo ni haya, moja tunamhitaji mwenzetu Robinson hapa pili unatakiwa kuingiza kiasi cha dola millioni kumi na tisa kwenye akaunti ambayo utapewa na pia mwambie Santana kuwa tunafahamu anawaza nini juu yetu hivyo na yeye ili aipange vizuri mipango yake atatakiwa kutoa na kuweka kwenye akaunti namba hiyo ambayo tutaitoa kwako kiasi atakachotakiwa kukiweka ni dola milioni mia mbili themanini na saba leo hii."
"Mnasemaje ninyi malaya?"
Aliuliza Santana mara baada ya kumnyanganya simu mzee Bruno Gautier.
"Usikorome hivyo mbele ya Warembo kama sisi unatakiwa kulegeza sauti eboo kwanza ongea na Malaika wako huyu."
Jackline alimjibu Santana kisha akamkabidhi simu Jasmine aliyekuwa karibu naye.
"Malaika wangu? Unamfahamu Malaika wangu wewe? Santana aliuliza.
" Yes ndiyo mimi hapa Santana na si Malaika wako tu bali Malaika wako mtoa roho wako na mliyoambiwa mnatakiwa kuyafanya leo kabla jua halijatua tofauti na hapo mtatujua."
"Mbona mbon...."
Santana aliishia hewani mara baada ya kukatiwa simu na Jasmine na kubakiawa na simu sikioni asijue cha kufanya nini.
"Vipi wanasemaje?"
"Wale si watu wa kawaida naanza kuamini iweje watoke hapa kabla hatujafika na kwenda kwa mkeo na kumteka?"
Santana aliuliza swali ambalo ni kama mzee Bruno hakulisikia kwani muda huo yeye alikuwa akichora chini sijui ramani ya Tanzania au ya Brazil huku akitokwa na machozi.
" Nini sasa unafanya wewe kizee?"
" Hakuna kitu mdogo wangu."
"Hakuna kitu wakati unatokwa na machozi? Usichekeshe walionuna hapa, cha kufanya ni kuiangalia tunamkomboaje mke wako na kulia utafikiri toto dogo."
"Ni kweli usemayo Santana lakini mke anauma, anauma kweli kweli nakuambia mdogo wangu."
"Ninyi nendeni kwenye majukumu yenu mliyopangiwa tupisheni hapa."
Santana aliona awatoe wafanyakazi wao kwanza ili aongee kikubwa na mzee Bruno ambaye hakuacha kuonesha hisia zake kwa mke wake.
"Tuondoke mzee tuelekee kambini kwangu tukapange cha kufanya juu ya hili maana lile li Jasmine nalielewa halina akili timamu."
"Jasmine? Kuna kitu pale? Huyo mwingine anaitwa Jackson sijui?"
"Halafu na wewe mzee umechanganyikiwa tayari Jackson ni wa kike? Yule anaitwa Jackline."
"Huyo huyo hafai hata kidogo anapiga kama hana akili nzuri."
"Kwa hiyo unawaogopa?"
"Hapana ila nikiwaona lazima viungo vikose ushirikiano labda mwenzangu."
Santana alicheka sana baada ya kumsikia mzee Bruno akiongea hayo juu ya Jackline na ilikuwa acheke kwani hajamtokea Jackline na hata yaliyofanyika kule kwake alijua ni Jasmine hakuwa na habari na Jackline.
JE NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO