IMETOSHA MAMA MKWE - 27
sultanuwezotz.blogspot.com
Fahamu zinanirudia najikuta niko ndani kijijumba kibovu bovu hivi, na nilipogeuza shingo yangu nilikutana na mtu mwenye sura ya kutisha huku mkononi kashikiria pembe jeusi pamoja kibuyu kinachotoa moshi, hali hiyo ilinitisha sana. Na nilipojaribu kutaka kuinuka nilishindwa.
"Unataka kufanya nini mjukuu wangu bado hujawa sawa wewe." Sauti nzito na yenye mikwaruzo iliongea kiasi cha kunitisha.
"Wewe ni nani na hapa ni wapi?" Nilijikaza kumuuliza mzee huyu japo sehemu ya ubavu ilikuwa inaniuma sana.
"Kwa sasa unahitaji utulivu wa kutosha mjukuu wangu kwani bado uko kwenye tiba ambayo haijakamilika bado kwani uliletwa hapa ukiwa hujitambui hata kidogo lakini kwa ninachokiona mbele yangu ashukuriwe Mola kwa muujiza huu." Mzee huyu alinijibu huku akiwa anamimina vitu fulani kutoka kwenye kile kibuyu na kuweka kwenye kibuyu kingine chenye mfano wa kikombe hivi.
" Hebu kunywa hii itakusaidia kukupa nguvu na kukuondolea maumivu yote mwilini." Niliipokea na kuipeleka mdomoni mmh ilikuwa ni chungu sana kwani baada ya kuimaliza mwili mzima ulitokwa na vipele kama vile vya baridi. Nilipomaliza kunywa nilikiweka kile kibuyu chini na kujipukuta mdomo kisha macho yangu nikayaelekeza kwa huyu mzee aliyekuwa pembeni yangu akivuta tumbaku.
"Wewe ni nani mzee na nini kilinitokea?" Nilimuuliza tena swali.
"Uliletwa hapa na rafiki yangu." Alinijibu.
"Rafiki yako? Yupi?" Nilijikuta nikitokwa na maswali mengine.
"Anaitwa mzee Mbogo alikuwa kaongozana na mjukuu wake aitwaye Rachel.."
"Wako wapi sasa na hapa ni wapi?" Nilijikuta namuuliza.
"Hapa panaitwa Inyara na mimi naitwa mzee Nyaswa ni Mtaalamu wa tiba za asili, uliletwa hapa ukiwa hujitambui hata kidogo kwani ulitupiwa jini...." (kabla hajamaliza nilimkatisha)
"Jini? Unamaanisha nini mzee Nyaswa?"
"Ni hivi, wewe ulitupiwa jini na bibi mmoja aliyejivika ngozi ya kondoo na kujidai msamaria mwema bibi huyo anaitwa Kiziwa."
"Bi Kiziwa?" Nilimuuliza tena.
"Ndiyo Bi Kiziwa, unajua ilikuwaje?" Aliniuliza swali.
"Sijui naomba unieleze mzee wangu."
"Ile siku uliyoingia nyumbani kwake na kupokea yale maziwa na kuyanywa ndiyo siku ambayo ulitupiwa hilo jini ambalo unatembea nalo bila kujua." Mzee Nyaswa alinieleza.
"Hapana mzee Nyaswa mbona mimi ninakumbuka siku ya mwisho nilikutana na sura ya Bi Kiziwa kwenye kioo? Na wewe unasema kuwa nilitupiwa Jini mbona sielewi?" Nilijikuta nachanganyikiwa.
"Mambo ya Ulimwengu wa giza huwezi kuyajua lakini elewa kuwa kilichokuwa kikikutokea ni taswira yake tu lakini wewe ulikuwa na Jini ambalo nimefanikiwa......." Mara mlango uligongwa na kumfanya mzee Nyaswa kusita kuendelea kusimulia na kuuangalia mlango kisha mimi.
" Sijui ni wenyewe?"Aliuliza huku akiuendea mlango na kuufungua.
" Oohh karibu sana Rachel." Alimkaribisha.
" Asante mzee mwenzangu." Alimjibu huku akiingia ndani.
" Jamani Christina ni wewe?" Alijikuta akiniuliza mara baada ya kunikuta nikiwa nimejilaza kwenye kimkeka pale ndani.
"Ni mimi Rachel, mbona unaniuliza kama vile nimekuwa mpya kwako?" Nilimuuliza.
"Kwa namna ambavyo ulikuwa siku tatu zilizopita we acha tu ndugu yangu." Rachel alinishtua kidogo kwa maelezo yake.
"Nimekuwa hapa kwa siku tatu? Na vipi kuhusu chuo na ndugu zangu?" Niliwauliza wakina Rachel.
"Ndiyo umekuwa hapa kwa siku tatu maana hali yako ilikuwa mbaya na kama tungekuchelewesha hapa sijui ingekuwaje?" Alinijibu Rachel.
"Najua utakuwa unajiuliza kwanini hawakukupeleka hospitalini, ukweli ni kwamba ungepelekwa huko tu usingechukua hata siku moja kwani huyo Bi Kiziwa alishatega mitego yake huko." Mzee Nyaswa aliongeza kwenye kitu ambacho nililenga kukiuliza.
"Christina mjukuu wangu." Aliniita.
"Abeee babu."
"Kwa sasa uko sawa baada ya kukutoa huyo Jini kilichosalia kwa sasa ni dozi ambayo nimekupa kwa ajili ya nguvu ambazo zilichotwa na huyo Jini wakati akitoka na kwa dawa ulizokunywa kwa hizi siku mbili utakuwa sawa muda si mrefu."
"Mzee wangu ninaweza kuondoka naye leo?" Rachel alimuuliza mzee Nyaswa.
"Bila shaka inawezekana kwani kila kitu nimeshaandaa kuna hizi dawa atazitumia atakapokuwa nyumbani na vipi kuhusu mzee Mbogo haji?"
"Babu ilikuwa tuje naye lakini akaniomba mimi nije huku na yeye kaenda kwa Bi Kiziwa kuchukua mkoba wa Tina lakini naweza kumpigia uongee naye." Rachel alimjibu na kuitoa simu mfukoni kisha aliitafuta namba ya mzee Mbogo na kuipiga wakati huo mimi nikajivuta kutoka pale nilipokuwa na kumfuata mzee Nyaswa kwa staili ya kushela(kujivuta).
" Mzee wangu sina cha kukulipa kwa hiki ulichonifanyia lakini Mungu atakulipa tu." Na kabla hajajibu chochote Rachel alikuja na kumkabidhi simu ambayo aliipokea na kutoka nje huku akituacha sisi ndani.
"Tina huna sababu ya kujiliza cha kushukuru ni uzima ulionao na pia unakumbushwa kuwa si kila unayemuona mbele yako ni mtu wengine ni wanyama japo huja kwenye maisha yetu kwa njia tofauti tofauti."
"Ni kweli kabisa Rachel kwa namna ambavyo nilikutana na Bi Kiziwa na kupelekea kumuamini sikutegemea kabisa angenifanyia hivi hata kidogo." Nilimjibu Rachel ambaye alikuja na kunikumbatia.
"Usijali Tina na unachotakiwa kukijua ni kimoja tu kila kitu hutokea kwa sababu na si kingine kwani hata dhahabu ili iwe na thamani kubwa ni lazima ipite kwenye moto na hata maandiko ya Mungu yanasema 'Heri mtu astahimiliye majaribu, kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia Wampendao.' Mistari hiyo unaipata kwenye Waraka wa Yakobo 1:12, upo Shosti." Alihitimisha kwa kunipiga bega.
" Rachel unanitisha unajua! Yaani mpaka maandiko unayajua? Sasa mbona huna msimamo maana nasikia ukiamua kuwa kwa Mungu simama huko na ukiwa kwa Shetani pia simama huko."
"Unajua nini? Nimeanza mazoezi ya kuiacha hii njia ya mzee Mbogo na kuifuata ile iliyo ya kweli." Rachel alininong'oneza sikioni sijui hakutaka kusikiwa na mzee Nyaswa kwani baada ya kuniambia hivyo aliinuka na kutoka nje na ndani ya dakika kadhaa walirudi wakiwa pamoja.
" Tina mjukuu wangu kwa mujibu wa maelezo ya mzee Mbogo ni kwamba leo mtalala hapa pamoja na rafiki yako Rachel kwani huko juu anga limechafuka sana." Mzee Nyaswa aliongea akiwa anampisha Rachel aliyekuwa akichat na simu yake pasipo kutazama mbele.
"Hizo simu zenu zitawatia upofu kwani hata mbele hamtazami, katika hilo mzungu alifanikiwa halafu hapo hapo tunataka kushindana nao kwa njia gani?" Mzee Nyaswa alimtania Rachel japo ulikuwa ni utani wenye ukweli ndani yake.
"Kivipi babu?" Rachel alimuuliza mzee Nyaswa akiwa bado macho yametazama kwenye simu yake.
"Si kama hivyo muda huu unachati na marafiki lakini wao muda huu simu zimeachwa majumbani huku wao wakiumiza vichwa kuvumbua teknolojia mpya huoni utofauti huo Rachel?" Mzee Nyaswa alimjibu jibu ambalo hata mimi lilinishangaza kwani sikuwahi kusikia kama wenzetu simu hawatembei nazo mifukoni kama sisi.
" Maneno tu hayo babu ambayo yametungwa tu na wajanja fulani wasiokuwa na jeuri ya kununua simu janja kama hizi si unakumbuka hata zamani zenu mlikuwa na tumisemo twingi twingi twa kutiana moyo mfano 'mchagua jembe si mkulima' na twingine twingiii." Rachel alimjibu babu.
" Samahani babu naomba nikurudishe nyuma kidogo tafadhali, umesema kuwa mzee Mbogo kasema inatubidi tulale hapa usiku wa leo maana anga limechafuka una maanisha nini kusema hivyo?" Ilibidi niwakatishe kwa kutaka kujua tafsiri ya yale maneno anga kuchafuka.
" Bado mdogo sana Tina lakini fahamu hivyo tu kuwa leo mtalala hapa na Rachel ili na mimi nimalizie dozi yangu ya mwisho ili mnapoondoka hiyo kesho uwe umeshapona tayari." Alinijibu mzee Nyaswa.
"Sasa na wewe babu umeyakubali maneno ya babu yangu haraka haraka tutalala wapi na nyumba yako yenyewe hii ndogo kiasi hiki?" Rachel alimuuliza mzee Nyaswa.
"Rachel niondolee umjini mjini wako mtalala popote pale hata kama ni juu ya mafiga shida yako nini wewe?" Alimjibu akiingia chumbani kwake ambako kumetenganishwa na pazia jeupe tu.
Tukiwa pale sebuleni Rachel alinifuata na kuniinua sikujua alitaka kufanya nini pale ikabidi nimuulize.
"Unataka kufanya nini Rachel?" Nilimuuliza.
"Jitahidi uinuke tufanye mazoezi ya viungo kidogo utembee tembee ili kujua kama uko vizuri au la." Alinijibu huku akipambana kuniinua kutoka pale chini.
"Ni kweli kabisa Tina unatakiwa ujitajidi kufanya mazoezi ya viungo hiyo nayo inaweza kusaidia kidogo ngoja na mimi niandae dawa ambayo itakusaidia." Mzee Nyaswa naye aliunga mkono maneno ya Rachel. Hivyo sikuwa na pingamizi lolote zaidi ya kukubali tu. Nilifanikiwa kuinuka na kisha Rachel akaushika mkono na kuanza kunivuta taratibu tukitoka nje.
" Tutatembea kidogo kisha tutatumia gari ili kuvinjari maeneo ya huku shamba kidogo au unasemaje Tina?"
"Niseme nini Rachel lolote lifanyike tu kikubwa nisisababishe majanga mengine." Nilimjibu.
"Wala usijali wangu." Rachel alinijibu.
"Lakini ngoja kwanza Rachel hivi simu yangu iko wapi?" Nilimuuliza.
"Kwa kweli hata sijui iliko ndugu yangu maana siku ile hata akili ya kuangalia simu sikuwanayo labda kama iko mle ndani." Alinijibu.
"Basi hebu jaribu kuipiga kama itaita maana sikumbuki kama niliizima." Rachel aliipiga lakini haikupatikana alirudia tena lakini hali ikawa vile vile.
"Haipatikani Tina lakini usijali kama unataka kufanya mawasiliano tumia hii yangu na tukirudi mjini nitakupa simu yangu moja ambayo inazagaa tu mle ndani ambacho utakifanya ni kuirudisha namba yako ile ile." Maneno ya Rachel yalinipa faraja kiasi chake nikajikuta napona hivyo nilimtajia namba ya baba akaipiga lakini haikupatikana ikabidi nimtajie namba ya baba ambayo yenyewe iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa hali hiyo ikanipa wasiwasi kwamba labda kuna jambo baya limewapata.
"Unaonaje kama una namba ya mtu wa jirani kwenu umeishika itaje nimpigie pia." Rachel aliniambia kitu ambacho niliona ni kizuri hivyo nikavuta kumbukumbu ya namba ya mtu wa jirani niliyoishika lakini sikuweza kuipata. Niliwaza sana kitu ambacho Rachel alikigundua hivyo kunitaka tuingie kwenye gari.
JE NINI KITAENDELEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI TUJUE NINI KITAENDELEA.
#SULTANUWEZO