MUUAJI MWENYE BARAKOA - 21 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 21

sultanuwezotz.blogspot.com 


Adoyee alimtazama Awadh ambaye alimpa ishara ya kutii amri, hivyo waliweka chini bastola zao chini mabegi yakiwa migongoni. Mmoja wa wale watu alisogea na kuinama kuzichukua zile bastola alianzia ya Adoyee na kisha akaigeukia ya Awadh, alifanya kosa alipompa mgongo Adoyee akiinama kuiokota bastola ya Awadh kwani Adoyee alimtazama kwanza yule aliyekuwa kasimama kawanyooshea bastola akagundua kuwa kajisahau hivyo haraka sana aliingia katikati ya miguu ya mtu yule ambaye bila shaka ni mmoja wa vijana wa mzee Malick Bolenge aliyekuwa kainama kuiokota bastola ya Awadh na kumfanya kijana yule kuanguka chini kama gunia la pamba na bila kuchelewa Adoyee alimfuata na kumpiga kichwa cha utosi kilichomfanya ashindwe kujimudu, yule mwenzake alipigwa na butwaa asijue afyatue risasi au afanye nini kwani lilikuwa ni tukio ambalo hakulitarajia na wakati akitaka kufanya maamuzi alishachelewa kwani Awadh aliviringika kwa kasi ya ajabu kuelekea alikokuwa bastola mkononi akimfyatulia risasi zisizo na idadi.

"Hamuwezi kuucheza mchezo huu ninyi vikaragosi." Awadh aliongea akiinuka baada ya kujiridhisha kuwa mpinzani wake alishakufa huku damu ikiendelea kuukataa mwili wake. Kwa upande wa Adoyee yeye alikuwa kambananisha vilivyo huyu mwingine baada ya akili kukaa sawa kutokana na kichwa alichogongwa.

" Sasa tunaweza kuongea kirafiki kabisa kwa kuwa sisi si kama ninyi mnaovizia wanaume wakiwa kazini haya niambie nani kawatuma kwetu?" Adoyee alimuuliza kijana huyo ambaye macho yalikuwa yamemtoka isivyo kawaida kutokana na kutazamana na mdomo wa bastola.

"Mimi hata sijui lolote niliambiwa na mwenzangu Keita kuwa kuna bosi kamwambia tumlindie nyumba yake mpaka atakaporudi na kwa kuwa nilikuwa sina kazi nilikubali." Alimjibu.

"Keita ndiyo nani?" Adoyee alimuuliza.

"Yule kule aliyelala."

"Aliyelala? Sema aliyekufa humu umebakia wewe tu na ukileta jeuri ya kutudanganya unamfuata." Awadh alidakia.

"Bila shaka umesikia hivyo hatutegemei brabra hapa, sawa?" Adoyee alimwambia akimgonga uso kwa mdomo wa bastola.

"Ndiyo kama nilivyokujibu kaka wala sijakudanganya." Kijana huyo aliongea.

"Wewe ni mwenyeji hapa?" Awadh alimuuliza.

"Ndiyo kaka." Alijibu.

"Mmh kwa hiyo unacheza na akili yangu siyo? Si umetoka kuniambia kuwa Keita alikupa dili kutoka kwa bosi mmoja ukimaanisha humjui." Adoyee alimsogelea karibu zaidi na safari hii alimkusanya shati kwa mbele huku sura yake ikiwa sambamba na ya huyo kijana.

"Ni kweli kabisa mimi simfahamu bosi wetu na wala sijawahi kuonana naye mawasiliano yote yalikuwa yakifanywa na Keita." Alimjibu.

"Una roho ngumu sana kwa ninavyokuona, hii nyumba ni ya nani?" Adoyee aliendelea kumbananisha huku Awadh akimkagua mifukoni.

"Mwenye hii nyumba?" Alirudia kuuliza kama vile hakusikia vizuri.

"Usitucheleweshe kaka tuma shughuli nyingi za kufanya tupe jibu haraka,, unafikiri haya ni matangazo ya vifo?" Mara hii Adoyee alimtolea utafikiri ndiyo alikuwa akimtazama kwa mara ya mwisho.

"Unamchelewesha tu huyo si unajua wa hivyo hata uwafanye nini hawaongeagi ukweli malizana naye fasta tutoke humu ndani." Awadh alimwambia Adoyee akiurekebisha mkanda wa begi lake.

"Naombeni msiniue nitawaambia kila kitu nimekumbuka."

"Una dakika moja tu ya kuvuta hewa safi ongea haraka." Adoyee alivurugwa.

"Bosi wetu ni mzee Malick Bolenge na ndiye mwenye hii nyumba." Aliona aongee ukweli tu maana kauli ya Awadh haikuwa salama kwake.

"Kwa sasa yuko wapi?" Awadh alimuuliza.

"Yuko Hotelini kwake."

"Hotelini kwake? Kivipi?" Adoyee alishangaa.

"Siwezi kuwadanganya yuko huko kaka." Alijitetea.

"Unauhakika na unachokiongea? Hajasafiri?" Adoyee alimuuliza.

"Hajasafiri yuko kule." Majibu yale yalimfanya Awadh atoe moja ya simu aliyoikuta kwenye mifuko ya Keita akaiwasha.

"Mpigie simu bosi wako huyo mwambie Keita hali yake ni mbaya sana."

"Sawa, sawa." Aliitika akiipokea simu. Na baada ya kuipiga haikupatikana namba ya mzee Malick.

"Hapatikani."

"Unasemaje?"Awadh alimsogelea na kumkita kisu cha tumbo kisha akamsindikiza kwa risasi ya kichwa.

" Hauwezi kutupotezea muda wetu kiasi hiki."Aliongea Awadh wakati kijana huyo akitapatapa pale chini.

" Chukua simu hiyo tuondoke zetu." Alimwambia Adoyee wakati yeye akianza kuondoka.

" Oya vipi kwema humu? Nimeona hamtoki nikajua mmekumbana na misukule maana mjumba wenyewe haueleweki huu." Alitokea Soud na kuwauliza.

"Acha maswali kaka okota zile silaha pale zinaweza kutusaidia mbele ya safari." Adoyee alimjibu.

"Okay sawa, lakini mnauhakika kama walikuwa ni hawa hawa jumba zima?" Soud aliuliza tena.

"Endelea kuuliza hapo hapo ukitosheka na maswali yako utatufuata." Adoyee alimjibu akitoka anakimbia. Soud hakuwa na la kufanya zaidi ya kuzihesabu hatua zake kutoka nje. Walifika nje moja kwa moja wakaingia kwenye gari, Awadh akaliwasha na kuondoka zao.

"Kuna kitu sijakielewa hapa mjue?" Awadh aliongea.

"Kipi hicho?" Soud aliuliza.

"Kama ni kuhusu mzee Malick mimi ndiyo nimechoka kabisa." Adoyee aliongeza.

"Ikoje kwani?" Soud ilibidi aulize baada ya kuona wenzake kuna jambo wanalijua.

"Kama ambavyo tulihisi ndivyo ilivyo mzee baba hayuko Mali tunaye mjini hapa hapa, sijui wakina Jumbe watakuwa wamefanikiwa?" Awadh alimjibu Soud na kuuliza swali.

"Sasa kama yupo hapa hapa na vipi kuhusu ile signo kuonekana nchini Mali?" Soud alitaka kujua.

"Soud unapouliza unatakiwa uwe unafikiria kwanza huu ni wakati gani?" Awadh alimjibu kwa swali.

"Basi bwana yaishe, unanikazia sauti utafikiri mimi ndiyo mzee wenu Malick." Soud hakutaka makuu.

"Acha hizo kaka kwa hiyo umeshachukia?" Adoyee alimuuliza.

"Niacheni bwana." Soud alijibu akigeukia mlangoni.

"Yaani hili jamaa sijui Madam aliitoa wapi maana mambo yake yamejaa utoto tu sasa hapa kipi kimemnunisha." Awadh aliongea akishuka baada ya kulipaki gari sehemu yake walikuwa wameshawasili nyumbani kwao.

"Unakwenda wapi hebu simama hapo." Soud aliongea akishuka na kumfuata Awadh aliyekuwa akielekea ndani.

"Unataka kufanya nini?" Awadh aliuliza baada ya kuona Soud anamfuata kwa kasi.

"Soud una nini wewe?" Adoyee alimuuliza.

"Unataka kujua?" Soud aliuliza akiiweka sawa bastola yake.

"Muache afanye anachotaka kufa si amedhamiria hilo huwezi kujua mzuka wake unamuongoza nini kwa wakati huu.

" Nakuona mrembo sana Awadh huwezi kucheza na mimi hata mara moja usione ni mpole hivi ukajua ni moto wa makaratasi, huu ni moto wa pumba za mpunga ambazo huwaka taratibu bila papara hivyo tuheshimiane sana." Soud alimwambia Awadh maneno hayo kisha akaishusha bastola yake ambayo alishamuwekea kichwani.

" Nimekuelewa Mwamba, lakini haikuwa kwa ubaya nilikuwa natania tu si unajua tena kazi yetu hii muda mwingine tunatakiwa tufurahi sasa kama tutakuwa tunanyanyuliana vyuma itakuwaje? Lakini usijali nimekuelewa katika hilo sitakukwaza tena." Awadh aliona ajishushe baada ya kuona Soud kapaniki isivyo kawaida.

" Ndiyo nishamaliza hivyo huwa sipendi kudharaulika hata kidogo." Alikazia akikaa chini pale pale nje akionekana kachukia kutokana na kauli za Awadh. Adoyee alimuangalia kwa muda kisha alimfuata pale alipokaa.

"Msamehe tu mshikaji alikuwa anatania, si unajua sisi ni timu au umesahau?"

"Najua hilo." Alimjibu.

"Kama ndiyo hivyo basi tusiruhusu pepo la hasira kupita katikati yetu badala yake tumruhusu utani awe sehemu ya maisha yetu. Tukiruhusu hasira tutakuwa na mwisho mbaya hebu angalia kama pale umemnyooshea bastola unafikiri nini kingetokea? Sijapenda hata kidogo." Adoyee aliongea maneno yaliyoonekana kumuingia vilivyo Soud ambaye aliinuka na kuingia ndani ambako alimfuata Awadh na kumtaka radhi. Walisameheana na kisha walitoka nje na kumkuta Adoyee akiwa bado kaketi pale chini akiwa mwenye mawazo mengi.

" Mbaba usiwaze sana tumezika mgogoro wetu ni ukurasa mpya sasa." Awadh aliongea akimshika bega Adoyee ambaye aliinua kichwa na kuwaona wako pamoja.

"Mambo si hayo sasa washikaji zangu." Adoyee aliinuka na kuwakumbatia kwa furaha huku kila mmoja akionekana mwenye furaha sana.

"Woyo woyo woooyoooo piga keleleeee!!" Awadh alipiga kelele.

"Oya tuingieni ndani tupange mipango tuna kazi ya kufanya mbele yetu." Adoyee aliongea baada ya kuona furaha inazidi katikati yao wakati wako kwenye uwanja wa vita.

Wakiwa bado katikati ya furaha mara simu ya Awadh iliita.

"Simu inaita hiyo." Soud alimwambia Awadh ambaye alionekana kutojali.

"Sijui ni nani huyu?" Aliongea akiitoa mfukoni na kuangalia mpigaji ni nani.

"Ni Seynabou huyu sijui kuna nini huko?" Aliongea akiiweka sikioni simu.

"Unasemaje Seynabou?" Awadh aliuliza.

"Aaagh kakata, oya ee hali ni tete kule wakina Jumbe yamewakuta."

"Yamewakuta? Kuna nini?" Adoyee aliuliza.

"Seynabou kapiga simu akiongea kwa sauti ya chini sana inavyoonekana ni kama kajificha hivi." Awadh alimjibu.

"Tunasubiri nini sasa?" Adoyee aliuliza akiingia ndani kasi.

"Sikilizeni ndugu zangu tusikurupuke huko huwezi jua inawezekana wametekwa na kuwashinikiza na sisi twende huko tukadakwe hivyo basi lazima tujiandae." Soud aliwaambia wenzake walioonekana kuwa na moto.

"Unasema nini Soud?" Awadh alimuuliza.

"Hebu twende ndani kwanza tukaichore ramani ya eneo hilo na namna tutakavyoingia." Soud alimjibu akimshika mkono. Waliingia ndani na kumwita Adoyee aliyekuwa chumbani akijiandaa.

"Fanya haraka basi." Soud aliita.

"Ninyi tayari?" Aliuliza akiwa anatoka.

"Mbona siwaelewi washikaji mnapata wapi nguvu ya kutulia wakati wenzetu wamebananishwa huko." Aliuliza baada ya kuwakuta wenzake wamekaa.

"Labda sisi ndiyo tukuulize wewe unakwenda kufanya nini?" Awadh alimuuliza Adoyee aliyekuwa akihema juu juu viatu mkononi. Swali hilo lilimfanya atulie kidogo kwani hakujua alijibu vipi.


JE NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post