NITAKUUA MWENYEWE - 28
sultanuwezotz.blogspot.com
"Ninyi hapo nifuateni haraka."
Jamie aliwataka walinzi wawili aliowakuta nyuma ya jengo la utawala waongozane ofisini kwa mkuu wao kuubeba mwili wa Ogingi.
"Jamie mbona ghafla hivyo tukufuate wapi na kufanya nini?"
Mmoja wa walinzi aliuliza.
"Umeota mapembe siku hizi dogo siyo umesahau tulikokutoa siyo?" Jamie alimuuliza mlinzi huyu.
"Samahani kaka Jamie nilikuwa natania tu twende zetu basi."
"Endelea kuvimbisha kifua wewe si Jemedari mkuu wa Ngome."
"Kaka Jamie na wewe hutaniwi tu mbona yamekwisha kitambo hayo."
"Maamuzi yangu ni haya, wewe baki hapa na maswali yako wewe pale nifuate huku haraka."
"Sawa brother."
Yule mlinzi alimfuata Jamie kule juu mpaka kwenye ofisi ya mkuu wao na kuingia ndani ambako bado mwili wa mwenzao ulikuwa pale pale chini ukisubiri kutolewa na kupelekwa eneo maalum ambalo huichoma kupoteza ushahidi kabisa.
"Jamie hivi tutaendelea kuyafumbia macho matukio haya ya wenzetu kuuawa mpaka lini lakini?"
"Sikiliza dogo sauti zetu hata tuzipaze vipi haziwezi fika popote zaidi ya kuishia kwenye tanuru la moto ambako mwenzetu ndo tunampeleka huko lakini laiti kama tungekuwa na roho za kijasiri kama wale wageni hakika Ngome hii ingekuwa huru na tungepata fidia kwa miaka yote tuliyohudumu humu ndani."
"Ni kweli kabisa kaka lakini bado tuna muda wa kufanya kitu." Mlinzi yule alimwambia Jamie kuwa muda wanao.
"Hebu mshike huko miguuni tufanye kama tulivyoagizwa si unamjua mzee huyu kwa machale?"
"Haya kaka twende zetu mshike vizuri hapo ila kaka fanyia kazi hili tunaweza kufanya jambo."
"Chunga mdomo wako dogo utakuponza shauri yako kumbuka Ogingi tulikuwa naye masaa machache yaliyopita na sasa jina lake limebadilika na zaidi roho yangu inaniuma sana kwani ni juzi tu alinionesha picha ya mpenzi wake ambaye alimuacha nyumbani Kenya akiwa mjamzito kabla hajahadaiwa na maajenti wa mzee Bruno Gautier walioenea bara zima la Afrika wakiwadanganya kuwa huku Brazil kuna fursa nyingi za kazi za migodini na baada ya kufika huku ndoto zetu zote huyeyuka na kufunikwa blanketi zito lenye kiza kinene ambacho hatujui hatma yake ni lini?"
Jamie alionekana kuguswa sana na kifo cha rafiki yake na hivyo kumsihi mlinzi mwenzake kuacha mawazo ya hovyo.
" Mlikuwa bado hamjamtoa tu si ndiyo?"
Mzee Bruno Gautier aliwauliza.
" Ni kweli mzee shida ilikuwa ni namna ya kumbeba ni mzito sana." Jamie alimjibu.
"Kelele wewe fanyeni haraka kisha mje hapa niwape jukumu jingine sawa?"
"Ndiyo mzee."
Walitoka na kuelekea eneo lililo na tanuru la kuchomea maiti na kisha kumuweka ndani yake wakapanga magogo kisha mafuta ya taa yakafuata na baadaye wakawasha moto ambao ndani ya muda mchache ulimteketeza Ogingi na kuwa majivu na hapo walirudisha taarifa kwa mzee Bruno ambaye mara zote hufurahia matukio hayo ila ilikuwa tofauti kwa tukio hili kwani pamoja na kupokea taarifa hiyo yeye alikuwa mbali kimawazo akivuta zake kiko tu huku mkono mwingine ukigusagusa kifuko cha kuhifadhia bastola.
"Mkuu tunasubiri oda yako."
"Okay hebu ongozaneni na walinzi wengine kumi muelekee kule mgodini mkaniletee wale wageni ambao tuliwapeleka kule kwa mateso."
"Sawa mkuu kama ulivyoagiza."
Waliondoka pale na kuwafuata wenzao na kumuacha mzee Bruno ambaye baada ya maagizo yale alianza kupanda ngazi taratibu kuelekea ofisini kwake kusubiria matokeo ya kile kitakachotokea huko.
"Sijui itakuwaje kwa hawa wakifika huko maana maji yamenifika shingoni daa, Weee naniiii.......! Aisee kumbe tayari wameshakwenda."
Alijishtukia kuwa mawazo yake yalivuka kiwango cha kawaida hadi kufikia kutaka kuwaita watu ambao muda mrefu walishakwenda mgodini.
Alipanda ngazi na kuufungua mlango wa ofisini kwake na kisha aliingia.
Wale walinzi wakiongozwa na Jamie walifika kule mgodini mpaka eneo linalochimbwa mawe na kuanza kulivizia eneo walilokuwepo wakina Jackline kwa tahadhari kubwa.
"Sikilizeni tunakoelekea kuna watu hatari sana na mpaka sasa wameshaua wenzetu kadhaa na wengine wanawashikilia huku huku cha kufanya hapa ni kila mmoja apite njia yake lakini makutano ni pale kwenye zile Tenti ambapo nina uhakika muda huu wa usiku watakuwa pale wakipumzika hivyo tukiwavamia kutoka pande zote itakuwa rahisi kwetu kuwakamata."
Jamie aliwatahadharisha wenzake na kuwapanga pia namna ya kuvamia Tenti za wakina Jackline.
" Tumekusoma kiongozi."
Alijibu mwenzao mmoja wakati wengine wakipotelea kizani.
Kila mmoja akifanya kama walivyokubaliana.
Kwa kuwa eneo lile wao ni wenyeji wakilijua vizuri halikuwasumbua sana kuzifikia zile tenti na kwa ishara ambayo walipanga kuitumia kwa pamoja waliwasili na kuitageti kutoka pande zote.
Baada ya kuhakikisha kuwa wote wako kwenye eneo lengwa Jamie alianza kuisogelea tenti ya kwanza na ili kuwateka waliomo ndani yake na baada ya kuchungulia kupitia kitundu kimoja wapo hakuweza kuona kitu ndani yake zaidi ya vigodoro visivyo na watu juu yake, hali ile ikamrejesha nyuma haraka Jamie kuwafuata wenzake kuwapa taarifa ya alichokiona.
"Kaeni sawa eneo hili si salama kwani ndani ya tenti la kwanza hakuna kitu inawezekana wametushtukia, ngoja niangalie lile la pili kwanza."
"Sawa big fanya yako."
Alirudi tena kwenye tenti la pili na safari hii akienda kwa staili ya kutambaa mpaka lilipo tenti la pili.
Baada ya kulifikia alisimama na kuchungulia kwa staili ile ile lakini bado hali ilikuwa kama ya kwenye tenti la kwanza kwani hakukuwa na mtu yoyote ndani yake na hapo akajua kwa vyovyote vile maadui zao wamewazunguka ikabidi arudi haraka kwa wenzake kuwataka kurudi nyuma haraka kabla hawageuzwa asusa na wakina Jackline. Lakini alishachelewa kwani ile anainuka tu alikutana na ngumi nzito iliyotua vilivyo kwenye shavu la kulia na kumtupa chini alipojaribu kuinuka alipigwa risasi ya mguu na kumfanya Jamie kutoa mlio wenye mchanganyiko wa maumivu makali.
"Usiniue, usiniue tafadhali siyo matakwa yetu ni mkuu wetu mzee Bruno."
Jamie alianza maelezo mwenyewe kabla ya kuulizwa inawezekana kutokana na namna alivyootewa na ile ngumi na kisha risasi akajua ahera inamwita.
"Brother mwili mkubwa namna hiyo kumbe muoga hivyo?"
Robinson alimdhihaki Jamie huku akimkanyaga sehemu ile aliyomtwanga risasi. Na kwa namna ambavyo kimwezi kilikuwa kiking'ara haikuwa tabu kwa mtu kuweza kumuona adui yake.
"Kaka nisamehe kwa kweli sisi si watu wabaya bali ni mzee Bruno ndiye aliyetuagiza kuja kuwakamata."
Aliendelea kujitetea Jamie.
"Anasemaje huyo?" Jasmine aliuliza.
"Anachochote basi ni stori zile zile za kukikimbia kifo." Robinson alijibu.
"Sikiliza kaka sisi si watu wabaya kwenu ila mnaweza kutuita Upepo wa Jangwani ambao huwa hauzuiliwi na chochote, na hatuwezi kuwaua ninyi ila tunawaagiza kwa bosi wenu mkamweleze kuwa chimbo limevamiwa na si chimbo tu bali Ngome nzima lakini anaweza fanya jambo ambalo si jingine zaidi ya kumtaka mzee huyo afike kwenye majadiliano."
Jackline alimuagiza Jamie kwa mzee Bruno Gautier.
" Sawa sister nashukuru kwa nafasi nyingine ya uhai wetu nakuhakikishia kulifikisha hili usiku huu huu japo mguu umepata hitilafu."
"Halituhusu fanya kama tulivyokuagiza brother na mkamweleze kuwa kuna kitu anachokitegemea tunakishikilia."
Jasmine aliongeza.
"Sawa dada ngoja tukamwambie."
Baada ya maagizo hayo waliwaachia na wao kurudi kwenye ficho lao ambalo bado halikuweza kufahamika mara moja.
Kwa kukongojana hivyo hivyo waliweza kuwasili ofisini kwa mzee Bruno Gautier na kumgongea mlango. Lakini haukufunguliwa hivyo hali hiyo ikawachanganya kidogo lakini wakaona wajaribu mara kadhaa ndipo mlango ukafunguliwa na mzee Bruno ambaye ilionekana wazi alikuwa kalala kwa namna alivyotoka akipiga miayo mingi.
"Lete taarifa Jamie."
"Mzee hali ni mbaya sana huko kama utuonavyo tulivyochakaa kwa majeraha."
"Keleleeeeeee weweeee unaongea nini majeraha kitu gani mbona hakuna aliyekufa kati yenu?"
"Mkuu wameteka baadhi ya maeneo yako mpaka sasa."
"Unasemaje weweeee?"
Mzee Bruno Gautier alipagawa baada ya kusikia habari za kutekwa kwa maeneo yake.
***
Black alishika njia mpaka ndani ya kijiji cha Bitimanyanga na kuibukia madukani, alipofika alielekea kule ambako aliiona ile Toyota Cruiser imepaki kwa rangi na muundo alijua ndiyo yenyewe. Baada ya kuifikia alijaribu kukigonga kioo cha mbele ili kuona kama kuna mtu ndani yake, lakini kimya kilitawala hivyo ikabidi anyonge kitasa lakini akakutana na lock akachanganyikiwa lakini wakati kijasho cha hofu kikimshika ikajikuta akishikwa bega kwa nyuma.
"Brother vipi kwenye gari langu?"
"Sorry ndugu nimeona imepaki hapa nilijua kuna mtu ndani yake na ndiyo maana nilikuwa nikigonga."
"Ili iweje baada ya hapo?"
"Shida yangu ni lift tu na si kingine ndugu yangu nimetembea kwa umbali mrefu kutoka Isangawana mpaka hapa kwa zaidi ya kilometa thelathini nimechoka hivyo nikaona niombe msaada."
"Isangawana ndiyo wapi na unaelekea wapi?"
"Ni mji ulioko huko nyuma na mimi naelekea Sikonge nilikuwa kwenye matumbaku lakini mambo yamekuwa tofauti na matarajio yangu hivyo nimeona nitoroke tu."
"Ha ha ha ha ha ha ha ha ha, kaka uko vizuri kwenye kutengeneza uongo ee, tuache hayo unamfahamu mzee Jonathan?"
Ilibidi Rashid amuingie kwa kutumia utambulisho wa mtu anayewaongoza wote, na kwa swali lile Black akajua ni mwenyewe ikabidi akubali.
"Namfahamu na ndiye aliyeniagiza kwako."
"Okay okay ngoja nimpigie basi kumjulisha kuwa umefika."
Alitoa simu mfukoni huku akimpa ishara Black ya kuingia ndani ya gari, baada ya kumpata hewani aliongea naye.
"Kijana wako keshafika tayari hivyo ni muda wako kuja tunakusuburi mzee wangu."
"Okay vizuri sana basi tangulieni mbele kidogo mtoke hapo katikati ya mji uelekeo wa Tabora."
"Sawa mzee kama ulivyopendekeza."
Kisha alikata simu na kuingia garini na kumkuta Black akimsubiri.
"Nambie brother habari ya Chunya?"
"Mmhh mimi si mwenyeji wa huku ni mwenyeji wa Mwanza huku tulimsindikiza mzee Jonathan kwenye shughuli zake za uwindaji sema nini tumechoka sana baada ya kupotea porini humo kwa zaidi ya kilometa ishirini."
"Aisee poleni sana."
"Asante sana brother, vipi mbona unaondoa gari kabla mzee hajafika?"
"Usihofu kaka kasema hapa tuondoe gari tukasimamie mbele kidogo."
"Okay sawa."
Wakiwa wanaeleweshana katika hilo mara simu ya mke wa mzee Jonathan iliingia kwenye simu ya Rashid na kisha aliipokea.
"Ndiyo mama nakusikia."
"Vipi umefika?"
"Nimefika ndiyo namsubiri atokee."
"Okay umewasiliana naye lakini kuwa uko hapo?"
"Yaani wakati yeye anakata simu tu na ya kwako inaingia mama."
"Vizuri mwanangu pole kwa usumbufu lakini?"
"Hapana mama kuwa na amani tu."
"Haya mwanangu nikutakieni safari njema muondoke salama na mfike salama pia."
"Asante mama."
Alipofika eneo ambalo barabara ni pana kiasi aliipaki gari pembeni kuwasubiri mzee Jonathan na Masanja. Kisha aliteremka chini kuangalia kama amelipaki sawa sawa na baada ya kujiridhisha alirudi garini na kuchukua moja ya kiboksi cha chakula na kumkabidhi Black huku yeye akishuka na kuelekea madukani kuongeza chakula pamoja na vinywaji.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA KITAKACHOENDELEA.
#SULTANUWEZO