IMETOSHA MAMA MKWE - 17 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE - 17

sultanuwezotz.blogspot.com 


Mama wa watu akiwa hajui chochote kile aliingia ofisini kwa mkuu wa shule Mr Magoma huku uso wake ukiwa umefunikwa na tabasamu. Baada ya kuingia alitusalimu wote mle ofisini kisha kukifuata kiti ambacho kilikuwa tupu na kuketi. Mr Magoma alimtazama kwa muda kisha aliinuka na kulifuata dirisha lililokuwa karibu na upande aliokuwa kaketi akalivuta pazia na kuchungulia nje kwa dakika kadhaa hivi, bila shaka ilikuwa ni katika kuvuta utulivu wa kuzungumza na mpishi ambaye ni maarufu shuleni kwetu kwa jina la Bi Boko kutokana na siku moja hivi kutuandalia msosi ambao haukuwa sawa ndipo kijana mmoja aitwaye Isaya mwenyeji wa Mbeya akalopoka 'Duu bonge la boko' hatukujua maana yake lakini mara baada kukionja na sisi tukabaini kuwa chakula kilikuwa kibichi. Basi Mr Magoma baada ya kuridhika alirudi kitini na kuketi na moja kwa moja akaanzisha mazungumzo.

"Samahani dada yangu kwa kukutoa kwenye shughuli zako ulizokuwa umezianza."

"Bila shaka mkuu yote ni majukumu tu." Bi Boko alimjibu huku akijichekeshachekesha.

"Vizuri, mbele yako kuna sura ngeni sijui kama umewahi kuziona popote pale sijui." Mkuu alimuuliza.

Alitutazama kwa muda mimi na mama yangu mlezi Bi Matilda kisha alimgeukia mkuu wa shule.

"Hapa mgeni ni huyu dada tu lakini huyu hapa ni mtoto wetu hapa shuleni si anaitwa Christina?" Alimjibu kwa njia swali.

"Sawa sawa hujakosea uko sahihi kabisa dada yangu na ninaweza kusema kuwa ugeni huu wote ni wako wewe." Mkuu alimwambia.

"Haaa karibuni ndugu zangu mimi ndiyo mama lishe hapa shuleni Christina ananifahamu vizuri tofauti na wewe nikiiangalia sura yako naiona ngeni machoni pangu." Aliongea akiwa kamgeukia Bi Matilda aliyekuwa kamkazia macho kama vile anamkadiria sehemu ya kumnyofoa nyama.

" Ni kweli ndugu yangu kifupi mimi ndiyo mama wa Tina na kilichotuleta hapa kuja kuonana na wewe tumeshamueleza mkubwa wako hivyo nimwachie yeye aendelee." Bi Matilda alimjibu na kutulia.

"Sawa sawa, ndiyo mkuu niko tayari kukusikiliza." Aliitikia na kumgeukia mkuu wa shule Mr Magoma aliyekuwa akiketi sawa.

"Ni kweli dada yangu ugeni huu ni wako kama nilivyosema hapo awali na kilichowaleta hapa hasa huyu mama ukimuacha Christina ni kuja kuongea na wewe juu ya kile ambacho ukimefanya inawezekana ni kwa bahati mbaya au makusudi." Mkuu alianza kwa kumpandisha presha mama wa watu ambaye macho yake yalionesha dalili zote za hofu baada ya kusikia maneno ya Mr Magoma.

" Kipi hicho mkuu?" Kwa kuzuga ilibidi amuulize.

" Kuna mawasiliano uliyafanya kwa mtu wako wa karibu huko kwenu juu ya kumuona Tina hapa hatujajua sababu ya kufanya hivyo ilikuwa ni nini japo nimeshaongea awali kuwa inawezekana haikuwa kwa lengo baya lakini kilichozaliwa hapa ndiyo kimesavabisha ubaya." Mkuu alimfafanulia Bi Boko.

" Mkuu ni kama vile bado unaniacha njiani kabisa naomba unifafanulie." Bi Boko ni kama vile mafumbo ya Mr Magoma hakuyaelewa hivyo akaomba ufafanuzi.

" Okay usipate tabu nitakueleza mimi mwenyewe, ni hivi wewe ulimpigia simu mtu huko kwenu sijui ni mume wako au sijui ni nani na kumueleza kuwa sehemu unayofanya kazi ndipo anasoma Christina huku akiwa unafahamu fika kule unakopiga simu kuna mtu aliyehusika na kumjaza ujauzito Tina anasoma ulidhani matokeo yake yangekuwaje?" Maelezo na maswali ya mama yalimchanganya Bi Boko na kujikuta akiuvuta upande wa kitenge na kujifuta jasho japo kulikuwa na baridi sana muda ule.

"Ndugu yangu na mkuu kwanza nianze kwa kukiri kuwa ni kweli kabisa mimi ndiye nilimjulisha mume wangu kule nyumbani juu ya kumuona Christina na haikuwa kwa ubaya bali nilikuwa nikimkumbusha kuwa walimfukuza kipindi kile kwa tatizo la ujauzito lakini kajifungua na anasoma shuleni kwetu na ndipo mume wangu ambaye naye ni mwalimu kule alinijulisha kuwa hata yule kijana ambaye alifukuzwa kwa tuhuma hiyo hiyo ya Tina alirudishwa kuendelea na masomo mara baada ya wazazi wake kuja kumuombea msamaha kwa kilichotokea, hivyo yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida na mume wangu lakini sikutarajia kama angeyafikisha huko yalikofika hata kidogo hivyo ninaomba msamaha wenu maana mimi ndiyo msababishaji." Bi Boko alikiri na kuomba msamaha huku akishuka kitini na kupiga magoti kusisitiza kile alichokizungumza kilitoka moyoni kwani tayari macho yake yalikuwa yameshaloa machozi.

" Naomba unyamaze kwanza dada yangu najua unajutia kwa kile ulichokifanya lakini tayari kimeshatokea unafiri tunafanyaje katika hili?" Mkuu shule Mr Magoma alimuuliza akiwa kamtolea macho yaliyojaa hasira.

"Nafikiri unakumbuka vizuri siku nilipokuajiri nilikuambia nini si ndivyo?" Alimtupia swali jingine.

"Nakumbuka vizuri sana mkuu wangu na kwa hilo ninalijutia kama ujuavyo mazungumzo ya wanandoa yanavyokuwaga sikufikiria kama matokeo yake yangekuwa haya. Christina ninakuomba unisamehe mama yako nimekukosea na niko ya kufanya lolote lile kutumikia adhabu kikubwa nibakie kibaruani." Alishafika miguuni mwangu na kuniangukia huku akibubujikwa na machozi kitendo kilichopelekea mimi kutokwa na hasira zote na kujikuta nikimuonea huruma.

" Nitafurahi iwapo nitaona mbele ya macho yangu ukikabidhiwa barua ya kusimamishwa kazi ni mfanyakazi gani usiyetunza siri za ofisi? Mimi nimechukua hatua juu yako na vipi kuhusu wale uliowafanyia hivi na wakaishia kukaa kimya? Nakuhakikishia kuwa nakula sahani na moja na wewe." Mama Fabiana hakuwa na chembe ya huruma kabisa kwa Bi Boko maana maneno yake na macho yake na vitendo vyake vilimaanisha na hapo nikajikuta njia panda nifanye kipi juu ya Bi Boko na nilipomtupia macho mkuu pale mezani alipokuwa kaegesha mikono yake niliona akigongagonga tu meza kwa kutumia biki yake akiwa hajui afanye nini naye kwenye hili.

"Dada unakubali kuwa umefanya makosa kwa makusudi? Nasema hivyo kwa kuwa ulijua kabisa madhara ambayo yangetokea." Mkuu alifungua kinywa na kumuuliza swali Bi Boko ambalo baada ya kulipima sikujua mantiki yake kwa sababu muhusika alishakiri awali.

"Naombeni mnisamehe ndugu zangu nayajutia makosa yangu sijui hata niseme nini ili mnielewe, lakini nasema tena nimekosa naombeni msamaha wenu." Bi Boko alirudia kuomba msamaha tena na safari hii uzalendo ulimshinda kwani alianza kulia kwa nguvu kitendo kilichonifanya nipige magoti na kumtuliza huku nikimnyamazisha kwani niliguswa na kilio chake ambacho nilihisi kama mtuhumiwa ni mimi mwenyewe. Na baada kuinua macho yangu na kumtazama mkuu niliona kashika karatasi nyeupe na biki mkononi nikajua maana yake ni nini na nilipomtazama Bi Matilda alikuwa kimya tu akikishuhudia kile ambacho kilikuwa kikienda kufanywa na mkuu wangu na hapo ndipo nilipofungua kinywa nikiwa pale pale chini.

"Mkuu nimemsamehe, na ninaomba hata mama yangu hapa afanye hivyo kwa ajili yangu na mwanangu pia." Hakuna aliyetarajia kusikia kile ambacho nilikiongea pale ndani kwani hata Bi Boko naye aliacha kulia na kunitumbulia macho kama vile hajanisikia vizuri.

"Christina umesemaje? Au umerogwa tayari hapo chini baada ya kumgusa?" Bi Matilda aliinuka kitini na kuniuliza maswali ambayo yaliambatana na hasira kwani hakutarajia hata kidogo.

"Wala sijarogwa hata kidogo mama yangu bali nimeyatafakari kwa kina maelezo ya mama yangu hapa nimeona hakuna haja ya kuendelea kumkandamiza katika hili kwa sababu keshasema alikuwa akiongea na mume wake kama vile kumshangaza kutokana na mimi kuwa shuleni wakati nilifukuzwa kipindi cha nyuma tatizo likawa kwa mume wake aliyeongoza kwa Meshack japo naye hakujua kama kuna mgogoro kati yetu yawezekana alijua tuna mawasiliano. Hivyo sioni haja ya kuushikiria msamaha huu." Maelezo yangu yalimwinua mkuu wa shule kitini na kumfuata mama Fabiana na kumnong'oneza kitu sikioni kisha walitoka nje wote na kutuacha pale ndani ambapo sikuona sababu ya kuendelea kubaki hivyo na mimi niliwafuata na kuwakuta wakiongea na baada ya kuniona mama alimwambia mkuu wa shule kuwa afanye kama nilivyosema mimi kisha akanigeukia na kunitaka tuondoke mahali hapo. Niliagana na mkuu wa shule Mr Magoma.

"Hakikisha kuwa kesho hukosi shuleni sawa Tina?" Mkuu aliniambia akipanda ngazi kuelekea ofisini kwake na mimi nikamuitikia kwa kichwa nikimfuata mama ambaye tayari alikuwa hatua nyingi kidogo kutoka nilipokuwa.

"Ndiyo umefanya nini sasa?" Lilikuwa ni swali lake baada ya kumfikia pale alipokuwa kasimama.

"Najua umenichukia kwa nilichokiamua juu ya Bi Boko." Nilimjibu.

"Bi Boko ndiyo jina lake?" Aliniuliza baada ya kulisikia jina la Bi Boko.

"Hapana ni jina la utani tu, lakini yote kwa yote naomba unisamehe mama yangu kumbuka kuwa wewe ndiyo uliyenifundisha kusamehe." Nilimjibu mama yangu mlezi Bi Matilda.

"Wala usijali mwanangu limeisha hilo kwanza fahamu kuwa umenisaidia sana maana nilikuwa kwenye wakati mgumu sana mle ndani na sikujua niamue kitu gani hasa baada ya kumsikia mtu mzima akitokwa machozi na akijutia kile alichokifanya niliishiwa pozi mwanangu lakini kama bahati vile ndipo nilipokusikia wewe jasho jembamba lilinitoka nikahisi kama vile nimeutua mzigo mzito kichwani kwangu." Bi Matilda alinieleza kitu ambacho sikukitarajia hata kidogo huku kanikumbatia huwezi amini ilibidi niangue kicheko pale pale.

" Unanicheka sasa? "Aliniuliza akiisimamisha Bajaj.

" Hapana mama bali nimeivuta picha ya sura ilivyokuwa mle ndani nikifananisha na maelezo yako hapa sasa nimejikuta ninaanza kucheka." Nilimweleza kitu ambacho naye alianza kucheka.

" Chezea Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya." Nilimtania nikimkumbatia Bi Matilda.

" Pumzi ilimkata ghafla Afisa Maendeleo wa watu." Bi Matilda alinijibu huku akiiangalia simu yake ambayo ilikuwa na miss call' za mama.

"Unaona sasa kilichotokea? Mama yako kanipigia mara kibao lakini sikuweza kumsikia maana simu niliweka kwenye 'vibration' sijui watakuwa wameshafika?" Alinieleza huku akiitazama saa yake kisha akampigia mama kujua kafika wapi.


     JE NI NINI KINAKWENDA KUTOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII KUJUA KITAKACHOJIRI.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post