MTOTO MALATWE - 16
sultanuwezotz.blogspot.com
Walijiandaa na kuungana na wenyeji wao sebuleni kwa ajili ya kifungua kinywa. Ilikuwa ni asubuhi yenye baridi sana siku hiyo kwani mpaka pale sebuleni ubaridi ulikuwa unapenya kiasi cha kuwafikia ndani. Hali hii ilikuwa ya kawaida kwa wenyeji lakini kwa wageni ilikuwa ni changamoto japo walianza kuizoea hali ile.
" Wanasemaga kuwa ukiona baridi kali kiasi hiki basi unatakiwa kuwa makini na chai ya maziwa, sijui kuna ukweli ndani yake?" Bi Priscilla aliuliza akimimina chai kwenye kikombe.
" Kwa kuwa uko eneo husika huna haja ya kuuliza cha kufanya ni wewe kujaribu." Mume wake alimjibu.
" Shemeji huna nia nzuri na mke wako, yaani afanye jaribio la kuungua? Usijaribu dada yangu tutashuhudia vipande vya nyama vyama hapa ohhohh!!" Mke wa Innocent aliona apingane na majibu ya mwalimu Vincent alihisi anaweza kusababisha matatizo yasiyo ya lazima. Chai iliendelea kunyweka pale mezani huku utani wa hapa na pale ukichukua nafasi mahali pale na baada ya kumaliza walifanya maandalizi na kutoka kuelekea mjini kufuatilia suala la Malatwe.
" Mtoto tunamuacha mdogo wangu utamchukua kama ataamka hatutakawia kurudi." Bi Priscilla alimwambia dada wa kazi wakiingia kwenye gari.
" Sawa dada." Aliitikia akiwaaga na kurudi ndani huku wao wakiondoka. Safari yao ilitia breki kituo cha Polisi na mwalimu Vincent akiwa kaongozana na rafiki yake mwalimu Innocent walishuka garini na kuingia kituoni huku wake zao wakisalia kwenye gari kuwasubiri. Walimkuta askari wa zamu ambaye alipekua faili husika baada ya kupokea maelezo yao na baada kulisoma kwa muda aliwatazama kwa zamu kisha akawapa maagizo aliyopewa na watangulizi wake.
" Kwa hiyo tunaweza kuondoka Afande?" Mwalimu Vincent alimuuliza.
" Mko huru tu, kesi kama hizi kwa mji wa Makambako ziko nyingi sana na huyu kadanganywa na makundi yote kwa yote kama atapatikana tutawajulisha bila tabu." Aliwajibu.
" Mimi nitaendelea kufika hapa kufuatilia na hata namba zangu itabidi niache kwa tahadhari maana kaka hapa yeye anaishi mbali na hapa mjini hivyo mimi kuacha namba kutarahisisha zaidi." Aliongeza mwalimu Innocent.
" Itakuwa vizuri zaidi, andika namba yako hapa." Alimkabidhi diary nyeusi aandike namba yake. Na baada ya kukamilisha taratibu zote walitoka na kurudi kwenye gari ambapo hawakupoteza muda waliondoka na safari haikuwa nyumbani bali walitoka nje ya mji.
" Safari ya wapi tena kijana?" Aliuliza mwalimu Vincent baada kuona gari linakunja kushoto badala ya kulia na kukamata barabara ya Njombe.
" Haa hivi hatukuwaambia asubuhi?" Aliuliza badala ya kujibu huku akicheka.
" Tulisahau nafikiri baada ya kulijadili tukabaki nalo wenyewe tusameheni bure ndugu zetu, tulipanga kuwa tukitoka hapa tutakwenda mara moja shamba ili mkaone tunavyopambana na maisha wenzenu." Bi Benabela alieleza.
" Kwa hiyo ndiyo tunaelekea huko sasa?"
" Kama kawaida kaka mkubwa." Mwalimu Innocent alimjibu akikata kona kuelekea uwanja wa Mashujaa uliogeuzwa soko la mbao la Makambako.
" Wala haina shida ila ninachowaza ni mwanangu akianza kusumbua itakuwaje?" Bi Priscilla alihoji.
" Shemeji yangu usitie shaka katika hilo kule hatuendi kukaa sana hivyo tutawahi tu." Mwalimu Innocent alimjibu.
" Na hii ni shule gani?" Bi Priscilla aligeukia swali jingine baada kuyaona majengo upande wao wa kulia.
" Hiyo ni Makambako Sekondari na kule mbele yanakoonekana majengo mapya ndiyo Ofisi za Halmashauri ya mji." Bi Benabela alimfafanulia kwa urefu zaidi.
" Aisee kumbe hii ndiyo Makambako Sekondari?" Aliuliza kwa kushangaa.
" Uliwahi kuisikia?" Mume wake alimuuliza.
" Ndiyo, kuna rafiki yangu mmoja kitambo hicho alikuwa akirudi likizo alikuwa anatutambishia sana hii shule kumbe ni hii?"
" Ndiyo hii kwa hapa Makambako na viunga vyake zipo nyingine kama Naboti Sekondari, Mama Clementina Foundation Sekondari, Genesis Sekondari, Mkilima Sekondari, na nyingine nyingi bila kusahau Chuo Kikuu cha St. Joseph hivyo siyo mji wa kubeza hata kidogo." Aliendelea kumfafanulia.
Na wakati walikuwa wakiporomoka kwenye mteremko uliokuwa ukiwapeleka mtoni. Na ndani ya dakika kadhaa walikuwa wakiupandisha muinuko na tayari walikuwa ndani ya kijiji fulani hivi ambacho wageni hawakukitambua. Walisonga mbele mpaka nje ya nyumba moja hivi iliyokuwa imezungushwa fensi ya mianzi na kusimama.
" Wageni karibuni sana hapa ni kwangu jisikieni nyumbani." Mwalimu Innocent aliongea akifungua geti la mianzi baada ya kushuka kwenye gari.
" Makubwa haya, kwa hiyo hapa ndiyo shambani?" Mwalimu Vincent aliuliza akishuka.
" Kaka punguza presha hatua moja huanzisha nyingine karibuni ndani." Aliwakaribisha ndani. Huku Bi Benabela akimuonesha ishara Bi Priscilla ya kuingia ndani wakati huo mume wake akiufungua mlango wa sebuleni.
" Shemeji huku ndiko anakofanyia kazi mdogo wako zile nyingine zilikuwa mbwembwe tu hapa panaitwa Itipingi na shule inaitwa Itipingi Sekondari." Bi Benabela alitoa ufafanuzi.
" Haa ina maana mwenzangu ulipanda ngazi?"
" Ndiyo kaka baada ya kuanza kazi tu nilisubiri miaka mitatu ikapita na kipindi hicho nilikuwa nafanya mitihani ya kidato cha sita. Mwanzo nilipata changamoto sana si unajua tena unasoma ndani ya mwaka mmoja unapiga mtihani kwa hiyo nilichemka mara mbili kwa 'kuscore' sifuri kabisa lakini sikurudi nyuma nilipiga moyo konde mpaka pale nilipofanikiwa kupata 'B' kwenye masomo ya 'Geography' na 'History' huku yaliyosalia nikipata 'C' haraka sana nikaanza harakati za kuomba Chuo na kwa bahati nzuri nilifanikiwa kujiunga na Chuo cha TEKU Mbeya na baada ya kumaliza kozi yangu nilirudi kuendelea na kazi kwenye kituo changu cha Itipingi shule ya msingi mpaka pale mkuu wa shule ya Sekondari aliponiambia kuwa kuna nafasi za kujazia hivyo kama niko tayari nimwambie tuuanze mchakato. Tulianzia hapo mpaka hivi ni mwalimu wa Sekondari." Maelezo marefu ya mwalimu Innocent yalionekana kumvutia rafiki yake ambaye mpaka muda huo hakujua kama mwenzake ni mwalimu wa Sekondari.
" Aisee hongera sana bwana mdogo kwa hatua hii yaani mimi muda wote nilijua ni wa daraja langu kumbe siyo."
" Hapana kaka sisi wote ni wa daraja moja kwani tunatambulika kama Elimu msingi." Alimjibu wakati huo wake zao wakiwa kwenye kishamba wakichuma mboga mboga.
***
Hii siku kwa upande wa Malatwe ilikuwa ndefu sana kutokana na yale aliyokuwa akikutana nayo kwa wenyeji wake, lakini bado alijipa muda wa kuendelea kutulia. Mpaka ilipofika saa nne asubuhi ambapo Naboti alimwambia watoke kidogo wakatembee ili ayafahamu mazingira ya kijiji cha Itipingi. Walikwenda mpaka kilabuni anakouziaga pombe za kienyeji na ulanzi. Kazi ile ilimchosha sana Malatwe kwani hakuwahi ifanya hata mara moja mpaka alitamani kumkimbia.
" Kumbe uko vizuri kwenye kazi?" Alimwambia Malatwe akiwa anasafisha vyombo vilivyotumika.
" Vizuri wapi kaka nilikuwa najaribu kuendana na aina ya mdundo si unafahamu ukiingia disko staili ya kucheza unaikuta hapo hapo?" Malatwe alimjibu.
" Sikutarajia kabisa kama itakuwa hivi lakini umenisaidia sana mdogo wangu nashukuru." Naboti alimshukuru.
Walifunga vifaa vyao kwenye pikipiki kisha wakarudi zao nyumbani. Walimkuta mwenyeji wao akiwa anaendelea na upishi.
" Karibuni."
" Asante mke wangu, vipi umeshindaje?"
" Salama, poleni na majukumu."
" Asante shemeji."
" Umekutana na shughuli zetu ee?"
" Nimekutana nazo lakini siyo ngumu nimezipiga ile mbaya."
" Kweli?"
" Muulize kaka usikie." Malatwe alijinasibu mbele ya shemeji yake. Wakati huo huo Naboti alirudi kutoka kuongea na simu kisha akapitiliza ndani ambako hakuchukua muda alitoka na kuwasha pikipiki.
" Wapi tena?" Mke wake alimuuliza.
" Narudi muda si mrefu sana." Akawasha pikipiki na kuwaacha hapo hapo.
" Mhhh." Aliguna tu mke wake na kuendelea na mapishi.
" Kunanini shemeji mbona unaguna wakati mwenyewe kaondoka?" Malatwe alimuuliza.
" Hakuna kitu shemeji kama unasikia baridi njoo huku jikoni." Alimjibu.
Kwa muonekano wa nje tu ilionekana Bi Judith hakuwa sawa hali iliyomfanya Malatwe kupata maswali juu yake. Hivyo aliamua kumfuata jikoni alikoingia ili akajue kulikoni.
" Keti kwenye kiti Malatwe." Alimkaribisha.
" Nishafika shemeji." Alimjibu akikaa kwenye kiti kilichokuwa karibu na jiko la moto.
" Naona umeifurahia siku leo."
" Kivipi shemeji?" Malatwe alimuuliza.
" Nauona tu uso wako ulivyochanua tofauti na ulivyofika."
" Nahisi ni macho yako tu shemeji lakini mimi najiona ni yule yule." Malatwe alimjibu akiugongagonga moto.
" Halafu hilo jina la shemeji mimi silitaki na silipendi pia, niite kwa jina langu la Judith tu itapendeza." Bi Judith alimgomea Malatwe kumwita shemeji.
" Lakini nimeshazoea hivyo shemeji."
" Ndiyo nimelikataa kama unalipenda jiite mwenyewe lakini siyo mimi, nimekukumbusha jina langu naitwa Judith jamani."
" Okay sawa tufanye kuwa ndiyo nakuita Judith.. " Kabla hajamalizia Bi Judith alidakia.
" Abee!!"
" Nini sasa?"
" Si umeniita mwenyewe." Alimjibu.
" Hapana mimi nilikuwa nataka kukuuliza swali hivyo sikuwa nakuita."
" Swali gani hilo?"
" Ni hivi, ikiwa nitakuwa nakuita kwa jina itakuwaje kwa kaka Naboti akisikia?" Malatwe alimuuliza.
" Hilo ni rahisi sana mtu wangu, akiwepo wewe niite shemeji lakini asipokuwepo niite jina langu, sawa eee.. " Bi Judith alimjibu akimalizia na kikofi kidhaifu begani kwa Malatwe.
" Sawa japo naogopa."
" Acha uoga mtoto wa kiume, halafu nilitaka kusahau Malatwe hivi mkiwa kilabuni hakuna mwanamke yeyote ambaye alikuwa karibu na mume wangu?"
" Hapana sikuona yeyote ukizingatia nilikuwa bize na kusafisha zile lita za kuuzia pombe." Malatwe alimjibu.
" Nilitaka kushangaa yaani usimtetee mwanaume mwenzako? Lakini nitajua tu." Aliongea na kutoka nje ambako moja kwa moja alikwenda ndani na muda mfupi baadaye alirudi akiwa na sufuria ambalo alilitenga motoni.
" Mhh kupika umeahirisha shemeji?"
" Umesemaje? Malatwe usitake kunikwaza muda huu."
" Kujisahau Judith wala si maksudi."
" Hilo ni moja ulirudia nakugeuza mboga." Malatwe alimtumbulia macho Bi Judith wakati akiongea hilo sijui aliwaza nini, lakini muda huo huo mlango uligongwa.
" Tuko huku jikoni." Bi Judith alimjibu mgongaji. Alikuja na kubisha tena hodi.
" Karibu."
" Asante, habari ya jioni dada."
" Aaa kumbe ni Hussein?"
" Ndiyo dada ni mimi."
" Lete habari kijana wangu wa nyeti."
" Nimeagizwa huu mzigo na mwalimu Danda."
" Mwalimu Danda?" Aliuliza kwa mshangao.
" Ndiyo."
" Yuko wapi na kasemaje?" Alimuuliza akitoka nje na mfuko mkononi.
" Kaondoka muda si mrefu alikuwa na haraka sana."
" Haraka? Kama alikuwa na haraka alifuata nini kwangu si angebaki na haraka zake huko huko?"
" Hakuwa peke yake alikuwa na watu wengine watatu kati yao nilimfahamu mmoja tu wale wengine sikuwafahamu."
" Mke wake siyo?" Alimkazia macho Hussein.
" Huyo huyo, dada mimi nawahi nyumbani ila kasema kesho au muda wenu atakupigia simu muongee." Hussein aliaga na kuondoka.
" Wee haya dogo, karibu tupike."
" Niko vizuri." Alijibu na kuondoka. Aliingia ndani kuweka ule mfuko kisha alirudi jikoni.
" Mazawadi gani tena ndugu yangu?" Malatwe alimuuliza.
" Mtoto wa kiume umbea haukufai hata kidogo, labda nikwambie kitu kimoja ambacho kitakusaidia maishani mwako, ukitaka uishi na mimi vizuri jifunze kupiga zipu hilo domo lako tofauti na hapo nitakuhamisha kabla ndugu yako hajakusaidia, umenielewa?"
" Nimekuelewa nitazingatia."
" Nimemaliza na sirudii tena. Uliuliza kuhusu kulitoa sufuria la ugali motoni?" Alimaliza na kuuliza swali.
" Ndiyo."
" Ndani hakuna chochote na kaka yako kaondoka kurudi hapa ni kesho au keshokutwa."
" Makubwa, kaenda wapi?"
" Akirudi jitahidi kumuuliza maana si wajibu wangu kumjibia maswali yeye." Alimjibu.
" Kama naanza kuiona migongo ya bati."
" Tena itasaidia sana kwani toka tuijenge hii nyumba sijawahi kujua mabati yote yana migongo mingapi." Bi Judith alimjibu akiwa kambinulia midomo yake. Ukimya ulitawala mle jikoni huku Malatwe akizidi kumuangalia Bi Judith bila shaka kuna jambo alikuwa analifuatilia usoni mwake kwani japo alikuwa akiongea naye lakini alionekana mwenye mawazo sana.
Mara ni kama alipata wazo fulani kwani aliinuka na kutoka nje lakini safari hii hakuingia ndani bali alitoka nje ya uwa. Malatwe hakutaka kupitwa na hili hivyo kwa tahadhari kubwa alitoka na kuanza kumfuatilia kwa nyuma. Japo kagiza kalianza kukomaa lakini hakupata shida kumuona shemeji yake alikokuwa akielekea hivyo naye alizidi kumfuatilia nyuma nyuma mpaka alipoingia kwenye nyumba fulani hivi ya bati. Malatwe naye bila ajizi aliongoza nyuma ya nyumba hiyo mpaka lilipokuwa dirisha na kujibana hapo huku masikio yake akiwa kayatega kwenye ukutani kutaka kujua kinachoendelea humo ndani.
" Inawezekana ule mfuko umetoka hapa japo alinizuga." Alijisemesha mwenyewe akiwa bado anasikilizia. Mara alianza kusikia makelele kutoka ndani ya nyumba hiyo na hayakuwa makelele ya kawaida, hivyo Malatwe aliangaza huku na kule kuona kama anaweza kuona mtu lakini wapi akajitoa mzima mzima kuuendea mlango ili aingie kutoa msaada lakini baada ya kufika mlangoni alisita kidogo.
" Hivi nikiingia humo ndani nitaonekanaje mbele ya shemeji si atajua nilikuwa nafuatilia? Nifanyaje hapa? Na huyu anayempiga ni nani?" Alijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu na kuamua kuondoka ili kwenda kutafuta msaada kwa majirani hivyo alitoka mbio mpaka kwenye nyumba moja hivi ya nyasi.
" Wenyewe hodi, hodi, hodi wenyewe!!"
" Veyaa karibu, wingile ndilikhuno (ingia niko huku)" Alikaribishwa.
" Sijui unachoongea bibi, naomba uongee Kiswahili tafadhali." Malatwe aliomba abadilishiwe lugha.
Muda mfupi bibi wa hiyo nyumba alitoka mpaka nje na kumkuta Malatwe mlangoni akimsubiri.
" Nikusaidiye nini mjukuu wangu?" Alimuuliza.
" Bibi kuna tatizo?"
" Tatizo? Tatizo gani?" Alimuuliza tena.
" Tafadhali bibi naomba tuongozane huku ukanisaidie kumuokoa shemeji yangu anapigwa."
" Wapi huko?" Bibi wa watu alimuuliza.
" Naomba nifuate." Akiwa kamshika mkono akimvuta.
" We kijana utaniangusha hebu niachie nitembee mwenyewe." Bibi aliona spidi ya Malatwe ni kubwa hivyo akaona aombe kuachiwa mkono wake.
" Bibi watamuua shemeji yangu." Malatwe alirudi na kutaka kumshika tena mkono lakini mzee huyu aliukwepesha. Lakini wakiwa bado kwenye mvutano kati yao mara wakasikia sauti na vicheko vya watu wakija upande wao ikabidi Malatwe atulie kwanza.
" Haa huyu si shemeji Judith? Mbona ana furaha zote na huyu aliye naye ni nani wakiwa wanafuraha kiasi hiki?" Malatwe alihisi anajiuliza kimoyo moyo kumbe alijiuliza kwa sauti ambayo ilimfikia yule bibi.
" We kijana kwa hiyo ulikuwa unakuja kwa Omary?"
" Omary ndiyo nani?" Malatwe aliuliza.
" Si huyo kijana aliye na Judith."
" Kumbe unawafahamu bibi? Mimi nilikuwa namfuatilia nyuma shemeji baada ya kutoka nyumbani bila kuaga lakini safari yake iliishia kwenye nyumba ya pale chini ndipo nilipomsikia shemeji akilia kwa sauti ya juu kama vile alikuwa akiadhibiwa ndiyo niliona nitoke kuja kuomba msaada." Malatwe alitoa maelezo.
" Mjukuu wangu una umri gani?" Yule bibi alimuuliza Malatwe baada ya kutoa maelezo marefu.
" Kwa sasa ni kama nina miaka kumi na mitatu au minne hivi sina uhakika sana maana mama hakuwahi kuniambia miaka yangu."
" Nakuomba urudi nyumbani kwanza kisha kesho ukipata muda njoo kwangu nikupe mkasa, lakini nakuona ni mgeni hapa kijijini?"
" Ni kweli kabisa mimi ni mgeni bibi naomba niende kesho nitakuja mapema."
" Karibu sana." Bibi aliagana na Malatwe kisha akarejea nyumbani kumuwahi Bi Judith.
JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KITAKACHOTOKEA.
#SULTANUWEZO