NITAKUUA MWENYEWE - 66 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 66

sultanuwezotz.blogspot.com 


Athuman na Shamimu waliwasili pale kona za mkoa karibu na kijiji cha Lwanjiro kilicho Mbeya vijijini wakiwa na vyakula vyao. Baada ya kutelemka kutoka kwenye basi linalofanya safari zake Mbeya kwenda Chunya waliungana na wakina Jackline pale walipokuwa.

"Wao ndiyo maana ninawapendaga ndugu zangu asanteni kwa kunijali dada yenu."

Jackline aliongea akiwakumbatia Athuman na Shamimu.

"Usijali dada yetu wewe mwenyewe unafahamu tumebakia wangapi? Lakini kuna muda hutushangaza sana dada Jack."

Athuman aliongea.

"Kivipi Athuman?"

"Si kuwa ndani ya Mbeya bila sisi kujua chochote."

Shamimu aliingilia.

"Naombeni mnisikilize wadogo zangu, nayafanya haya yote ili kurahisisha maisha yetu ya baadaye kama mnavyojua hatuwezi kuishi maisha ya ndoto zetu kama mzee Jonathan na wengine waliojitokeza kuendelea kuishi hapa duniani na ndiyo maana nikaamua kuibeba hii vita kwa gharama yoyote ile, na wale pale ni rafiki zangu waliojitoa kunisaidia japo nao wametendwa pia hebu tusogee niwatambulishe kwao."

Aliongea hayo huku akisogea nao pale walipokuwa wameketi wakina Jasmine.

" Naona uko na ndugu zako, yaani mmefanana sana aisee."

Jessica aliongea baada ya kufika wakina Jackline.

" Ni kweli Jessica hujakosea sisi ni ndugu na huyu hapa ni Shamimu na huyu ni Athuman taarifa zao nilishawaeleza."

Jackline aliwatambulisha wadogo zake kwa timu yake.

" Wadogo zangu hawa ni rafiki zangu kama nilivyowaambia huyu ni Jasmine na huyu hapa ni Jessica nao ni ndugu wa damu lakini pia tuko na Roberto kama mnavyomuona pale kwenye ile gari akiwa anahakikisha mzee Jonathan hainui hata kichwa chake na huyu hapa ni Titiana mpenzi wa Roberto naye kaamua kuachana na likizo pamoja na masomo na kuungana basi kwenye oparesheni yetu."

Alimaliza utambulishi wake.

" Ndugu zetu mnavyotuona hivi sisi ni ndugu wapya kutokana na familia zetu kusambaratishwa na wabaya wetu katika Mazingira tofauti ya kiutafutaji."

Jasmine alijazia maelezo ya Jackline.

" Jamani sisi tumefurahi kuwaona na kuwafahamu tunaamini baada ya hii oparesheni kuna hadithi mmeibeba ambayo mtatusimulia kwa sasa hatupendi kuwasumbua kutaka kujua nini kinaendelea."

Athuman aliongea hayo huku akimpa ishara Shamimu ya kumuonesha Jackline vile walivyovinunua.

" Usijali Athuman kama tulivyosema kuwa sisi ni familia moja kwa sasa tunaipigania haki yetu iliyopokwa na watu wenye roho mbaya lakini tunachowaomba ni kuendelea kutuombea kwani vita hii ni kubwa sana na msije shangaa leo hii mnatuona watano kwa idadi lakini baada ya vita hii tukawa hivi hivi au pungufu hivyo kwa kila hatua yenu kila siku hakikisheni mnatuombea turudi salama kwani baada ya hapa tunarejea Brazil."

Maneno hayo yalizungumzwa na Roberto ambaye alifika pale baada ya kuwaona wakina Athuman wakiwa na mifuko ya mapochopocho na mwishoni mwa nasaha yake alimwaga machozi kitendo kilichoungwa na kila mmoja pale na kuwaduwaza wakina Shamimu ambao wao hawakujua chochote kilichopelekea waanze kulia lakini baada ya kufuta machozi yao walisogea na kukumbatiana kwa pamoja kama ishara ya umoja kwenye vita ulivyo mbele yao.

"Tunawapenda sana lakini ndiyo hivyo bado tuko kwenye Uwanja wa vita kwenye hiyo gari hapo mbele ndimo tulimowafungia mzee Jonathan na mke wake ikiwa ni dalili njema kuelekea kuishinda vita hii."

Jackline alijazia nyama kwenye maneno ya Roberto.

"Tutaendelea kuwaombea kuanzia leo kesho na wakati wote wa zoezi hili."

Shamimu aliona naye azungumze yake yaliyo moyoni mwake.

"Kwa upande wangu naomba niongozane nanyi kwenye vita hii mliyoianzisha ndugu zangu."

Athuman aliomba kuingia vitani,lakini hakuwa kuikuwa rahisi kwake kukubaliwa katika hilo.

"Kama tulivyosema hapo awali kuwa hii vita ni yetu wote kila mmoja anapigana kwa njia yake na ndiyo maana tukawaomba mtuombee tu hiyo nayo ni shirika katika vita hii lakini kusema tuongozane hapana Athuman kwa hapa tulipofikia ni pabaya sana kwani mimi mwenyewe nimeingilia katikati mpaka naogopa hivi lakini namshukuru mpenzi wangu kanitia moyo hivyo naombeni mrudi nyumbani tuombeeni tuishinde hii vita ili siku ya mwisho tufungue shampeni ya ushindi."

Maneno ya Titiana yalimuacha mdomo wazi kila mmoja kwani si mtu wa kuongea ongea sana lakini akifungua mdomo wake hutema madini.

"Tumewaelewa ndugu zetu, tunawatakia mafanikio mema katika hili na nina Imani kubwa mnakwenda kuishinda kwa mlipofika tu ni ushindi tayari."

Shamimu aliwajaza matumaini.

"Tuendelee kumuomba Mungu atende miujiza katikati yetu."

Roberto aliongea hao akiondoka kuelekea kwenye gari anayoifanyia ulinzi.

"Dada tuongee mara moja."

Athuman alimtaka dada yake waongee kidogo.

"Okay sawa." Walisogea pembeni kidogo kuteta.

"Najua tuko kwenye kipindi gani dada lakini kwa kuwa nimepata nafasi ya kuonana nawe na kuuona muonekano wetu ulivyo, kifupi dada yangu mambo si shwari kabisa kwani biashara zangu zilisimama muda mrefu kinachoniweka mjini ni kuotesha maua ambayo kwa sasa soko limeshuka nadhani ni kutokana na mtaji kwani wengi wetu wanaofanya shughuli hii wamewekeza kweli kweli hivyo niombe kama una salio kidogo nipige kampani dada ili mambo yaende."

Athuman aliongea kile ambacho alipanga kumwambia dada yake.

" Usijali mdogo wangu nimekuelewa katika hivyo kuna kahela kidogo nitakuingizia kwenye akaunti yako kikubwa unipe akaunti namba yako na hapa kuna kiasi kidogo kitasaidia kwa siku kadhaa."

Jackline aliongea akiingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha fedha na kumkabidhi Athuman kisha walikumbatiana na kurudi kwa wenzao. Na kwa kuwa ilikuwa tayari ni magharibi waliagana na wakina Shamimu walisimamisha basi na kupanda wakaondoka zao huku nyuma wakina Jackline nao walitulia kupata chakula  tena na kuwasha magari yao na kutimua vumbi ila pamoja na yote kitu walichowafanyia wakina Jonathan ni kuwanyima chakula bila shaka adhabu imeanza kufanya kazi yake.

Safari iliendelea na hatimaye waliwasili mjini Lupa na kukita breki zake nyumbani kwa mzee Kaaya nyumba ambayo miaka kadhaa Jackline aliiishi akiwa kama mmoja wa wanafamilia kama mkwe na sasa kaja tena kama nani hapo. Mzee Kaaya akiwa ndani kalala alisikia mlio wa gari nje ya nyumba yake na baada ya kuchungulia nje kupitia dirishani aliweza kuona taa za gari nje. Alimuamsha mke wake na kumuonesha kilichopo nje mara mlango uligongwa. Bado walibaki kuulizana ni wakina nani hao wanaogonga mlango nje? Kelele za mlango ziliwaibua na kuufungua lakini kitu walichokutana nacho hawakuamini macho yao kwani walikutana na tochi iliyowamulika machoni kitendo cha kutoona mbele na hapo walidakwa na kufungwa vitambaa usoni na kupigwa cheni mikononi na kupakiwa garini kwani Roberto aliifanya kazi yako bila woga wowote huku akisaidiana na Jasmine na Jackline akisalia garini. Baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa Jasmine aliifunga milango ya nyumba ile kisha alirudi garini na kisha waliondoka zao na safari hii ilikuwa ni kuelekea njia ya njia ya Tabora.

"Jamani huku kuna baridi kuliko hata ile ya Mbeya mjini?"

Titiana aliona aongee baada ya kuona baridi inapuliza sana na muda huu ilikuwa ni usiku mnene wa saa sita usiku.

"Mkoa mzima wa Mbeya unabebwa na baridi kama hivi."

Jackline alimjibu Titiana ambaye walikuwa naye kwenye Honda jet5.

"Hivi dada Jackline safari hii tunakwenda kuishia wapi?"

Jessica aliuliza.

"Tunakaribia kufika unajua nini? Kuna pori moja linaitwa Kipembawe huko kuna ndiko tunakwenda kufanya yetu."

Alijibu Jackline huku akiendelea kupiga gia.

"Na hawa wazee inakuwaje?"

Jessica aliuliza tena.

"Kuwa mpole mdogo wangu muda ukifika utajua subiri tushuke."

Alimjibu tena na ikabidi Jessica awe mpole na baada ya kufika ndani ya msitu wa Kipembawe gari ziliacha njia na kuingia porini huko walitia breki karibu zaidi na kilima na kisha kuwashusha watu wao na kuwapeleka moja kwa moja mpaka kwenye pango moja ambalo linaonekana hutumiwa na Majangili kwani japo liko ndani sana lakini lilikuwa lina joto la kutosha na kulikuwa na vitu kama mikeka, ngozi ngozi za wanyama kwao haikuwatisha waliwaingiza ndani watu wao na kuwafunga cheni nyingine miguuni na kisha kuwafungua vitambaa na pale ndipo mzee Jonathan hakuamini macho yake baada ya kukutana na sura ya Jackline.

"Mzee mbona unatoa mimacho kiasi hicho?"

Jessica aliongea wakati huo akisaidiana na Titiana kuwaweka kila mmoja sehemu yake huku Roberto akiwa nje ya pango kwenye gari kuutoa mwili wa Masanja ambaye tayari mwili uliachana na roho kwani risasi ambazo zilimtwanga hazikumuacha salama alishakufa hivyo Roberto alimtoa na kwenda kumtupa mtoni. Na kisha kurejea kuungana na wenzake.

"Jackline ni wewe kweli?"

Mzee Jonathan aliuliza kwa mshangao mkubwa.

"Unashangaa nini mzee wangu si ulisema kuwa uko China? Na kwanini umebadili muonekano wako? Nilisikia kuwa ulimwaga mihela kunitafuta mimi ili iweje?"

Jackline alimjibu na kumtwanga maswali mfululizo.

"Mwanangu na mimi mbona umenileta huku?"

Mzee Kaaya alimtupia swali Jackline kabla mzee Jonathan hajajibu maswali ya Jackline.

"Mzee naomba ukae kimya wewe na mkeo kesi yenu inakuja kwa sasa niko na huyu Rastaman na mke wake haka kadereva kameingia mkenge kwenye kesi isiyokahusu."

"Mwanangu naomba naomba sana unisamehe kwa niliyokufanyia najua una hasira na mimi."

Mzee Jonathan alianza.

"Naomba uyajibu maswali yangu sihitaji kingine."

Jackline alimkatisha maneno yake ya maigizo.

"Mwanangu nisamehe tu yote haya ni kwa ajili ya Uroho wa Mali si kingine."

"Unasemaje mzee?"

Roberto alimsogelea mzee Jonathan na kumpiga swali akiwa kamshika mashavu.

"Mwanangu naomba nihukumiwe mimi na mume wangu aachiwe sababu mimi ndiye chanzo cha yote haya maana nilimshawishi kwenda kwa mganga wa kienyeji ili kuzipora Mali zenu na ndicho kilichotokea na kusababisha ajali iliyowaua wote na sisi kujibebea Mali zenu zote na kujifanya watu wema kwako na kukupeleka nje ya nchi kwa masomo na huku nyuma ilikuwa ni nafasi yetu kujiimarisha kumiliki Mali zenu... "

Kabla hajamalizia neno lake alikutana na ngumi ya mdomo kutoka kwa Jasmine iliyompeleka chini na kuanza kutoa damu mdomoni kitendo kilichomfanya mzee Jonathan kuanza kutokwa jasho kwani alishajua nini maana ya kuletwa mle Pangoni.


NINI KITATOKEA HUMO?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.


     #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post