IMETOSHA MAMA MKWE - 57
sultanuwezotz.blogspot.com
Maskini Jofrey alipozinduka na kubaini kuwa wako katikati yetu alimtazama Bi Kiziwa kisha mama yake bila shaka kuna kitu alitaka kuwaambia lakini hakuweza kutokana na madawa ambayo walimwagiwa dakika chache zilizopita ambayo yaliwanyong'onyesha nguvu na kuwafanya kuwa kama misukule iliyokosa chakula kwa muda mrefu. Jofrey hakukubali hali ile iendelee kumtafuna alichokifanya alianza kutambaa kama nyoka kumfuata mama yake na kama bahati vile alifanikiwa kumfikia na kitu cha kwanza kukifanya alimvamia mwilini na kuanza kumpiga mangumi, kituko kilikuwa pale ambapo akirusha ngumi ilikuwa haifiki popote kutokana na mwili kuishiwa nguvu.
"Yaani siamini macho yangu yaani mwanangu uliangukia kwenye mikono ya hawa wala watu? Hebu waangalie walivyo sura zao kwanza." Mama aliniambia baada ya kutufuata tulipokuwa na Rachel. Nilishindwa nimwambie nini mama yangu badala yake nilianza kulia kwa sauti na nikainuka kuwafuata pale walipokuwa wametulizwa lakini nilipotaka kuingia ndani ya dimba tu Rachel alinifuata na kunizuia.
"Dada unakwenda wapi na kufanya nini haujaambiwa kuwa eneo hili ni hatari kwa sasa?" Rachel aliniuliza.
"Niachie mdogo wangu nikawaoneshe njia iliyo sahihi wanyama hawa." Lakini Rachel hakuniachia alinivuta mpaka kwenye gari na kunitaka nipande lakini sikuwa tayari kwa hilo nilikaa chini na kumpa wakati mgumu wa kuniinua.
"Hata usipopanda kikubwa uko nje ya eneo la hatari dada yangu."
"Kwanini msiniache nikaimalize hasira yangu lakini?" Niliendelea kupiga kelele ambazo zilimfikia mzee Mbogo ambaye alimpa ishara Rachel aniruhusu niende.
"Haya twende babu anakuita." Rachel aliniambia lakini sikuweza kumjibu zaidi ya kuinuka na kuongoza walikokuwa, nilipofika tu mzee Mbogo alinimwagia dawa iliyokuwa kwenye kibuyu ambacho alikuwa amekibeba kisha alinipa ishara ya kuingia naniliu ya dimba lakini akinitaka nipite alipokuwa ameketi mzee Nyaswa na mimi nilifanya hivyo.
"Ruksa mjukuu wangu kufanya chochote kwa watu hawa lakini hakikisha kuwa huwagusi miili yao unachotakiwa kukifanya ni kuitumia silaha yako ya mdomo tu." Mzee Nyaswa aliniambia.
"Ni...ni...mekuelewa babu." Nilimjibu hasira zikiwa zimelikaba koo langu kiasi cha kushindwa kupumua vizuri na wakati najaribu kuanza kufanya kile ambacho nilitaka kukifanya ghafla nguvu ziliniisha na kujikuta nikienda chini na kupoteza fahamu na sikuweza kujua ni nini kiliendelea pale mpaka narejewa na fahamu nilikuwa nimezungukwa na sura nyingi ambazo zilikuwa kama zinanizomea hivi kwani nilikuwa sioni viwiliwili vyao zaidi ya vichwa vyao tu na sehemu za vifuani tu, hali hii ilinitisha sana na kujiuliza niko wapi mbona kuna watu wa ajabu kiasi hiki. Mara niliisikia sauti ya mama kwa mbali ikiniita.
"Mwanangu umezinduka?" Sauti hiyo ilinifanya nigeuze shingo yangu na ndipo nilipoweza kuwaona wote vizuri, kumbe nilikuwa siwaoni vizuri kwa sababu nililala chali.
"Ndiyo mama kwani hapa ni wapi?" Nilimuuliza.
"Usijali mwanangu utakuwa sawa muda si mrefu." Mama alinijibu akiuvuta upande wa kitenge na kujifuta machozi.
"Unajisikiaje Christina?" Daktari alifika na kuniuliza.
"Niko vizuri tu, wewe ni daktari?" Nilimuuliza.
"Ndiyo, naitwa Daktari Maneno ndiye niliyeupigania uhai wako Tina." Alinijibu Daktari Manéno.
"Kwa hiyo hapa ni Hospitali?" Sikuishiwa maswali.
"Dada Tina uko Hospitali ya Rufaa Mbeya hali yako ilikuwa mbaya sana tukachukua jukumu la kukukimbiza hapa." Rachel alinijibu baada ya kuona nimembana sana Daktari ambaye aliondoka wakati Rachel akinijibu swali langu. Wakati mdogo wangu Rachel akinieleza kilichotokea mara macho yangu yalitua kwa mtu ambaye sikutarajia kuiona sura yake mbele ya macho yangu.
" Na huyu anafanya nini hapa Rachel?" Nilimuuliza Rachel baada ya kumuona Jofrey kando ya kitanda.
"Tulia kwanza mwanangu tutakueleza kila kitu hali yako ikiwa sawa." Mama alinijibu.
"Hapana naomba aondoke mara moja kabla sijamfanyia kitu kibaya."
"Kijana naomba uondoke kwa usalama wa mgonjwa kama kuna jambo unalotaka kumweleza subiri mpaka awe sawa." Alitokea Daktari wa zamu akiwa na dawa kwenye kitrei kidogo na kumtaka Jofrey atoke nje.
"Sawa kaka." Jofrey alimjibu na kutoka nje.
"Mama ilikuwaje mkamruhusu muuaji kuingia humu? Au mlitaka aniue?" Niliwauliza.
"Hapana siyo hivyo mwanangu naomba umsikilize Daktari kwanza kisha wao walitoka nje na kuniacha na Daktari ambaye alifanya kazi yake na akiwa anataka kutoka nilimzuia kwa swali.
" Samahani Daktari nasumbuliwa na nini tafadhali usinifiche." Aligeuka na kunifuata pale kitandani.
"Tina juzi wakati unaletwa hapa hali yako ilikuwa mbaya sana kwani uliishiwa maji pamoja na damu hivyo kwa jitihada zetu tulifanikisha hilo, hakuna tatizo jingine ulilokuwa nalo." Alinijibu na kutoka.
"Kwanini niishiwe damu na maji wakati nilikuwa vizuri kuna nini kilitokea?" Ni swali ambalo nilijiuliza na wakati huo wakina mama waliingia.
"Rachel naomba kujua kwanini niko hapa na nini kiliendelea pale na mwisho nieleze Jofrey kafikaje hapa?"
"Dada Tina kwanza hongera kwa kurudi kwenye hali yako ya kawaida kulingana na maelezo ya Daktari. Kuhusu hayo mengine naomba nikwambie kuwa kitendo chako cha kuingia pale uwanjani uliharibu utaratibu au ulivunja masharti kiasi cha kuwafanya maadui kupata nguvu na kupelekea kujibu mashambulizi.... " Wakati Rachel akijibu swali langu nilimkatisha.
" Usiniambie kwamba wametoroka kwa mara nyingine tena?"
" Hujakosea katika hilo ni kweli kabisa wamefanikiwa kututoroka unajua nini dada wakati ukipiga zile kelele ulisababisha kazi kuwa ngumu na ndiyo maana wazee waliamua kukuruhusu uingie dimbani japo walijua ni hatari cha kushukuru Mungu hakuna aliyedhurika miongoni mwetu ila kwa upande wao hali ni mbaya japo wamekimbia na ndiyo maana wamemtuma mtoto wao aje kutuomba msamaha ili wazazi wake warudi kwenye hali yao ya kawaida." Rachel alitoa maelezo ambayo yalianza kunitoa machozi.
" Unafanya nini sasa hebu nyamaza." Rachel alinituliza.
" Kwa hiyo wakina babu wamenichukia kiasi cha kutokuja kuniona?"
" Hapana siyo hivyo mwanangu wako huko porini na baba yako wakihangaika juu yako." Mama alinijibu. Nilimtazama Rachel kisha mama baada ya hapo niligeukia ukutani na kutulia kimya nikiendelea kutafakari hawa viumbe wakoje kiasi cha kuukwepa mtego kila wanapodhibitiwa. Nikiwa nimegeukia ukutani ambako sikutaka kuziona sura za wakina mama mara ule ukuta ukawa kama vile umepasuka na kunifanya kuweza kuona kila kinachoendelea nje, nikamuona mama mkwe akiniita kwa ishara huku Bi Kiziwa akiwa kwenye machela iliyobebwa na Jofrey pamoja na wifi.
"Umechanganyikiwa? Unamwita nani na ili iweje?" Niliongea kwa sauti ambayo iliwashtua wakina mama.
"Dada Tina kuna nini?" Rachel aliniuliza swali na kabla sijamjibu aliweza kuhisi kitu kupitia pale kwenye ule ukuta hivyo alitoka bila kumuaga mama.
"Kuna nini mwanangu?" Mama aliniuliza.
"Hakuna kitu mama, ila naomba kama unanipenda mwanao nitoroshe hapa Hospitali." Nilimjibu.
"Nikutoroshe tena? Kwanini wakati Daktari hajaturuhusu?"
"Mama hapa si salama maadui wameshafika na wameanza kunishawishi niwafuate. Mama kama huwezi kufanya nilivyokuambia naondoka mwenyewe." Ilibidi nimwambie kwa sauti ya juu ili ajue sitanii katika hilo.
"Basi nisubiri mwanangu nikakodi gari ambalo tutalitumia sawa?" Aliniuliza lakini sikumjibu maana niliona kama ananipotezea muda tu, hivyo hakutaka kusubiri alitoka nje na kuniacha mle ndani.
"Enhh Tina....." Sikutaka kuisubiri hii sauti imalizie sentensi yake nilirusha ngumi ambayo sikumpata baada ya kukwepa.
"Mwanangu umechanganyikiwa mpaka utake kunipiga baba yako?" Kumbe alikuwa baba kaingia mimi nilijua washenzi wale wametumia upenyo wa waangalizi wangu kuondoka.
"Samahani baba yangu wala sijachanganyikiwa bali wale wachawi wameshafika hapa kuifuata roho yangu na ndiyo maana huoni mtu humu ndani." Nilimjibu baba.
"Pole mwanangu na ndiyo maana niko hapa huko nje babu zako wako kuweka mambo sawa mara baada ya Rachel kutupigia simu."
"Sawa baba lakini pamoja na hayo siwezi kulala hapa Hospitali naomba mfanye kila mnaloweza kuhakikisha naondoka na iwapo kama mtashindwa kufanya hili nitalifanya mwenyewe."
"Naomba uwe na subira kwanza wacha waje tuwaeleze hili kisha tutajua la kufanya lakini tusifanye mambo kienyeji huoni itakuwa hatari zaidi ukizingatia sisi hatuna chochote cha kutulinda mwanangu?" Baba aliongea kwa hisia sana kiasi cha kutokwa machozi.
"Nina imani litakwisha tu hili na maisha mengine yataendelea." Baba aliongeza.
"Ni kweli baba lakini si rahisi kama unavyodhani ilhali wakina Jofrey wanakuja mpaka humu wodini kwa kisingizio cha kuja kuniomba msamaha kumbe ana lake jambo."
"Alikuwepo hapa Jofrey?" Baba aliuliza kwa mshangao.
"Ndiyo alifika hapa akiwa kaongozana na yule mjumbe wa kitongoji kwa lengo la kuja kuomba suluhu." Mama alimjibu baba baada ya kuingia na kukuta nikimpa maelezo haya.
"Kuomba suluhu gani tena mama Christina? Huoni hii ni hatari?" Baba alifoka.
"Baba Christina unafikiri ningefanya nini wakati mdogo wake alisema wasubiri mpaka aamke ndipo hili lijadiliwe." Mama alijitetea.
"Aaaggh... Okay ila wakati mwingine unatakiwa kuwa makini mke wangu." Aliongea akiwa kauma meno na kuondoka.
"Sawa mume wangu sasa safari ya wapi tena?" Mama alimuuliza baada ya kuona anaufuata mlango ili aondoke bila shaka alitaka kuwa mbali kidogo na sisi anazijua hasira zake huwa zikimpanda tu maamuzi yake huwa si mazuri.
UNAFIKIRI NINI KINAKWENDA KUTOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI.
#SULTANUWEZO