MUUAJI MWENYE BARAKOA - 40
sultanuwezotz.blogspot.com
Catherine alimuuliza mzee Mahmoud huku akiyakagua mazingira wanayopita kwani yalimpa wasiwasi kutokana na muonekano wake wa uswahilini tofauti na matarajio yake ya kuwa katikati ya jiji.
"Mmh lakini nimepata wazo jipya ambalo nahisi litakuwa zuri binti yangu, unaonaje nikikupeleka kwa huko kisha mimi ndiyo nilete mzigo?"
" Mimi naona kama unanichanganya tu mzee wangu, naomba nipate hifadhi sala tu na si vinginevyo." Catherine alimjibu akiminyaminya vidole vyake vya mikononi.
" Ondoa shaka muda si mrefu tutakuwa hapo." Mzee Mahmoud alimjibu akiendelea kunyonga usukani wake. Na baada ya muda waliwasili kwenye mtaa mmoja uliochangamka sana lakini ukionekana kukaliwa zaidi na watu wa hali ya chini na hii ilikuwa ni kutokana na watoto waliokuwa wakipishana barabara japo walikuwa na furaha sana lakini walikuwa wachafu huku wakiwa uchi wanacheza. Alitamani kuuliza juu ya kile anachokiona lakini akaona auzibe tu mdomo wake na kutulia.
"Naomba ushuke binti yangu tumefika." Mzee Mahmoud alimwambia Catherine ambaye alionekana mwenye mawazo kiasi huku akilisimamisha gari lake vizuri. "Sawa mzee." Catherine alimjibu.
Walishuka na kuelekea kwenye kiuchochoro kilichopita kwenye nyumba moja ambayo ni chakavu ikiwa na bomba la maji nje yake, walipita hapo na kutokea mtaa wa nyuma huko waliingia kwenye jumba moja ambalo kwa nje lilionekana ni chakavu lakini ndani yake kulikuwa na shughuli nyingi na za ajabu ambazo Catherine hakutarajia kukutana nazo.
"Kwanini umenileta humu mzee wangu?" Catherine alimuuliza wakiwa wanakatisha katikati ya watu waliokuwa wakiburudika kwa vinywaji na starehe nyingine.
"Usijali binti yangu humu ni sehemu salama japo kuna shughuli kama unazoziona na ninafikiri hata hao wanaokuwinda itakuwa ni ngumu kujua kama uko kwenye jumba kama hili ambalo ni changanyikeni masaa ishirini na nne." Mzee Mahmoud alimjibu akigonga moja ya mlango ambao umeandikwa 'MANAGEMENT OFFICE' na kumfanya Catherine kuendelea kuwa na maswali kichwani mwake.
" Mbona mazingira ya humu ndani yanaonesha hili ni Danguro?" Catherine alimuuliza.
" Ndiyo ni Danguro lakini pia huwa tunahifadhi watu ambao wanawindwa na vyombo vya Kiusalama na huwa tunafanya hivi kutokana na usalama wa hapa."
"Una maana gani?" Catherine alimuuliza na wakati huo mlango ulifunguliwa na mrembo mmoja aliyejitokeza akiwa na bikini tu huku sehemu ya juu kavaa kit-shirt cheusi kilichokatwa usawa wa maziwa na kuliacha eneo lote la tumbo wazi na mkononi akiwa na sigara.
" Aaahh Bosi mwenyewe karibu."
"Asante Herieth, vipi big mama yupo?" Mzee Mahmoud alimuuliza.
"Yupo ofisini kwake, vipi ni mali mpya nini?" Alimjibu na kuuliza huku akimpulizia moshi usoni Catherine.
"Umeanza vituko vyako hebu tuache kwanza." Mzee Mahmoud alimjibu akimpa ishara Catherine amfuate nyuma. Mazingira yale yalianza kumtia hofu Catherine kiasi cha kutamani kuondoka lakini pia alitamani kulijua zaidi hili jengo na shughuli zake, kitu kilichomuuma zaidi ni kuiacha silaha yake kwenye gari kutokana na ukubwa wake. Wakiwa wanalifuata korido linaloelekea kwenye mlango wa kioo uliokuwa mbele yao Catherine aligeuka nyuma kumtazama yule msichana aliyewafungulia mlango na kumuona akiwa anaongea na simu hiyo kwake ni ishara nzuri au mbaya. Alichokuwa akijiuliza ni kwa namna gani jengo hili liwe chakavu kwa nje lakini kwa ndani linapendeza sana kwa namna lilivyotengenezwa.
"Catherine mbona macho hayatulii? Una hofu na mazingira ya humu ndani?" Mzee Mahmoud alimuuliza akibofya swichi ya kengele.
"Wala siyo hofu bali ni ugeni tu si unajua sijawahi kuingia mazingira kama haya." Catherine alimtoa hofu mzee Mahmoud.
"Piteni ndani tafadhali." Aliwakaribisha ndani mama mmoja ambaye alikuwa ndani dela moja matata huku mkononi akiwa na sigara na macho yake akiwa kayaficha kwenye miwani mikubwa ya rangi ya pink.
"Asante mama la mama." Mzee Mahmoud aliitikia wakiwa wanapita mlangoni.
"Mbona unapotea hivyo mzee wangu? Au wifi yangu kaanza kukufungia ndani nini?" Mama huyo alimtania.
"Anawezaje kwa mfano, sema kutingwa tu ndiyo kunanifanya kuwa bize na si vinginevyo mdogo wangu." Mzee Mahmoud alimjibu.
"Yanaukweli maneno yako kaka?" Alizidi kumuuliza.
" Hebu tuachane na maneno yako yasiyo na mwisho na badala yake tujadili lililonileta."
" Karibu, uwanja ni wako."
"Pembeni yangu anaitwa Catherine ni binti yangu niliyekutana naye njiani nikitoka Dosso na kikubwa ni kwamba hana ndugu yeyote hapa mjini wala nini hivyo aliniomba nimtafutie sehemu ya kujiegesha wakati anafanya harakati zake." Maelezo ya mzee Mahmoud yalimfanya Catherine amkate jicho la hasira mpaka yule mwanamke aliona kile kitu.
" Uyasemayo ni ya kweli mzee isije kuwa kama wale mabinti wawili ambao uliniletea kwa mara ya mwisho ulipoondoka tu walianza usumbufu mpaka nilijuta kufanya kazi na wewe lakini sikutaka kukuambia niliamini ni utoto wao tu watatulia lakini wapi unajua nini kilifuata?"
" Ndiyo uniambie wewe."
"Walitoroka na mauzo yangu ya siku hiyo na mpaka leo sijawahi kuwaona tena hivyo nina hofu hata kwa huyu."
Aliongea huku macho yakiwa kwa Catherine.
"Kuhusu mimi ondoa wasiwasi dada yangu na ninaamini utafurahi mwenyewe ndani ya muda mfupi." Catherine aliona amuondoe hofu mama huyo anayeonekana ndiye mmiliki wa Biashara zinazofanywa mle ndani.
"Kweli binti?"
"Niamini."
"Kaka imekwisha hii labda kama kuna jingine?"
"Hakuna kingine zaidi ya mambo yetu tu."
"Usijali mpaka kufikia mchana kesho nitakuwa nimerekebisha." Mama huyo alimjibu akiupuliza moshi juu.
"Catherine kama tulivyoongea hapa ndiyo nyumbani kwako kwa sasa na unayemuona mbele yako ndiye mama yako mlezi anaitwa Carolyn Othello almaarufu kwa jina la...."
"Mama Burudani" Alidakia na kujibu.
"Okay nafurahi kukufahamu dada yangu na mimi nikuahidi kukupa ushirikiano wakati wote nitakaokuwa hapa." Catherine alimjibu akiwa kamkazia macho mzee Mahmoud.
"Usijali Catherine."
"Basi mimi niwaache ili niwaishe bidhaa yangu sokoni, Catherine kale kamzigo nitakahifadhi nyumbani." Akiinuka alimtaarifu Catherine juu ya silaha yake naye hakutaka maneno mengi aliitikia kwa kichwa tu.
"Catherine nisubiri humu humu wacha nimtoe kaka kwanza." Mama Burudani alimwambia Catherine akitoka na mzee Mahmoud.
"Sawa dada." Catherine alimjibu.
Walitoka na kuufunga mlango huku ndani Catherine aliinuka na kuanza kuikagua ile ofisini kuanzia pale mezani kisha aliinama kwenye droo za meza ambazo hakufanikiwa kwani zilikuwa zimefungwa kwa ufunguo. Ikabidi arudi na kukaa kusubiri utaratibu wa mwenyeji wake ambaye dakika sifuri aliingia akiwa kaongozana na yule msichana aliyempulizia moshi wakiwa wanaingia aitwaye Herieth.
"Catherine karibu sana na jisikie nyumbani." Mama Burudani aliongea akikaa kwenye kiti chake cha kuzungumza.
"Asante sana."
"Pembeni yako ni mfanyakazi mwenzako anaitwa Herieth na kwa lugha nyingine huyu ni Msaidizi wangu mimi hivyo basi yeye ndiyo atakupa utaratibu mzima wa nini cha kufanya ndani ya Kasri letu la Burudani."
"Okay sawa lakini kama hamtojali naomba kuuliza swali."
"Uko huru Cath uliza tu."
"Ni majukumu gani ambayo nitayafanya humu ndani?" Swali lake liliwafanya wakina Herieth kucheka sana tena huku wakigonga mikono.
"Usijali kwa kuwa umechoka naomba nikupeleke kwenye chumba chako ukaoge kwanza wakati Afisa Afya akikuandalia mavazi yako ambayo utayatumia maana hayo naona yamechafuka sana." Herieth alimgeukia na kumwambia.
"Haya yangu nimemaliza mnaweza kwenda." Mama Burudani aliwaaga. Walitoka na moja kwa moja walitoka nje ya vile vyumba vya utawala na kuelekea kwenye korido la pili ambalo liliwapeleka mpaka kwenye vyumba vilivyokuwa vimepangana kama vile vya nyumba za kulala wageni na baada ya kukifikia chumba na 107 Herieth aliufungua mlango na kumkaribisha.
"Karibu dada yangu hiki ndiyo kitakuwa chumba chako kwa muda wote wa maisha yako hapa BURUDANI HOUSE."
"Okay asante Herieth." Catherine alimjibu akimkadiria kuanzia juu mpaka chini.
"Na hivi vitu vyote uvionavyo humu ndani ni vya kwako."
"Herieth hebu keti mara moja." Catherine alimwambia Herieth aliyekuwa akifungua mlango wa kabati la nguo.
"Niambie."
"Kwa hiyo humu ndani kazi kubwa ni ipi maana mzee Mahmoud aliniambia ananileta kwa ndugu yake kukaa sasa naona mambo ni tofauti kabisa." Catherine alimuuliza.
"Acha kuzuga Catherine mbona nikikuangalia haufanani na uongo au unataka nijichanganye ili Big mama aniadhibu?" Herieth aliona kama anategwa vile hivyo aliamua kutoka na kumuacha Catherine peke yake.
" Kwa wao kwa akili zao tatu wanajua mimi nina shida na hela? Kweli usimdharau usiyemjua." Aliinuka na kulifuata dirisha akalichunguza kwa muda kisha akarudi na kukiendea kioo kilichokuwa kwenye kabati la nguo na kujitazama.
"Catherine umepatwa na nini mbona mchafu kiasi hicho? Ndiyo maana wamenichukulia poa eee?" Alijiuliza akizishikashika nywele zake zilizokuwa kama za kichaa vile. Hakuona sababu ya kuendelea kutulia pale akaufungua mlango wa bafuni. Alitumia kama dakika za kutosha kuoga na baada ya kumaliza alitoka na kukaa mbele ya kioo na kuanza kuulainisha mwili wake kwa mafuta yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili yake na ukizingatia ana muda mrefu hajafanya hivyo aliona ni muda muafaka wa kufanya hivyo. Aliporidhika alihamia kwenye kabati lenye nguo za kila aina lakini yeye alichagua 'tracksuit' ya rangi nyekundu na kuivaa kisha akachukua na kofia aina 'cap' nyeusi akaitupia kichwani. Alipojiangalia kwenye kioo yeye mwenyewe alijicheka.
"Muonekano mpya eee?" Alijiuliza akichukua miwani na kuivaa kisha akavaa raba nyeupe za Nike na kutoka nje.
"Madam Herieth anakuita ukumbini." Alikuja msichana mmoja ambaye kwa muonekano tu alionekana bado mdogo sana kiumri.
"Kuna nini?" Alimuuliza.
"Sijui kuna nini yeye kaniambia hivyo." Namna alivyomjibu kulimpa mashaka Catherine kwa haraka sana aliinua kichwa na kutazama juu ndipo alipoona kuna kamera za ulinzi.
"Mmh ina maana walikuwa wananifuatilia." Aliongea kimoyo moyo baada ya kuona zile kamera na ili kuonesha hajaona chochote aliongeza mwendo na kumfikia yule msichana ambaye alikuwa amemuacha kidogo.
"Naitwa Catherine mwenzangu unaitwa nani?" Alimuuliza.
"Mimi naitwa Bettina ila maarufu kwa jina la 'Cute Girl'"
"Nimefurahi kukufahamu Cute Girl." Aliongea wakiwa wanaingia ukumbini ambamo alishangaa kukutana na wasichana wasiopungua arobaini wakiwa kwenye vivazi vya ajabu ajabu kama vya Herieth kidogo huyu Bettina alijisitiri kiheshima japo kilikuwa ni kigauni kilichobana sana mwili wake lakini ilikuwa bora yake.
"Ndugu zangu wana wa mama Burudani mbele yenu kakaa dada Catherine akiwa ni mgeni wetu."
"Tunamkaribisha ndani ya Burudani." Msichana mmoja aliyekuwa akivuta sigara huku akicheza cheza muziki aliongea kwa niaba ya wenzake. Catherine alimtazama kwa muda kisha aligeuka macho kwa wengine wote na baadaye kwa kiongozi wao Herieth aliyekuwa karibu yake.
" Hivyo ndugu zangu tumpe ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kumuonesha mazingira yote muhimu humu ndani na namna ya kulilinda soko lake." Herieth aliendelea kutoa maelekezo.
"Sijui una lolote mgeni wetu?"
"Hapana sina lolote lile zaidi ya kuwashukuru kwa ukarimu wenu zaidi mfikishie shukrani zangu mama Burudani mwambie nimefika kutoka ni hatua nyingine."
"Tunafurahi kusikia hivyo dada yetu na sisi tunaahidi kutoa ushirikiano asilimia mia moja..." Wakati Herieth akiendelea na kuongea aliingia mvulana mmoja chotara wa Kiarabu na kumfuata Herieth moja kwa moja na kumnong'oneza kitu sikioni. Baada ya kumaliza kuongea naye alitoka huku macho yake kwa Catherine mkono wa kulia ukizishikashika ndevu zake zilizokifunika kidevu chake chote. "Usishangae dada huyo kijana ni mtoto wa Tajiri mmoja hapa mtaani kwetu anaitwa Taraj, huwa anakuja na kumpa kazi Herieth ya kumtafutia mnofu laini."
"Mnofu laini?" Catherine aliuliza kama haelewi kinachofanyika mle ndani.
"Mbona unauliza kwamba hujui dada?" Msichana huyo alimuuliza Catherine.
JE MAMA BURUDANI KAPATA AU KAPATIKANA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KINACHOKWENDA KUTOKEA NDANI YA JENGO HILI LA BURUDANI.
#SULTANUWEZO