IMETOSHA MAMA MKWE - 37 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE - 37

sultanuwezotz.blogspot.com 


Nilitafakari kwa muda jina la mtu huyu ambaye nakumbuka majuma kadhaa ni kweli nilisafiri naye na kuketi kwenye siti moja ndani ya Kibiki Express kutoka Iringa mpaka mji wa Makambako ambapo yeye alishuka na mimi kuendelea na safari ya jijini Mbeya. Na baada ya kuvuta kumbukumbu vizuri ndipo nilipolikumbuka jina lake hivyo nikamjibu.

"Nimekukumbuka tayari.."

"Wala hujanikumbuka hata kidogo naona unavyokuna kichwa kulitafuta jina langu."

"Wala wewe si ni Salehe Mabena au siyo wewe?" Nilimjibu.

"Ndiyo mwenyewe japo umeumiza kichwa kiasi cha kutokwa jasho mpaka kwenye meno."

"Hebu acha utani wako Salehe, vipi lakini habari ya siku?" Nilimsabahi. 

"Nashukuru Mungu naendelea vizuri na kama bahati vile nilibahatika kupata kazi ndani ya kituo cha redio cha 'Ice fm' kama Afisa masoko."

"Aisee hongera sana bwana Mabena na Mungu akuongoze katika kutimiza ndoto zako katika njia iliyo sahihi na si vinginevyo." 

"Ameen na kwa muongozo wake aliye juu nitafanya hivyo." Alinijibu. 

"Salehe tafadhali naomba nikutafute baadaye kidogo niko eneo ambalo si rafiki." Niliona nikatishe kwanza maana muda ulienda kidogo. 

"Wala usijali wacha na mimi niingie studio kushughulikia tatizo moja hivi." 

"Pamoja." Nilimjibu na kuinuka kisha nilimfuata kijana aliyekuwa akiniandalia chips za mwanangu na baada ya kunikabidhi nilimlipa kisha nikaondoka bila kujali mezani nimebakiza nini nilitoka na kuingia ndani jengo la hospitali ambapo niliwakuta wakina mama wakiwa ndani na si pale nilipowaacha. 

"Christina mwanangu mbona umechelewa hivyo?" Mama hakusubiri alinianzia hapo hapo. 

"Nilikuta kila kitu kimekwisha hivyo nikamuomba aniandalie na ndiyo maana nimechukua muda mrefu hivyo." Nilimjibu. 

"Mhh haya mkabidhi mhitaji kisha tutoke tutarejea baadaye." Mama aliongea hayo na mimi nikafanya vivyo hivyo na kisha tukatoka na kumuacha mwanangu akiwa na babu yake. 

"Tunaelekea wapi?" Nilimuuliza mama tukiwa tunatoka nje ya geti. 

"Tunaelekea kwanza sokoni kuangalia kunaendeleaje maana vijana wa kazi si wa kuwapa asilimia mia moja peke yao kisha tutaelekea nyumbani." Alinijibu. 

"Okay sawa." Nilimjibu pia kisha tuliingia ndani ya taxi na kuondoka. 

"Mtarajiwa wako anasemaje?" Mama aliniuliza swali ambalo nilijua kuwa lilikuwa ni tageti yake kwangu. 

"Mama bwana, nitakueleza kila kitu tukifika nyumbani." Nilimjibu. 

"Haya japo mwenzako koo linawasha sana bila shaka linahitaji ubuyu tena ule wa Zanzibar." 

"Liache liendelee kuwasha tu litatulia lenyewe." Nilimjibu wakati dereva akisimamisha gari kando ya lango la kuingia sokoni. 

Nilimlipa ujira wake kisha tukashuka na kuingia sokoni ambako tuliwakuta vijana wa kazi wakiendeleza shughuli ya kuuza mazao na kilichotufurahisha zaidi ni baada ya kukuta mzigo umepungua kiasi cha mama kuchukua simu yake na kumpigia dalali wake aishie Isimani kumuangalia mzigo mwingine. Baada ya kuwaachia maagizo tulitoka hapo na kuelekea nyumbani na kwa kuwa nyumbani siyo mbali sana kutoka mahali hapo hatukuona sababu ya kuchukua Bajaj wala Taxi tukatembea kwa miguu mpaka pale tulipofika nyumbani. 

"Kwa hiyo hata ndani hukuingia?" Mama aliuliza baada ya kuuona mkoba wangu karibu na mlango. 

"Ningewezaje kuingia baada ya kukutana na baba akiwa anatoka nikaona niongozane naye kwa kuwa alikuwa na pikipiki." Nilimjibu. 

"Aisee pole sana lakini ndiyo ukubwa huo unafikiri kuitwa mama ni kung'arisha kope, sura na mwili? Ni malezi kwa familia." 

"Nashukuru mama na ndiyo maana na mimi najaribu kutembea kwenye hatua zako." Nilimjibu mama nikiupeleka mkoba chumbani kwangu. 

"Ndiyo hivyo, sasa usihamie huko nakufahamu fanya urudi hapa unipe ubuyu kabla baba yako hajarejea." 

"Nimekusikia." Nilimjibu na kuingia chumbani kwangu ambako niliona nioge kabisa kabla ya lolote lile na baada ya kuoga na kubadili mavazi yangu na kisha kutoka. Nilimkuta mama akiwa katulia akiwa kaandaa soda pale mezani huku yeye akiendelea kupoza koo lake huku yangu ikiwa inanisubiri. 

"Fungua mwenyewe." 

"Si ungenifungulia kabisa mama nawe." 

"Nikununulie na kukufungulia nikufungulie? Thubutuu kama huwezi iache hapo hapo." Alinijibu akiendelea kunywa yake. Hivyo niliifungua na kisha nikaikata kwanza kisha nikakaa sawa kuliandaa koo tayari kwa kumpa mkasa ambao nilikutana nao huko Mbeya. 

"Mama yangu." Nilimwita. 

"Abee mwanangu." Aliitika. 

"Najua una hamu kubwa kusikia safari yangu ilikuwaje." 

"Kabisa mwanangu." Aliitikia. 

"Baada ya kuwasili jijini Mbeya nilikutana na mpenzi wangu Jofrey ambaye una hamu ya kumfahamu, alinipokea na kisha tulichukua Bajaj na kuondoka pale stendi ya Nanenane japo sikujua tunaelekea wapi. Unajua nini kilitokea?" Nilimuuliza. 

"Nitajulia wapi wakati mimi nilibaki huku." Alinijibu akitingisha mabega. 

"Wakati tunataka kuondoka kuna kitu kiliingia kwenye simu yake baada hapo nilimuona kabadilika sura hivyo hata tukiwa ndani ya Bajaj alikuwa ni mtu mwenye vihasira hasira. Hatukuweza kufika popote kwani ilifikia hatua akakwaruzana na dereva Bajaj kiasi cha kushuka sehemu ambayo hatukuitarajia."

"Kisa nini?" Mama aliuliza. 

"Hata mimi sikujua lakini baada ya kuona bado haeleweki nilimuacha hapo hapo nikaondoka na kuingia kwenye Bajaj ambapo sikujua naelekea wapi." 

"Weee mtoto mbona una majanga hivyo sasa ikawaje?" Aliniuliza. 

"Tulipofika kituo cha mbele alitokea bibi mmoja ambaye alisimamisha Bajaj na kisha kuingia na baada ya kuingia alikuta tukiongelea sakata la mpenzi wangu na kisha kuingilia kati na kunipa pole na kuniambia hata yeye ni mtu wa mkoa wa Njombe hivyo kwenye hakuna haja ya kwenda kulala gesti nitafikia kwake na nitakaa hapo mpaka nitakapomaliza mishe zangu ni kweli tulikwenda mpaka kwake maeneo ya Magege maana sikuona sababu ya kwenda kulala gesti wakati mwenyeji wangu yupo lakini wakati tunashuka ndipo nilipoanza kupata hofu."

"Kwanini tena?" Aliniuliza. 

"Ni baada ya kuiona nyumba ikiwa mjini lakini imechoka haina umeme wala watu ndani yake na kama vile hofu yangu ilipata jibu kwani tukiwa ndani bibi yule aitwaye Bi Kiziwa alinipa maziwa ambayo nilikunywa hivyo hivyo mpaka pale nilipokutana na mzee mmoja ambaye alitokea nikiwa nakoleza jiko la mkaa na kuniambia nimfuate, mwanzo sikumuelewa lakini baadaye nilimuelewa baada ya kuniambia kuwa Bi Kiziwa ni mchawi sana kwani pale anapoishi hana hata mtoto wa kusingizia alishawatafuna wote hivyo huvizia wageni ambao akiwalaza tu ndani ya nyumba yake lazima akumalize.

Hivyo mzee huyu aitwaye Mzee Mbogo ambaye kazi yake ni kupambana na watu kama Bi Kiziwa kwa watu wasio na hatia japo tulitembea masaa kadhaa usiku tukipita katikati ya msitu ulioko eneo la Ilolo eneo maarufu kwa kilimo cha mboga mboga.... " Niliendelea kumueleza mama kitu ambacho hakukitarajia hata kidogo maana nilianza kuyaona machozi kwenye macho yake.

" Pole sana mwanangu uliponaje mpaka sasa uko hai na kwanini hukutuambia?" Aliniuliza akiyafuta machozi yake.

" Mama sikuona sababu ya kuwaeleza haya niliamua kukaa kimya huku nikishirikiana na mzee Mbogo pamoja na mjukuu wake Rachel. Huyu Rachel ndiye huyu ambaye nilikabidhiwa kwake na mzee Mbogo mpaka pale ambapo nilifanikiwa kupata nafasi chuoni St. Aggrey. Huyo Rachel ndiye aliyenisindikiza mpaka Makambako na ndiye huyu huyu aliyeninunulia hii simu na ndiye huyu huyu aliyeninunulia mpaka nguo niseme nini juu yao hawa watu mama yangu." Niliishia hapo baada ya kushindwa kuvumilia kwani machozi yalinizidia mpaka sauti ilianza kukata.

" Pole sana mwanangu, wazazi wako hatukuwa tukijua kitu kama hicho kumbe ulipitia magumu hivyo? "

" Magumu gani hayo tena?" Baba alifika na kuuliza swali hilo ambalo lilitushtua kwani hatukutarajia.

"Baba Christina, huyu mtoto ana majanga sana yaani kwa aliyokutana nayo acha tu nitakusimulia baadaye." Mama alimjibu.

"Mwanangu kuna nini?" Baba aliniuliza baada ya kumsikia mama.

"Ni historia ndefu baba yangu nafikiri kama alivyosema mama atakusimulia maana nimemwambia kila kitu." Nilimjibu kwa kifupi.

"Haya mwanangu nimekuelewa kikubwa yasiwe ya majonzi tu." Aliongea hayo huku akiingia chumbani.

"Mama kingine kilichonifanya kuwa na hofu zaidi ni pale ambapo yule Bi Kiziwa alipokuwa akinitokea mpaka nilipozimia na kubebwa na familia ya mzee Mbogo na kunipeleka mpaka kwa mganga mmoja pale Inyala ndipo nilipopona na mwisho kabisa ni kuiota ndoto ambayo niliiona ikimhusisha mpenzi wangu na Bi Kiziwa hofu yangu kuhusu hawa watu sijui wana undugu? Maana hata Jofrey sijawahi kumuuliza, kifupi mama yangu ni hayo tu." Nilimsimulia mama huku machozi yakiendelea kunitoka nilisimama na kukimbilia chumbani na kumuacha mama pale sebuleni.

Nilipoingia tu chumbani simu yangu iliita na nilipoiangalia alikuwa ni dada Noela nikajua bado ana hamu ya kutaka kuongea nami.

Nilijifuta macho nikakohoa kidogo kuweka koo vizuri kisha nikaipokea.

"Enhh niambie mdada mwenyewe."

"Hivi unajua mimi kwa sasa naishi wapi?" Aliniuliza dada Noela.

"Nitajulia wapi wakati wewe mwenyewe hujaniambia?" Nilimuuliza.

"Mdogo wangu mara baada ya kuondoka kwa mama Fabiana pale Makambako nikiwa nina mtaji wangu kiasi nilikuja kuanza maisha yangu mapya mjini Njombe eneo la Ramadhan hapa ambapo nilianza shughuli ya kilimo cha bustani pamoja na ufugaji wa kuku na miaka miwili baadaye niliungana na mpenzi wangu wa muda mrefu ambaye si mwingine bali ni Kennedy... "

" Wee acha utani Kennedy alikuwa mpenzi wako?" Nilimkatisha.

" Huwezi amini lakini ukweli ndiyo huu mapenzi yetu tuliyafanya siri kiasi kwamba wewe mwenyewe hukuweza kujua na kama huamini huyu hapa ongea naye."

"Tina Tina Habari ya siku?" Kennedy alianza kwa utani.

"Jamani kweli mapenzi shikamoo yaani tumeishi pamoja pale Makambako kumbe mlikuwa mnawezana?" Nilimtania.

"Kila kitu ni Sara ndugu ni kweli kabisa tulikuwa wapenzi kwa muda mrefu na kwa sasa tumekuwa familia moja tukiwa tumebahatika kuwa watoto wawili wote wakiwa wa kike." Kennedy alinijibu.

"Sasa wewe Kenny nitakuitaje?" Nilimuuliza.

"Vyovyote vile ukiniita shemeji sawa ukiniita kaka sawa pia karibu sana Tina hapa Ramadhan uje uone matunda ya mama Fabiana." Alinikaribisha.

"Nitakaribia tu shemeji yangu nilikuwa Mbeya nimerudi hivi leo tu hapa Iringa na kama siku kadhaa nyuma niliongea na Fabiana ambaye yuko Zanzibar pamoja na mama yake ambaye anamuuguza kwa kujifungua."

"Yes hata sisi alituambia na hata hivyo dada yako anajiandaa kuelekea huko baada ya kuuza hizi nyanya zilizochumwa kwanza si unajua tena ndiyo mlezi wetu yule mama."

"Ni kweli kabisa na kama nitakuwa vizuri nitaongozana naye." Mara mama alikuja kunifuata hivyo ikabidi niangane naye kaka yangu na shemeji yangu Kennedy na kutoka sebuleni. Nikiwa naurudisha mlango kuna ujumbe uliingia kwenye simu yangu na nilipoangalia mtumaji ni nani niliamua kuachana naye kwanza maana baba naye alikuwa akinisubiri.


JE NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI TUJUE NINI KITAENDELEA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post