NITAKUUA MWENYEWE - 30
sultanuwezotz.blogspot.com
"Ina maana haya yote yanafanywa na hawa vimburu?"
Mzee Bruno Gautier alijiuliza akiwa bado chini kakaa huku macho yake yakiwa kule kwenye kile anachokishuhudia mbele ya macho yake walinzi karibia wote walikuwa wamepigwa kudu za kutosha nje ya banda ambalo walifungiwa wakina Jackline kwa mara ya pili mara baada ya kutoka kwenye vile vibanda ambavyo walifungwa tofauti tofauti na walinzi hawa walifungwa kila mmoja peke yake na kulazwa eneo moja kama vile wanasubiri hatma yao kutoka kwa Faraoh.
"Jamie nini kimewakuta mbona sielewi elewi jamani?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Jamie kilichotokea, lakini Jamie hakujibu chochote zaidi ya kumtolea macho tu kitu kilichoendelea kumtisha mzee Bruno.
Alipoona hajibiwi chochote aliamua kufanya maamuzi ambayo alihisi yataleta mafanikio usiku huo hivyo alikiendea king'ora ambacho huwa kikigongwa tu watu wote mle ngomeni hutoka haraka kwani huwa ni kiashiria cha hatari.
Alifika na kupeleka mkono kwenye swichi ya king'ora ili abonyeze lakini katika hali ya kushangaza kabla hajabonyeza alikutana na teke moja matata sana lililompata sehemu nyeti na kwenda kuangukia ukuta wa banda lile lililofungwa king'ora kile huku akipiga ukelele wa maumivu.
"Aaaaghhh pu**u zangu jamani."
"Kelele mzee, hautakiwi kupiga kelele unapokutana na sura hizi sawa?"
"Mmmmmmmmmhhhhh."
Mzee alishindwa kujibu zaidi ya kuguna huku akitikisa kichwa sura akiwa kaikunja kama vile anakamuliwa kijipu uchungu.
"Siyo Mmmmmmmmmhhhhh kwani bubu wewe toa sauti yako ile ya kibabe."
"Nimekukoseeni nini mimi?"
"Unataka kujua?"
"Ndiyo nahitaji kujua."
"Okay vizuri sana sasa nakwenda kubonyeza swichi ya king'ora ili kuwatoa nje watumwa wako uliowafuga humu ndani ili uwaeleze kile ambacho ulilenga kukifanya nilipokukuta."
"Ha... !" Kabla hajamalizia alikatishwa.
"Shiiiiiiiiii funga domo lako mzee utaongea king'ora kikijibu."
Kama vile Jackline alikuwa anatania kumbe alikuwa kadhamiria kweli aliisogelea swichi na kuibonyeza huku nyuma mzee alijipapasa kuangalia kama bastola iko sehemu yake ili amuwahi Jackline kabla hajakipiga king'ora lakini alikuwa kachelewa kwani muda ule kapigwa teke la Ikulu na kuangukia ukutani bastola ilianguka pembeni na kuonwa na Jackline ambaye aliichukua, king'ora kililia kweli na watu waliokuwa ndani ya Ngome ile wake kwa waume na watoto walitoka nje huku kila mmoja akiwa hajui usiku ule kuna kitu gani wanakwenda kuulizwa, waliongoza mpaka eneo la makutano na kusubiri kinachokwenda kutokea muda huo Lakini walishtushwa na tukio ambalo lilitokea muda ule kwani taa zote za ulinzi pamoja na zile za kawaida zilizimwa na kuzua taharuki kutokana na giza ambalo lilitanda mbele ya macho yao. Na baada ya dakika kama nne hivi ziliwaka tena na mbele yao tayari kulikuwa na watu wakiwa wamesimama ambao waliwafahamu vizuri sana.
"Poleni kwa usumbufu ndugu zangu na tunaomba mtusamehe kwa kuwaondoa kwenye malalo yenu lakini tulikuwa hatuna jinsi ilibidi iwe hivi. Mbele yenu kuna sura ambazo si ngeni kwenu hasa huyu mzee Bruno Gautier."
"Ndiyooooo....!"
Waliitikia kwa pamoja na bila shaka tayari walishajiandaa kuzipokea taarifa zile kwani hawakuwa na hofu yoyote ile.
"Kiongozi wenu kuna mambo kadhaa anataka kuongea nanyi msikilizeni tafadhari."
Jackline aliendelea kupaza sauti mbele ya umati ule ambao ulikusanyika.
"Poleni na majukumu watu wangu watiifu kwangu." Alianza mzee Gautier.
"Asante twashukuru kiongozi." Walijibu.
"Nimewaiteni usiku huu kutaka kukuelezeni kuwa kuanzia sasa kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kiutawala zaidi katika eneo la Ulinzi ambalo siku za hivi karibuni limeonekana kupwaya sana na mfumo wa maisha pia utabadilika kabisa kutoka kwenye mfumo wa kufanya kazi na kutolipwa mpaka kwenye mfumo wa kulipwa kiasi chochote kitu."
"Ubarikiweeeeee milele kiongozi wetuuuuuu....!!!!!"
Walipaza sauti kumshukuru lakini hawakujua kilichokuwa nyuma ya pazia kwani yale yote aliyoyaongea yalikuwa si maamuzi yake mzee Bruno Gautier bali aliamrishwa na Jackline muda ule taa zimezimwa akisogezwa pale mbele bila wao kujua chochote kile ila kuna baadhi yao waliujua mchezo mzima kwani walikuwa wakishirikiana nao katika kutoa taarifa.
Na baada ya shangwe lile kuendelea pale mara taa zilizimwa tena na mzee Bruno aliondoshwa pale na Jackline mpaka ofisini kwake kule juu huku akimuachia maagizo mmoja wa walinzi ambaye tayari alikuwa mshirika wao kitambo kuwasha taa na kuwataka kurudi vyumbani mwao mpaka kesho ambapo watapewa utaratibu.
Taa iliwashwa tena na kila mmoja alishangaa kuona mbele kukiwa tupu hakuna mzee Bruno wala Jackline lakini alifika yule mlinzi na kuwapa maagizo.
"Mnatakiwa kurudi vyumbani kwenu kuendelea kuutafuta usingizi wenu mlioupoteza ghafla mpaka kesho ambapo taratibu nyingine zitafutwa."
Wakatawanyika wote kutoka lile eneo wakiwa na maswali mengi vichwani mwao.
"Mbona kama naota hivi?"
"Kivipi mzee mwenzangu?"
"Mbona kiongozi wetu leo kaongea lugha rafiki sana ambayo sikuwahi itegemea hata siku moja? Na yule binti mbabe mbona alikuwa karibu yake wakati hawapatani?"
"Hayatuhusu hayo sisi tunachotakiwa kuangalia sasa ni maisha yetu mapya tunayokwenda kuyaishi."
"Ni kweli kabisa mzee mwenzangu, sasa nikutakie usiku mwema."
Waliagana na kila mmoja kuingia sehemu yake. Huku nyuma yule mlinzi aliwafuata wale walinzi wenzake wakina Jamie na kuwafungua zile kama walizokuwa wamefungwa na wakina Jackline.
"Sikilizeni jamaa zangu, mnatakiwa kuungana na mimi katika harakati za kuwaunga mkono hawa ndugu zetu kama walivyosema na kwa yeyote atakayekuwa kinyume nao watampoteza."
"Mimi siko tayari kuhatarisha maisha yangu kisa mzee Gautier nitaungana nao kwanza ukizingatia nilishajiwekea kisasi cha siku moja kuja kumuangamiza mzee huyu baada ya kumuua rafiki yangu Ogingi."
Jamie aliongea hayo kwa uchungu mkubwa huku akiwaangalia wenzake ambao nao walisema wanaungana kuupambania Uhuru wao.
" Hayo ndiyo maneno jamaa zangu na muda huu tunaanza ulinzi feki ikiwa ni pamoja na kufuatilia nyendo zote za mzee Bruno Gautier na kuwataarifu wakina Jackline."
"Kazi rahisi sana hiyo kwanza nimeipenda sana ile kombinesheni ya wale madada na yule bro." Alijibu Jamie na kutoa ya moyoni mwake.
Wakiwa wanapanga yao pale nje kule ndani moto ulikuwa unaendelea kuwaka kati ya mzee Bruno na wakina Jackline.
"Haya mzee tuongee kikubwa sasa kwa sababu tumeagiza jumbe mbalimbali kukutaka uje kule lakini ukatia jeuri na ndiyo maana tuko mbele yako."
Jasmine aliongea kwa mbwembwe akiwa kwenye kiti cha mzee Bruno akizunguka huku na kule kama vile ndiye mmiliki wa kampuni akiwafanyia usaili wafanyakazi wapya.
" Naombeni tuongee mbona haya yanaongeleka kabisa?"
Mzee Bruno Gautier aliongea kwa sauti ya upole.
"Kwa sasa ndiyo yanaongeleka baada ya kukumbana mbavu siyo?"
Jackline alimsogelea mpaka pale alipokuwa kaketi na kumuuliza.
"Mjue pia mimi si mtu mbaya kwenu hata kidogo hayo niliyowafanyia ilikuwa ni katika kutaka kuwajua zaidi kwani nilijua mnanidanganya siku ile na ndiyo maana sijatoa taarifa kokote kule juu ya uwepo wenu hapa kambini."
"Haituhusu hiyo unadhani hata ungetoa taarifa tunaogopa? Haujui kutoa kwako taarifa kutapelekea kupoteza utajiri wako wote na pia kuchukuliwa hatua wewe na jamaa yako Santana au unafikiri hatujui kuwa Santana ana hisa karibia asilimia hamsini na tano na zinazobakia ndiyo zako wewe na mjomba wako aishiye Misri?"
Jackline alimchana ukweli.
" Mmeyajua vipi haya wakati ni mambo ya ndani sana?"
Mzee Bruno Gautier alitokwa na macho baada ya kuambiwa ukweli huu.
" Tumepata wapi taarifa hizi siyo kazi yako ila tu unachotakiwa kujua ni kuwa sisi ni moto wa kuotea mbali kwani ukiotea karibu nini kitatokea?"
" Hapo lazima uungue."
Alijibu mzee Bruno huku akitazama chini.
"Halafu mzee unajiona jeuri sana wewe?"
Robinson aliuliza naye swali.
"Kivipi kijana wangu?"
"Sikiliza mzee Santana unamjua humjui maana uliuliza tu baada ya kuambiwa na kisha ukaishia kuuliza tu swali."
"Ni kweli namfahamu vizuri kama mlivyo sema ni Shareholder mwenzangu ila mimi nina dhamana ya kusimamia mgodi huu kutokana na uzoefu wangu kwenye eneo hili na juzi hapa nilimtaarifu juu ya uwepo wenu na akasema niendelee kuwahadaa ili siku ikifika aje na watu wake kuwakamata na kisha kuwanyofoa viungo vyenu muhimu kama Moyo, Figo, Macho, na Ulimi kisha kuwauwa na kwenda kuviuza vitu hivyo India ambako vina soko sana na ni biashara ambayo tumekuwa tukiifanya kwa kuwafanyia hivyo watumwa wetu wa hapa na wale wanaojipendekeza kwake kupitia Mitandao ya kijamii kama nyinyi... "
" Keleleeeeee..... "
Jackline hakutaka kuendelea kuusikiliza upuuzi ule uliokuwa ukielezwa na mzee Bruno Gautier.
" Sikiliza mzee inatosha sana kwa madhambi yenu mliyofanya kwa damu zisizo na hatia na sasa ni muda wenu kuyalipia haya na mtayalipia vipi itafahamika."
"Wewe ni kama mwanangu najua kwa umri wenu ninyi bado mnayapambania maisha ikiwa na wewe kuzipigania Mali za marehemu baba yako na mama yako hivyo basi mimi niko tayari kutoa msaada kwa kufanikisha kumtia nguvuni mzee huyo aliyedhulumu na pia kuwapa nusu ya utajiri wangu ambao ni mabilioni ya dollar ikiwa tu mtaniacha huru na biashara zangu."
Mzee Bruno Gautier alitoa ahadi hizo mbele ya wakina Robinson. Kitu kilichomfanya Robinson kutoa mimacho kwenye mgao huo ambao alijua umaskini kwa heri lakini akashangazwa na majibu ya wenzake.
" Ndiyo unajidanganya hivyo mzee Bruno Gautier? Hatudanganyiki na vihela sisi ila tu ili uendelee kuishi utapaswa kufanya yale ambayo tutahitaji uyafanye muda huu, sijui uko tayari?" Jackline alimuuliza.
"Niko tayari hata sasa."
"Lakini watu wangu mnaonaje kama tukijibebea mihela hiyo na kutokomea zetu kwetu?" Robinson aliwauliza wenzake.
Kitu kilichowafanya wakina Jackline na Jasmine kutazamana kwa sekunde kadhaa kabla ya Jasmine kumjibu.
"Inaonekana una uchu na vihela vya mzee huyu ambaye anachozungumza hakina ukweli ndani yake."
"Hapana Jasmine nilikuwa nauliza tu."
"Dada zangu muwe makini naye huyo tayari kaota pembe zinazoweza kutuchoma."
Jessica aliongezea lake kama tahadhari.
"Kwa hilo Robinson hawezi kufanya namtetea alikuwa akitoa wazo tu jamani tuwaze mbali sana."
Jackline alimtetea mpenzi wake.
"Yameisha hayo tuendelee na mzee Bruno."
Jasmine aliongea akimuangalia mdogo wake kwa jicho la kumtuliza.
KUNA NINI HAPO?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO