MUUAJI MWENYE BARAKOA - 23
sultanuwezotz.blogspot.com
Alipoingia kwenye kile chumbani alimfuata Mchungaji Rodney Hauser na kumkagua mifukoni mwake na kufanikiwa kutoa waleti pamoja na simu nyingine aina ya 'Motorola smartphone T45' kisha akaviweka mfukoni mwake.
"Mchungaji Simon endeleeni na maombi ngoja mimi nifanye kazi moja hivi." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia.
"Sawa baba, mlango wa ofisi uko wazi haukufungwa." Mchungaji Simon Mwaiduko alimwambia kiongozi wake.
"Okay basi endeleeni na maombi akizinduka na kila kitu kuwa sawa mtaniita."
"Sawa baba." Mchungaji Simon Mwaiduko alimjibu. Kisha Daktari Sylvester Kitesa alitoka na kuelekea iliko ofisi ya Kanisa hilo na baada ya kuingia alirudisha mlango, akatoa vitu alivyovitoa kwa Mchungaji Rodney na kuviweka mezani kisha alivua koti lake na kuliweka nyuma ya kiti. Alisogea mbele kidogo akavuta pumuzi kwa nguvu kisha alifumba macho na kuanza kuomba kwa Mungu.
"Ee Mungu baba nakushukuru kwa Upendo wako na Baraka zinazoendelea kumiminika ndani ya jengo hili. Nasema asante sana na sisi tukiwa kama daraja na waonyesha njia hatutachoka kuwaongoza wapendwa wako malangoni mwako, imani yetu ikaimarike kila iitwapo leo ili majaribu ya wakala wa Shetani walio kila kona chini ya jua wakashindwe. Ni katika wewe unitiaye Nguvu, nikiomba na kushukuru. AMEEN!" Kisha alirejea kitini akaketi na kuanza kuikagua ile waleti ya Mchungaji Rodney.
" Ooh my God! Nini hiki? " Daktari Sylvester Kitesa alijiuliza mara baada ya kukikuta kibahasha cha kaki kilichokuwa na vifuko vidogo viwili vya nailoni kimoja kikiwa na unga mweupe na kingine kikiwa na unga mweusi. Hii ikamfanya azidi kuikagua ile waleti vizuri, alijikuta mwili ukitokwa na kijasho chembamba kilichotiririka kwenye uti wa mgongo wake na hii ni mara baada ya kukutana na shanga nyeupe iliyotungwa kwenye kiuzi cheusi.
"Mhhh Mchungaji Rodney ni Mungu gani unayemuamini wewe?" Daktari Sylvester Kitesa alijiuliza akivirudisha vile vitu vilimokuwa kwenye waleti.
"Ee Mungu tupe jicho la tatu lenye nguvu tuweze kuyaona ya sirini." Alishukuru akiitoa simu ya awali ambayo ilipotea ujumbe uliomfanya Mchungaji Rodney kupoteza fahamu kisha akaichukua namba ile na kuipiga.
"Haloo!"
"Haloo, naitwa Daktari Brown Lutasya naongea na nani tafadhali?" Alijitambulisha baada ya kuipokea simu.
"Daktari Sylvester Kitesa hapa, bila shaka wewe ni miongoni mwa wazee wa Baraza la Wadhamini wa Kanisa la JESUS OUR KING nchini Senegal sijui niko sahihi?" Aliuliza.
"Hujakosea ni kweli kabisa na wewe je?" Aliuliza baada ya kukubali.
"Mimi ndiye Mkurugenzi mkuu wa Makanisa haya nchini Tanzania lakini pia nahudumu mara moja moja Makao makuu jijini Mbeya." Alimfafanulia.
"Ooh Bwana Yesu asifiwe Kiongozi!" Utambulisho huo ulimshtua kidogo Daktari Brown kwani hakutarajia kuongea na kiongozi kama huyu.
"Amina Daktari mwenzangu, nafurahi sana kuona Kanisa letu lina Madaktari wa kutosha. Wanasemaje Senegal?"
"Haswaa baba kiongozi, huku si kwema kabisa kwani Mchungaji wetu Rodney hajapatikana mpaka leo..."
"Kwani alipotea?" Daktari Sylvester Kitesa aliuliza kama vile hajui kinachoendelea.
"Ni muda mrefu sana na hii ilikuja mara baada ya mke wake na mlinzi kupotea na kuuawa lakini mama Mchungaji kaonekana jana usiku nyumbani kwao aliingia na kisha kutoka akitumia moja ya magari yao." Daktari Brown alieleza.
"Una uhakika ni yeye? Na mlifuatilia kujua anaelekea wapi?" Aliuliza Daktari Sylvester Kitesa.
"Kiukweli hatuna uhakika wa moja kwa moja kwani taarifa hizi tuliambiwa na jirani yao aliyenipigia simu na tukapata uhakika kidogo kuwa inawezekana baada ya kufika pale na kutolikuta gari moja ambalo alipenda kulitumia yeye mama Mchungaji."
"Polisi mlikwenda kutoa taarifa hizi?"
"Hapana baba Kiongozi." Alijibu Daktari Brown.
"Okay hebu fanyeni uchunguzi wa chini chini kujua yuko wapi ikiwa ni pamoja na kutafuta mawasiliano yake."
"Sawa baba."
"Basi fanyeni hivyo na sisi huku tukiendelea kumtafuta Daktari Rodney." Daktari Sylvester Kitesa aliongea.
"Kuna tetesi zinasambaa kuwa yuko huko Tanzania sijui ni za kweli?" Aliuliza.
"Hizo ni tetesi tu kiongozi na kama ni za kweli basi tutamuona wala msihofu."
"Sawa baba."
"Tujuzane kila hatua ambayo mtaifikia."
" Bila shaka kabisa Kiongozi." Daktari Sylvester Kitesa alikata simu baada ya mlango kugongwa aliuangalia kisha akatoa vitu pale mezani akainuka na kwenda kuufungua.
" Mchungaji kuna Habari gani huko?" Alikuwa ni Mchungaji Simon Mwaiduko ndiye aliyekuwa akibisha hodi.
" Mungu mkubwa baba Kiongozi mgeni wetu ameshazinduka tayari."
"Asante Mungu wangu, asante sana kamleteni sasa." Alifurahi sana kupata taarifa hii ya kuzinduka Mchungaji Rodney.
"Sawa baba Kiongozi." Mchungaji Simon Mwaiduko alijibu na kutoka. Na kumuacha Daktari Sylvester Kitesa akiendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa muujiza alioufanya.
"Ni muda muafaka wa kupata machache kutoka kwake yanayomhusu mke wake." Aliwaza Daktari Sylvester akiwa kaiinamia meza.
***
Awadh alibana kwenye ukuta wa nyumba ya jirani na Hotel ya mzee Malick ambapo kuna mtu alikuwa akija kasi huku risasi zikimfuata nyuma.
" Mamaaaaa........ " Ulikuwa ni mlio wa maumivu makali baada ya kukutana teke kifua kutoka kwa Awadh aliyekuwa kajiandaa. Na kabla hajamsogelea mtu huyo alishafika Jumbe akiwa kachakaa huku sura yake imetapakaa damu.
"Awadh? Mlikuwa wapi?" Jumbe aliuliza akimrukia kwa furaha.
"Tutaongea lakini huu si muda muafaka." Awadh alimjibu akimsukuma pembeni Jumbe kumuepusha na risasi ambayo mtu yule alikuwa anajiandaa kuifyatua kisha yeye Awadh akamshindilia za kutosha kichwani na kifuani.
"Asante brother." Jumbe alimshukuru akimuangalia mtu huyo.
"Usijali, umemtambua?" Awadh alimuuliza.
"Huyu ni miongoni mwa vijana wa IT wa mzee Malick Bolenge ndiyo waliotufanyia shambulizi la kushtukiza kiasi cha kummaliza Mathew." Alimjibu.
"Kwa hiyo ni kweli Mathew hatuko naye?" Awadh aliuliza kwani hakuamini ambacho alichoambiwa na Seynabou.
"Ni kweli tupu wala si utani kaka hawa jamaa si watu wazuri hata kidogo huko ndani kulikuwa kudogo acha tu." Jumbe alimjibu akitema mate yaliyochanganyika na damu.
"Poleni sana, na vipi kuhusu Seynabou?"
"Yule mwanamke nilimdharau duu ni moto wa kuotea mbali kawasambaratisha huko wee acha tu kwanza hebu twende alikuwa akifukuzana na dada mmoja mle ndani." Jumbe alimjibu wakiondoka mbio. Waliupanda ukuta na kutinga ndani ya Hotel kwa kutumia mlango wa 'Emergency' ambao waliutumia wakati wanatoka na kijana aliyesambaratishwa na Awadh. Walishachelewa kwani waliwakuta wakina Adoyee wakiwa na Seynabou wanakikagua kile chumba chenye kompyuta ambazo baadhi yake zilikuwa zimechakazwa na risasi.
"Wanajeshiiii....!" Awadh alipiga kelele baada ya kuiona timu yake.
"Hapana chezea hili 'crew' ni moto mwingine kabisa omba usikutane nao." Seynabou alijibu akikumbatiana na Awadh.
"Kwanza poleni kwa yaliyowakuta." Awadh aliwapa pole.
"We acha tu Awadh yaani ile namaliza kukutumia ujumbe wa mwisho jinga moja hili hapa likiwa limevurugwa, si likamvaa Jumbe ambaye hakuwa na silaha yoyote muda huo na kuanza kupimana ubavu. Jumbe alimsambaza chizi yule we acha tu lakini bado nikaona anamchelewesha si nikamfyatulia risasi iliyozua tafrani mle ndani kwani waliokuwa nje wakajua tuko kwenye kile chumba." Seynabou aliwasimulia.
" Kilichoendelea baada ya hapo?" Soud aliuliza.
" Unauliza kilichofuata Soud? Muulize Jumbe nilichowafanya pale mlangoni." Seynabou alimjibu.
" Kila aliyekuwa akiingia ndani alikutana na risasi ya kichwa kutoka kwa Seynabou mpaka yule mmoja aliyekuja dirishani na kuachia risasi ambayo hata hivyo haikuwa na madhara lakini ndiye aliyesaidia wanne kuingia wakati sisi akili ikiwa dirishani wao ndiyo wakatuvaa na kuanza kutudunda. Lakini tuliwaonesha ni kwanini sisi ni timu ya ushindi." Jumbe alimaliza.
" Poleni sana ndugu zetu, lakini kuna mtu mmoja haonekani hapa?" Adoyee aliuliza.
" Nani mzee Malick?" Seynabou alimuuliza.
" Huyo huyo."
"Lile dingi ni chawi wala si hivi hivi kwani wakati kimechanganya alitoroshwa na mmoja wa wafanyakazi wake ila kuna yule mpishi niliyepiga na kumfungia kule uliko mwili wa Mathew ndiye ataeleza kila kitu ikiwa ni pamoja na kuchimba kaburi." Seynabou alimjibu akiwaongoza wenzake kwenye hicho chumba.
" Vipi kuhusu hiki chumba?" Soud aliuliza.
"Mfumo umeharibiwa hapo hakuna jipya." Awadh alimjibu wakitoka lakini Soud kwa hasira alirudi na kuzisambaza zile zilizosalia na baada ya kuridhika alitoka zake.
"Oyaa tokeni haraka shoti imeanza kwenye kile chumba."
"Nini wewe?" Seynabou aliuliza.
"Acha maswali jengo linashika moto muda si mrefu." Soud alijibu akiushika mkono wa Seynabou na kuanza kumvuta.
"Ndiyo umefanya nini sasa?" Seynabou alimuuliza Soud ambaye hakujibu zaidi ya kuongeza hatua kuelekea nje.
"Ongeza spidi ninyiii....!!!" Awadh aliwaambia baada ya kuona limeanza kuwaka moto. Kama bahati hivi ile wanafika tu nje jengo liliwaka moto.
"Soud utatuua wenzako bwana ndiyo nini sasa?" Adoyee alimuuliza.
"Sikutarajia hili kutokea mimi nilikuwa nahesabu nyingine kabisa."
"Hesabu gani hizo bwana angalia sasa tumeshindwa kuuzika mwili wa mwenzetu Mathew." Seynabou alimuuliza.
"Tuangalie tunatoaje taarifa kwa dada mkubwa hili lilishatokea tayari hakuna haja ya kutupiana lawama, ama vipi?" Jumbe aliwaondoa kwenye malumbano na kuwataka kuangalia Catherine anapataje ujumbe. Wakiwa wanajadiliana hilo mara simu ya Seynabou iliita ikabidi aipokee.
" Uko wapi dada? " Seynabou alimuuliza.
" Kuna sehemu niko nipe habari ya huko." Catherine aliuliza.
"Huku mambo ni magumu dada mzee Malick hatujafanikiwa kumtia mikononi badala yake tumempoteza Mathew inauma sana." Seynabou alimjibu.
"Unasemaje?" Catherine alimuuliza.
"Ndiyo hivyo na hapa bado tuko nje Hotel tukiishuhudia inavyoteketea." Seynabou alimjibu lakini Catherine hakuongeza neno zaidi ya kukata simu.
"Anasemaje dada mkubwa?" Awadh aliuliza.
"Amepaniki si unamjua mambo yake? Kakata simu." Seynabou alimjibu.
"Tuondokeni mahali hapa najua muda si mrefu tutapokea simu ya dada kiongozi ya maelekezo hivyo tunatakiwa kufanya maandalizi." Jumbe aliwaambia wenzake waliokuwa wamekaa macho yakiwa kwenye Hotel ya TRAVIS MARK iliyokuwa ikiishia lakini kilichoanza kuwatisha zaidi ni kitendo cha moto kuhamia nyumba ya jirani ambayo haikuwa ya biashara bali ya mtu binafsi ya kuishi.
" Janga jingine hili?" Seynabou aliongea baada ya kuuona moto unavyohama.
"Hili giza kwetu ni msaada hebu tuondokeni haraka kabla chochote hakijatokea hapa." Awadh aliongea huku akiwapa ishara wakina Seynabou kuingia kwenye gari.
"Tunapitia mtaa wa nyuma ambako tulilificha gari letu." Awadh aliwaambia wenzake.
"Washa gari kaka." Jumbe alimwambia Awadh akihisi kama vile anachelewesha muda, waliondoka eneo hilo huku kwa mbali wakisikia mlio wa king'ora.
JE NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA MBIVU NA MBICHI KWENYE KIGONGO HIKI.
#SULTANUWEZO