MTOTO MALATWE - 18
sultanuwezotz.blogspot.com
Mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea huku Malatwe akiwa kajaa woga kutokana na mazingira aliyoyakuta kwa bibi Mpinge. Na hilo alilitambua baada ya kuona mgeni wake hatulii pale alipokaa hivyo aliamua kutengeneza mazingira ya kumfanya asimuogope.
" Hivi ulisema umetokea wapi kweli?" Bibi Mpinge alimuuliza Malatwe.
" Mimi natokea mkoani Songwe na hapa nilikuja tu kwa msaada wa kaka Naboti ambaye tulikutana Makambako." Alimjibu.
" Na Makambako ulifuata nini maana Songwe ni mbali mpaka uipite Mbeya?"
" Kiukweli nilikuja kumtafuta mama yangu ambaye alitoweka miaka kadhaa nyuma."
" Makubwa, yaani alikuacha peke yako?" Lakini Malatwe badala ya kumjibu alianza kulia kitu ambacho kilimsogeza bibi Mpinge karibu na kuanza kumtuliza.
" Mhh kama nimekukwaza kwa maswali yangu naomba unisamehe mjukuu wangu, hebu malizia kula nikueleze kile unachopaswa kukijua kuhusu wenyeji wako." Alimbembeleza.
" Asante bibi nashukuru." Alimjibu. Baada ya kumaliza kula bibi Mpinge alitoa vyombo na kisha alirudi pale na kuketi wakati huo huo Malatwe alikaa sawa kutaka kujua kilichowakutanisha pale.
"Mjukuu wangu!" Aliita bibi Mpinge.
" Naam bibi." Aliitika.
" Huyo Naboti unamjua vizuri?"
" Hapana bibi kama nilivyokwambia awali kuwa nilikutana naye tu Makambako na haikuwa rasmi bali ilitokea tu." Malatwe alimjibu.
" Iko hivi mjukuu wangu, huyo Naboti na mke wake maisha yao wanayajua wenyewe kwani huyo unayemuita shemeji yako hajaanza kuchepuka leo toka wakiwa wachumba na huyo uliyemkuta naye ndiye huyo huyo toka kitambo hicho."
" Na bwana yake analijua hilo?" Malatwe alimuuliza.
" Anajua vizuri tu na ambacho hua anakifanya ni kumpotezea na kuendelea na mambo yake japo kumuacha hawezi kwa kuwa anazijua siri zake nyingi hivyo anahofia akimuacha siri zake zitakuwa nje."
" Bibi ulijuaje haya wakati huishi nao sehemu moja?" Malatwe alimuuliza.
" Ni la kuuliza hilo? Kama unavyojua mambo mabaya huenea kama moto wa petroli na mazuri hujivuta kama mwendo wa kinyonga."
" Mhh kwa hiyo mimi nilijikoki kwenye hili eti bibi?" Malatwe alimuuliza.
" Hapana cha kufanya wewe ni kufuata yako yasiyokuhusu achana nayo, na kingine unatakiwa kuwa makini na huyo Naboti kwa shughuli azifanyazo ni za hatari usije ingia matatani."
" Sijakuelewa hapo bibi una maana gani?"
" Utanielewa tu, kaka yako anajishughulisha na biashara haramu zilizopigwa marufuku za bangi huwa anazifuata huko vijijini na kuzipeleka Makambako na mara moja moja hapa kijijini." Alimfafanulia.
" Ndiyo maaana!!" Malatwe alishangaa.
" Nini?"
" Hapo naanza kupata picha kwa mfano kama jana aliondoka asubuhi na kurudi usiku pia leo kafanya hivyo hivyo."
" Ndiyo maana nimesema kuwa makini, umenielewa?"
" Nimekuelewa bibi." Alimjibu.
" Vizuri yafanyie kazi haya niliyokueleza tofauti na hapo usije kujilaumu yakikutokea puani." Baada ya kuhitimisha mazungumzo yao Malatwe aliomba kuondoka kwani muda ulikuwa umesogea hivyo alihitaji kurudi nyumbani. Bibi Mpinge hakuwa na pingamizi lolote juu yake alimruhusu akaondoka. Hakupitia popote aliongoza moja kwa moja nyumbani lakini akiwa kama mita kadhaa kufika nyumbani alikutana na tukio, alimkuta kijana mmoja akimvuta mbuzi kama vile alikuwa anampeleka machungoni.
" We dogo naomba unisaidie kumvuta huyu mbuzi nataka nimfunge pale kwenye kile kichaka." Aliitwa Malatwe.
" Nani mimi?" Aliuliza.
" Ndiyo naongea na wewe au kuna mwingine hapa? Dogo mbona hivyo?"
"Sawa." Alimjibu, kisha akakatisha safari yake na kumfuata mtu huyo aliyeomba msaada. Aliikamata kamba na kuanza kumsaidia kumvuta yule mbuzi aliyekuwa akirukaruka kugomea alikokuwa anapelekwa.
" Huyu mbuzi wako mbona mbishi sana?" Malatwe aliuliza baada ya kuona ni mbishi sana.
" Mbuzi ndivyo walivyo kwani kwenu hakuna mifugo?"
" Ipo ila mbuzi ni kuku tu." Alimjibu.
" Malatwe unafanya nini huko na huyo mwizi?" Aligeuka kumtazama aliyemuuliza swali.
" Waoo shemeji ni wewe?" Alimuuliza akiiachia ile kamba na kumfuata Judith.
" Nauliza imekuwaje uambatane na huyo mwizi?" Alimuuliza tena.
" Nani mwizi? Hebu jaribu kujiheshimu wewe sista." Kijana yule alimuuliza Judith.
" Si wewe hapo kwani hujijui kama wewe ni jizi lililokubuhu?" Jibu lile lilimfanya kijana yule a unachievable mbuzi na kuanza kuwafukuza wakina Malatwe ambao nao hawakutaka kubaki nyuma walitoka mbio kujiepusha na kichapo kutoka kwa kijana huyo ambaye alitibuliwa na Judith. Mbio zao zilikwenda kugota nyumbani kwao huku wote wakizama nyumba kubwa.
" Yaani shemeji na wewe hakuna kitu mimi nilijua niko na kidume kumbe sifuri kabisa!!"
" Kidume? Yaani uyatibue wewe halafu mimi nibebe dhamana? Aa thubutu hilo siliwezi labda kama kuna jingine?" Alimjibu akitoka nje na kumuacha Judith aliyekuwa akihema juu juu.
" Safari ya wapi sasa?" Judith alimuuliza Malatwe.
" Kulala." Alimjibu kwa mkato na kutoka.
" Nakiona kiburi chako Nguruwe wewe." Alimsindikiza kwa tusi ambalo hakulisikia kwani tayari alishakuwa mbali. Aliingia chumbani kwake na kujilaza pale mkekani lakini kichwani akiyachambua yale aliyoambiwa na bibi Mpinge juu ya wenyeji wake. Aliwaza na kuwazua kupata jibu lakini bado hakuweza kupata kutokana na ugeni alionao kijijini hapo. Na kikubwa kilichokuwa kikimuumiza kichwa ni namna alivyoachana na walezi wake na kuangukia mikononi mwa rafiki yake Linus Litonovela ambaye hakumjua kiundani na sasa ulikuwa ni muda wake wa kuondoka na kurudi Makambako akafanye mpango wa kurejea kwao Songwe hivyo baada ya kuukamilisha mpango wake wa namna ya kuondoka alitoka akaikuchukua ndoo na kwenda bombani kuchota maji ya kuoga.
" Leo usiku ni lazima nitimue vumbi haya masuala ya kwenda jela kwa kosa ambalo si langu ni ujinga. Na ndiyo maana hakuna amani ndani ya nyumba kila mmoja ni kivuruge huyu mchepukaji mwingine muuza bangi sasa ukichanganya unapata nini kama siyo matope." Alikuwa akiyawaza hayo akielekea bombani. Lakini kwa mbali aliweza kumuona shemeji yake akiwa kando ya gari dogo jeupe.
" Duu huyu katoka muda gani ndani? Hii kali na huyu aliyenaye ni nani tena?" Malatwe alijiuliza akitafuta sehemu iliyojificha vizuri ajifiche aweze kuwachora. Hakuwa na mpango tena wa kukinga maji ya kuoga badala yake akili yake akaielekeza aliko shemeji yake. Akiwa anatafuta sehemu nzuri ya kujificha alimuona shemeji yake akiingia kwenye gari kisha wakatokomea zao.
" Shemeji ninaye aisee sasa wanakwenda wapi muda huu? Mmh lakini hayanihusu wacha nikinge zangu maji nikaoge haraka ikiwezekana kabla hawajarudi mimi nitakuwa mbali nikihesabu hatua." Alijisemesha akilisogelea bomba la maji. Alikinga ndoo yake ilipojaa aliibeba na kuondoka kurudi nyumbani.
" Acheni kunibishia ninyi, mimi nina uhakika huyu aliye kwenye hili gazeti ni yule yule dogo aliyekuwa na Naboti pale kilabuni."
" Wanafanana tu wala si mwenyewe bwana." Akiwa anapita karibu na nyumba fulani aliyasikia mabishano kutoka ndani ambayo yalimfanya afunge breki baada ya kulisikia jina la Naboti.
" Hebu iangalieni hii picha hapa ina utofauti gani na yule dogo?" Mmoja aliwaambia wenzake.
" Kwa hapa sina neno ni mwenyewe kabisa hebu mcheki hata huu mwanya kama yule dogo, mimi nafikiri hakuna cha kupoteza ni kuelekea nyumbani kwa Naboti tukamchukue tumpeleke Makambako tukachukue chetu kila mmoja kimpango wake hakuna kujuana tena kijijini tumebanana sana." Mmoja wao aliwaambia wenzake ambapo walitoka kuelekea kwa Naboti na muda huo Malatwe alikuwa kabana kwa nyuma akisikiliza.
"Ina maana natafutwa?" Alijiuliza akiivuta ile ndoo kutoka pale alipokuwa kaiweka huku akiyazungusha macho kuona kama kuna anayemfuatilia pale alipokuwa.
" Supu imeingia vumbi, hakuna cha kwenda kuoga wala nini siwezi kujua ni nani anayenitafuta na kwa kosa gani? Kama siyo wakina Linus wameniuzia kesi hapa." Aliongea na kuikamata njia inayokatisha katikati ya shamba la mahindi na kuanza kukimbia kuwakwepa wale watu wanaomsaka. Hakutaka kujiuliza mara mbili mbili anakokwenda yeye aliangalia kuinusuru roho yake tu.
" Hakuna mwingine huyu ni Linus na baba yake tu wameamua kunitafuta popote ilmradi kunishikisha. Hapa hashikwi mtu wala nini." Malatwe aliongea haya akikivuka kikorongo kilichokatisha ndani ya shamba hilo. Alikimbia sana na kujikuta ndani ya kimsitu chenye vichaka vichache na kuelekea kupangua huku jasho likimtiririka kutokana na jua lililokuwa limewaka kama limetumwa hivi na kwa mbali aliweza kuziona paa za nyumba ziking'aa.
" Kumbe na huku kuna makazi ya nyumba vizuri sana lakini tahadhari ni muhimu nisije angukia kwenye mikono kama ya wakina Naboti bure." Alijisemesha.
Baada ya mwendo mrefu Malatwe alikuwa pembezoni mwa shamba la matunda ya parachichi akalipita huku akiyashangaa kwa namna yalivyokuwa yamebeba huku miti yake ikiwa midogo.
" Haya ni maparachichi kweli mbona miti ni midogo tofauti na ya kule nyumbani?" Alijiuliza akilipita shamba hilo.
" Haa kumbe hii ni shule?" Alijiuliza baada ya kukutana na kibao kilichosomeka 'EMABERG SCHOOL' ikiwa ni shule iliyo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Alipita hapo kwa mwendo wa hofu kwani hajawahi kupita kwenye mazingira ya shule za juu tofauti na shule za msingi ambazo kasoma. Alipoipita tu mwendo ule ule uliendelea wa mbio na hii ni baada ya kusikia ngurumo za magari akajua amekaribia barabara ya magari.
" Eee Mungu wangu nisimamie nifike barabarani kabla sijatiwa nguvuni." Aliongea akiifunga kamba ya raba yake iliyokuwa imefunguka. Na baada ya kuinuka alitembea kidogo tu akawa ameifikia barabara ya lami iendayo Songea kutokea mjini Makambako.
" Hapa ndiyo kwenye mtihani, Makambako ni wapi?" Alijiuliza akiwa hajui uelekeo ni upi.
" Potelea mbali acha nielekee huku itafahamika kuliko kuuliza mtu yeyote ambaye simfahamu." Alielekea upande wa Njombe akiamini ndiyo Makambako. Alitembea kwa muda mrefu kidogo baada ya kuona kachoka aliamua kusimamisha gari la abiria lililokuwa likija.
" Ingia haraka kuna mwanga nyuma." Kondakta alimwambia Malatwe. Aliingia na safari ilianza mle ndani alisimama kutokana na abiria kutosha kwenye viti vyote. Kwake haikuwa tatizo alisimama karibia mlango kijana damu inachemka na kwa kuwa ilikuwa ni ligi kati ya lile basi na basi lililokuwa nyuma yao mwendo ulikuwa ni wa kasi na ndani ya dakika kadhaa walikuwa wamefika Kibena na ndipo kondakta alimgeukia Malatwe kumtaka ampe nauli.
" Chekecha mifuko yako."
" Shilingi ngapi?" Malatwe aliuliza.
" Unashukia wapi?" Kondakta alimuuliza.
" Mimi nakwenda Makambako."
" Unasemaje dogo?" Ni kama hakumsikia vizuri hivyo alimuuliza tena.
" Naelekea Makambako."
" Nahisi dogo una matatizo ya akili si bure aliyekwambia huku ni Makambako ni nani?" Abiria waliokuwa viti vya karibu waliagua vicheko kwa kile Malatwe alichoongea walihisi ana tatizo la akili haikuwa bure hata kidogo.
" Dogo umenyofua fyuzi nini yaani hujui kama huku ni Njombe?" Abiria wa karibu yao alitia utani.
" Kwa hiyo huku siyo Makambako?" Malatwe aliuliza.
" Suka ee hebu sugua pedali kuna mbu wa malaria kapenya kwenye neti." Kondakta alimwambia dereva asimamishe gari, na baada ya kusimama alimtaka ashuke.
" Na ushukuru Mungu umenikuta leo hii ya nyumbani hayajanipanda ningekushushia porini na hela yangu ungetoa kokorochi wewe." Alionekana kukerwa sana na kilichofanywa na Malatwe. Alishuka na kisha wao wakaendelea na safari, Malatwe alijivuta pembeni kidogo akiwa hajui aanzie wapi kutokana na ugeni wa eneo. Alijiangalia mfukoni kuona kama ana salio lolote.
" Afadhali." Alijisemea baada ya kukutana na gome la shilingi mia tano. Alikwenda yalipokuwa yanachomwa mahindi na kumuomba muuzaji amtafutie wa kufanana na ile hela.
" Mahindi yameanzia shilingi elfu moja wa hela hiyo huwezi kuupata labda chukua huu hapa." Alimuonesha mhindi ambao ulikuwa umejaa mapengo, hakuwa na jinsi aliupokea na kuanza kuula pale pale huku akiwa anamuangalia sana muuza mahindi kama vile kuna kitu alitaka kumwambia.
JE SAFARI YA MALATWE ITAISHIA WAPI?
TUUNGANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA TAMATI YAKE.
#SULTANUWEZO