IMETOSHA MAMA MKWE - 19
sultanuwezotz.blogspot.com
Ghafla mama Fabiana alirudi ndani mbio na kupitiliza jikoni ambako huko nako hakukaa sana alirudi na kuketi macho yakianzia kwa baba kisha kwa mama na alipojiridhisha ndipo aliponigeukia mimi.
"Tina na mwanao nenda chumbani kwako tupishe mara moja."
"Kuna usalama mama?" Nilimuuliza maana aliniambia hivyo huku upande wa kitenge ukiwa usoni kwake kufuta jasho.
"Ni salama Tina fanya kama nilivyokuambia tafadhali." Alinijibu.
"Sawa mama nimekuelewa." Niliinuka na kuondoka pale sebuleni na kuelekea chumbani ambako nilimlaza mtoto na kwa kuwa nilikuwa nina hamu ya kutaka kujua kilichomfanya Bi Matilda kunitoa pale sebuleni hivyo nikatoka na kujificha koridoni ili kuyapa nafasi masikio yangu kudaka kila neno ambalo lilikuwa likitoka midomoni mwao.
"Ndugu zangu nilitaka huyu Tina atupishe kwanza maana ndugu zake wameshawasili tayari na hivyo nimewaweka kwanza kwa jirani yangu ili tujadili kwanza huo ujio wao si mnajua toka nimefika hatujalizungumzia hili." Mhh kumbe wamefika sasa kwanini wanitoe pale au ndiyo wamepanga kunioza kwa nguvu nini.
" Unajua nini shemeji yangu hao watu nawasubiri sana na hakuna haja ya kujadili kwanza maana wao ndiyo wenye shida na sisi jukumu letu ni kuwasilkiliza mengine yatazaliwa baada ya kuyasikia maelezo yao." Baba alimjibu mama Fabiana.
"Hata mimi naungana na mume wangu katika hili kwamba wao waitwe tuwasikilize wana lipi la kutueleza kisha na sisi tutawajibu kutokana na yale ambayo watayaongea kwanza nina hasira nao hao wee acha tu kumkatishia masomo mwanangu basi tu." Mama naye alipigilia msumari na hivyo kumfanya Bi Matilda akubaliane nao na kuamua kuinuka na kutoka nje bila shaka ni kuwafuata wageni.
" Hivi ikiwa kama watasema wamekuja kuniposa nitafanyaje? Au kama watasema wanamuhitaji mtoto wao nitafanyaje?" Ni maswali ambayo yalikuwa yakipita kichwani kwangu wakati mama Fabiana katoka nje. Na mara mlango ulipambwa na sura mpya kabisa ambazo zilikuwa tayari kukaribishwa ndani na mwenyeji wao Bi Matilda.
" Karibuni wageni, karibuni sana." Bi Matilda aliwakaribisha wageni wake ndani.
"Asante sana mama tumekaribia." Nilipowachungulia walijibu huku wakiwa wanavua viatu vyao pale mlangoni lakini baada ya kuwaangalia vizuri sikuweza kumuona Meshack zaidi ya yule kaka yake ambaye nilimuona shuleni ile siku tulipofukuzwa shule.
"Karibuni mketi wageni." Bi Matilda aliwakaribisha huku akiwaonesha mahali pa kuketi.
"Asante tunashukuru." Mmoja wao alijibu wakiketi na hapo ndipo nikatafuta upenyo bila wao kuniona wa kuelekea jikoni ambako nitakuwa huru zaidi kuliko hapa nilipokaa hivyo kwa kulitumia korido lisilotokea sebuleni nililipita na kuelekea jikoni ambako nilimkuta dada Noela ambaye kwenye mambo kama haya ndiyo balaa ni mmbea hatari.
"Kama kawaida yako umeacha na kupika masikio kama madishi ya televisheni za zamani unahatari wewe!!" Nilikwambia hayo baada ya kumkuta akiwa kategesha masikio kwenye mlango aliokuwa kauegesha.
"Huna lolote Christina hata wewe ni kama mimi tu tofauti yetu ni umri tu mimi ni mkubwa na wewe ni mdogo lakini ndiyo hivyo mwenzangu tayari unaitwa mama na muda si mrefu unakwenda kuitwa mke wa Meshack." Alinijibu akivifuata viungo alivyokuwa kaviweka mezani na kusogea navyo pale pale mlangoni.
" Dada Noela naomba usinitafute tafadhali." Nilimtahadharisha baada ya kuona ananipanda kichwani.
" Hebu niondokee humu umekuja kila kitu kimeharibika hakuna ubuyu wala ukwaju." Dada Noela alichukia na kunitaka niondoke kwani alikuwa hajaambulia chochote toka niingie mle jikoni.
" Nani atoke? Hatoki mtu humu ndani." Nilimjibu.
"Na kama hautoki humu utabaki kwa masharti yangu na kama usipoyafuata nitakwenda kumweleza mama kuwa umetoka chumbani." Aliamua kunitisha baada ya kuona simpi nafasi ya kuyasikiliza yaliyokuwa yakizungumzwa pale sebuleni.
"Usinitishe hapa bwana shida yako si umbea haya nitakaa kimya usije nifia bure maana kuna rafiki yangu aliwahi kuniambia kuwa mbea akikosa umbea anaweza kufa kwa alosto ni kweli?" Nilimuuliza swali ambalo lilimfanya anitolee mimacho.
"Hivi una nini wewe mbona huelewi nilikuwa nimeanza kufaidi uhondo umenikatisha tayari. Yaani unakera kama nini Tina." Aliongea kwa hasira kisha akaufungua mlango na kutoka zake nje. Lakini mara nikamsikia Bi Matilda akimwita dada Noela.
"We Noela hebu tuitie Christina huko chumbani kwake." Mmh niliposikia hivyo ikabidi nitoke haraka ili asije inuka na kunikuta jikoni bure maana mama Fabiana naye mtata kweli kweli usipokwenda sawa na maelezo yake.
"Si jeuri unakimbia nini sasa muone hebu nenda huko najua umesikia kila kitu." Niliishiwa pozi ikabidi niongoze sebuleni na kumuacha dada akielekea jikoni na baada ya kufika sebuleni nilikutana na sura tano zote macho yakiwa kwangu mpaka nikajisikia vibaya lakini nifanye nini nikaongoza mpaka karibu na mama yangu na kuketi.
" Mwanangu Tina mbele yako kuna sura ngeni mbili ambazo zimekuja na jambo ambalo utatakiwa kulisikiliza kama sisi tulivyowasikiliza." Mama Fabiana aliniambia nikiketi.
"Itabidi uwasikilize kwa umakini zaidi kisha utajua ufanye nini japo sisi kama wazazi wako tuna tamko pia." Baba naye aliongeza kisha akatoa ishara ya kuwaruhusu waongee kilichowaleta na mimi nikiwepo.
"Asante kwa nafasi hii, samahani Christina kwa yote yaliyotokea mwaka mmoja uliopita kati yako na mdogo wetu Meshack kiasi cha kupelekea kufukuzwa shule na siku ile mimi mwenyewe nilikuwepo mkifukuzwa......." Wakati akiendelea na mahubiri yake baba alimkatisha.
" You boy! What are you talking to my daughter? Please nenda kwenye pointi yako hayo mengine hayana maana hapa, sijui tumeelewana?" Maneno ya baba yalimfanya kaka yake Meshack ashushe pumzi kwanza kabla ya kuendelea.
"Nisamehe mzee wangu na ngoja niende kwenye pointi moja kwa moja, Tina tumekuja hapa kuyaweka sawa haya matatizo baina yako na Meshack ili ikiwezekana huko mbeleni muweze kumlea mwanenu pamoja." Maneno yale yalinitia hasira nikajikuta natamani nimrukie mzima mzima lakini ndiyo hivyo simuwezi. Lakini sikutaka ipite hivi hivi hivyo nikamtolea uvivu mbele ya wazazi wangu.
" Leo ndiyo umeuona umuhimu wangu? Au unafikiri nimekusahau wewe si ndiye uliyetutimulia vumbi pale getini mimi na wazazi wangu huku ukiwa umempakia mdogo wako na kama haitoshi bado mlirudi kutoa rushwa ili kijana wenu arudi kumalizia masomo yake na kwa hilo mlifanikiwa, vipi kuhusu mimi mliwahi kujiuliza kuwa toka nimefukuzwa shule naishije mimi na mwanangu? Au labda nikuulize swali unayejiita shemeji yangu. Unajua nilifikaje hapa? Kaka hunijui vizuri lakini elewa kuwa mimi bado mdogo sana ila huyo mdogo wako kanikuza na kuikomaza akili yangu na kupitia yeye nimeyafahamu maisha, hivyo kwa hilo tu inatosha sihitaji jambo jingine lolote kutoka kwenu labda kama mtakubaliana na wazazi wangu ila siyo mimi. Mtaniacha mimi na mwanangu na maisha yangu hivyo nawaomba mkae mbali nami." Nilipomaliza kuyatoa yale moyoni mwanangu machozi yakinitoka niliinuka na kuelekea chumbani.
Dakika chache mama naye alinifuata chumbani na kunikuta nikiyamwaga machozi mtoto akiwa mkononi mwangu.
"Mama naomba uniache peke yangu tafadhali sihitaji maongezi ya aina yoyote ile kwa sasa." Nilikwambia mama nikiwa simtazami usoni macho yakiwa kwa mtoto wangu.
"Sijaijia hayo mwanangu naomba unisikilize kwanza kilichonileta kisha utoe maamuzi mwenyewe, sawa mwanangu?" Mama aliniambia huku akiketi karibu yangu.
"Najua bado una hasira na familia ile lakini mwanangu kumbuka kuwa ndiyo familia ya Thobias hiyo hata kama wewe na sisi hatuwataki." Aliendelea kunisihi juu ya yale niliyafanya pale sebuleni.
"Hata kama mama lakini msimamo wangu hauji badilika labda nitakapokuwa nimekufa ndiyo watamchukua mtoto wao lakini nikiwa mzima thubutu hakuna kitu kama hicho mama." Nilimjibu mama huku nikitaka kuinuka.
"Sasa unaelekea wapi? Hebu kaa hapa kwanza." Alinishika mkono.
"Wewe ni mwanangu hivyo kumbuka kuwa pamoja na yote yaliyotokea lakini hatuko tayari kuyashuhudia machozi yako mengine yakitiririka kisa tu wajinga wale hapana mwanangu adhabu hii ya kuishi ugenini imetosha hatuko tayari litokee jingine hivyo hata sisi tumewaambia hivyo hivyo kuwa waondoke wakajipange kwa jingine lakini si kwa hili." Maneno ya mama yalinipa nguvu na kuona kuwa kumbe wazazi wangu nao wako upande wangu kwa hilo nilifurahi sana.
" Mama ni kweli au unataka kunifurahisha tu hapa huku nyuma ya pazia mna mambo yenu."
"Aahh mwanangu ina maana hutuamini wazazi wako?" Aliniuliza huku akimchukua mwanangu.
"Nawaamini sana wazazi wangu lakini kuna hofu iliniingia baada ya hao wageni wenu kuja......." Kabla hajamalizia kuongea mara mlango ulisukumwa kwani mama hakuufunga vizuri hivyo mama Fabiana akaingia ndani kwa urahisi.
"Mwanangu mwenyewe huyo, yaani Tina kwa leo umenifurahisha sana kwa ulichokiongea pale sebuleni kwani hata baba yako amewashindilia maneno bombom kiasi cha kujikuta hawana la kujitetea, unajua kilichotokea?" Aliniuliza swali baada ya maelezo yake.
"Sijui kuna kwani au wamemshambulia baba yangu?" Nilimjibu.
"Walaa wanaweza kufanya hivyo mbele ya mzee Thobias? Amewafurumshia huko, hivi ninavyoongea wameshaondoka tayari hebu inukeni tukale chakula bwana." Mama Fabiana alitueleza huku akimfuata mama ili amchukue mtoto.
JE NINI KITAENDELEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI.
#SULTANUWEZO