NITAKUUA MWENYEWE - 94
sultanuwezotz.blogspot.com
Muda ulipita bila Madam Nafiwe kurudi toka alipotoka kwenda kuwaangalia Jasmine na Titiana kama wamezinduka baada ya kupokea kipigo kikali kutoka kwao, ikabidi Santana amwambie Robinson akaangalie nini kimetokea huko kwani hata namba yake ya simu ilikuwa ikiita tu bila kupokewa.
Robinson aliondoka na kuelekea kwenye chumba ambacho waliwahifadhi mateka wao lakini alibaki mdomo wazi baada ya kukuta chumba kiko wazi na ndani hakuna mtu si Jasmine wala Titiana na hata Nafiwe mwenyewe hakuwepo. Alitoka na kumfuata Santana jasho likimtoka na halikuwa jasho la kawaida bali la hofu juu ya kilichotokea.
"Bosi tumechezewa mchezo na Nafiwe."
Robinson alimwambia bosi wake Santana.
"Tumechezewa mchezo? Una maanisha nini Robinson kusema hivyo?"
Santana alitoa sigara yake mdomoni na kumuuliza Robinson anamaanisha nini kusema wamechezewa mchezo.
"Unauliza? Twende ukajionee mwenyewe nisije ongeza chumvi bure ukanigeuza bucha."
Robinson alimjibu huku akimshika mkono kutoka naye nje mpaka kwenye kile chumba ili akajionee mwenyewe.
"Haaa nini kimetokea Robinson? Unajua msijaribu kunichanganya mimi ni chizi kitambo ohooo..."
Santana alishangaa baada ya kukuta chumba kitupu hakina mtu yeyote yule.
"Na ndiyo maana nikakwambia tumechezewa mchezo na Nafiwe, kama si yeye yuko wapi sasa?"
Robinson alimuuliza maswali ambayo inawezekana Santana hakuyahitaji zaidi ya majibu.
"Hebu ngoja kwanza Nafiwe anawezaje kunifanyia kitu cha kishenzi kama hiki?"
Santana alichanganyikiwa kitambaa kikiwa mkononi kufuta jasho ambalo sijui lilitoka wapi kwani muda huo kulikuwa na baridi kali,ikabidi atoke nje kwanza kuangalia chochote kile kinachoweza kumsaidia kubaini waliko watu wake. Hakuweza kuamini alichokutana nacho nje ya jengo lile miili kadhaa ya walinzi walikuwa wameuawa.
"Ahaa ina maana huyu Nafiwe ni mshenzi kiasi hiki? Haiwezekani hata kidogo mimi ndiyo Santana kiboko yao nitamuonesha."
Akiwa ameshika kichwa chake alijisemea maneno hayo huku akishuhudiwa na Robinson.
"Bosi hivi waliohusika na huu mchezo hawawezi kuwa wakina Jackline kweli?"
Robinson alimuuliza huku akimfuata nyuma kwani Santana hakuona sababu ya kuingia ndani ikabidi awafuate walinzi wa geti kuu la kuingilia mle ndani.
"Ngoja kwanza niwafuate walinzi kule geti kuu watanieleza ni nani aliyefanya hivi."
Walitembea haraka kulifuata lango kuu ambalo lilikuwa na walinzi wa kutosha.
"Hee hiki si ni kiini macho kweli? Wako wapi hawa mbona geti liko tupu?"
Santana aliuliza baada ya kukuta geti halina mtu na mlango mdogo wa pembeni uko wazi.
"Nafiwe kafanya yake bosi hapa hakuna cha kuendelea kujadili zaidi ya kumtafuta popote pale alipo."
Robinson aliyekuwa na uhakika kuwa Nafiwe ndiye mhusika wa kuwatorosha wakina Jasmine aliongea kwa kujiamini huku akilifuata gari lao walikokuwa wamelipaki.
" Nitakula nyama ya mtu ikiwa mbichi iwapo nitamkamata huyu mwanaharamu."
Santana aliongea akifunga mkanda wake huku Robinson akiwa nyuma ya usukani tayari kwa safari ya kuanza kumsaka Madam Nafiwe.
"Tunaanzia wapi mkuu?"
"Breki ya kwanza iwe nyumbani kwake kwanza japo sina uhakika kwani kwa alilolifanya hawezi kuwa kwake lakini tuanzie huko."
"Sawa mkuu."
Robinson alimjibu na kukanyaga mafuta kutoka mle bandarini. Wakiwa nje ya lango hilo simu ya Santana iliita akaichukua na kuangalia mpigaji ni nani alipombaini akapokea.
"Haloo Santana."
"Umeona unifanyie Umafia baada ya kulisikia dili la Wahindi siyo?"
Santana aliuliza kwa ghadhabu baada ya kuisikia sauti ya Nafiwe.
"Ulijua wewe ni mjanja baada ya kuyafanya uliyofanyia siyo? Sasa nakuahidi kuwa wewe na huyo mshenzi wako uliyebaki naye muda wenu umefika tayari."
Jackline aliichukua simu ambayo alimuwekea Nafiwe aongee na Santana.
"Mwanaharamu wewe usiye na kwenu kumbe ndiye uliyenichezea kauntataki hii?"
"Usiulize kuhusu hilo jiulize nikikukamata nitakuuaje? Kwani mpaka sasa uko kiganjani kwangu pamoja na huyo nyangarika mpenda kifo."
"Unajidanganya Jackline huwezi kufanya unachokifikiria kwani nitakuangamiza kabla ya kutekeleza ulichokipanga kwetu."
"Vizuri sana Santana, unajua nini mimi siku zote hupenda kucheza michezo kama hii na adui anayejiamini kama wewe, na kama uko tayari kwa hilo niambie tuuanze huu mchezo sasa hivi."
Jackline aliendelea kumchimba mkwara Santana ambaye muda huo alikuwa katota kwa jasho kwani hakutegemea kama aliyewatorosha mateka wake anaweza kuwa Jackline.
" Mshenzi huyu atanitambua, hawezi kucheza na akili yangu namna hii."
Santana alikuwa akijiwazia hayo kabla ya kumjibu Jackline aliyekuwa hewani akisubiria jibu.
"Mbona kimya Kamanda? Au ndiyo ule msemo wa kiswahili usemao kuwa 'ukiona kimya pigia mstari' na mimi nifanye hivyo?"
Jackline alimtupia swali jingine baada ya kuona kimya.
"Jackline ninakuapia haki ya mama yangu mzazi aliyelala pale makaburini Brazil nitakuua."
"Maneno ya mfa maji hayo huna lolote lile unaloweza kulifanya, hivi kati yangu na wewe ni nani awezaye kummaliza mwenzake?"
"Mimi ndiyo nitakayekuua kabla yako."
Santana alimjibu huku akimuashiria Robinson apunguze mwendo.
"Mimi ndiye niliyekuwa na nafasi ya kukuangamiza lakini niliona niwaache mvute hewa ya mwisho mwisho na ikiwezekana muwapigie simu ndugu zenu kuwaaga na kuwaambia kuwa muda si mrefu bara la Afrika linakwenda kuwameza."
"Kelele wewe unazungumza hayo kwa mamlaka ya nani?"
Santana aliona aongee kiume baada ya kuona sauti ya kike inataka kumpanda kichwani.
"Hapo ulipo unaweza kuangalia nyuma ukipenda lakini."
Jackline aliongea hayo na kumkatia simu,na hapo Santana aligeuka nyuma kuangalia kuna nini alichoambiwa na Jackline akiangalie.
"Mwanahizaya huyu kuna nini sasa mbona sioni chochote huko nyuma? Hebu paki gari pembeni tuone kuna nini."
Walitelemka baada ya kupaki gari na kurudi nyuma kuyakagua maeneo yote kama aliambiwa kwenye simu lakini hakuna walichokiona.
"Unajua huyu mwanamke anaendelea kunipandisha hasira zangu atajuta kuingia anga zangu."
Santana aliongea hayo baada ya kutokuona chochote kile eneo lile ikabidi wageuze kurudi kwenye gari kuendelea na safari lakini hawakuamini kilichotokea mbele ya macho yao, gari liliondolewa kwa kasi ya ajabu na kuwaachia vumbi pale walipokuwa.
" Bosi mbona gari linaondoka?"
"Kweli tunachezewa akili zetu na huyu Mwanaharamu yaani atushushe kwenye gari kisha yeye aondoke nalo?"
"Kinachonishangaza kafanyaje wakati funguo ninayo hapa?"
Robinson alimuonesha funguo ile ya gari Santana huku akilishuhudia gari likipotea mbele ya upeo wa macho yao.
"Yaani wewe kweli bado sana kwenye fani hii unauliza funguo? Watu wana taaluma zao hebu tufanye utaratibu wa kuwafukuzia."
Santana alimshangaa Robinson baada ya kuuliza wamefanyaje ilhali funguo anayo yeye.
"Umeona sasa namna ninavyoweza kuwasambaza kama upepo wa kimbunga? Nakuangamiza kidogo kidogo nimeanza na watu wako wa karibu, nimechukua gari lililokuwa linakupa jeuri mpaka kufika kwa mwenyekiti na kufanya naye umafia ule lakini napenda kukujulisha kuwa naye pamoja na mke wake wako kukuandalia makao yenu wewe na Robinson."
Ilikuwa ni simu kutoka kwa Jackline moja kwa moja.
" Hivi we..... "
Kabla hajamaliza kuongea simu ilikatwa.
"Shabash, nitakukamata tu hata kwa kuchelewa lakini lazima iwe hivyo haiwezekani Santana nionekane hayawani nisiye na dhamani mbele ya waonao."
Aliongea hayo na kuchomoa sigara mfukoni na kuiwasha huku nyuma Robinson akiwa kavua na koti lake japo ilikuwa ni baridi.
***
" Pole sana Jasmine Mungu bado ni mwema anakupigania."
Daktari Abbas aliongea baada ya kumpatia huduma Jasmine alipofikishwa na pale hospitali na Jessica akiwa sambamba na Roberto ambaye muda huo alikuwa hatuii mlangoni kusubiri ni taarifa gani atakayoambiwa kwenye oparesheni inayoendelea kwa mpenzi wake Titiana ambaye hali yake ni mbaya sana.
"Ninakushukuru sana daktari Abbas kwa kujitolea kutupigania."
"Usijali nilijitolea kwenu kwa hiyo bado nina deni ambalo litakamilika baada ya maadui zenu kusalimu amri."
Daktari Abbas alimtia moyo Jasmine aliyekuwa katika tabasamu kubwa baada ya kupata matibabu.
"Kwa uweza wake Mungu tutaishinda hii vita ikiwa nilipoteza matumaini ya kuishi tena baada ya kutekwa na kuteswa lakini Jackline alitokea na kutusaidia."
"Mungu awasimamie muishinde hii vita mapema."
Daktari Abbas aliongea hayo na kumuomba apumzike kisha alitoka nje kuendelea na majukumu mengine.
Jessica aliendelea kumliwaza mzee Jerome Whistle ambaye giza zito la huzuni lilitanda mbele yake mara baada ya kuwapoteza watoto wake wote Victor na Mustapha ambao muda huo walikuwa wamehifadhiwa Mochwari wakisubiri kuhidhiwa kaburini.
"Binti yangu, wanangu wameniacha peke yangu nitaishi vipi mimi bila wao?"
Mzee Jerome aliendelea kuomboleza huku machozi yakimtiririka machoni.
"Mzee Jerome jipe moyo utayashinda haya yote yanayokutokea kipindi hiki kumbuka kila jambo hutokea kwa sababu chini ya jua."
Daktari Abbas alimwambia mzee Jerome baada ya kumkuta akiomboleza mbele ya Jessica aliyekuwa akimpa sapoti kwenye kutembea.
"Eee Mungu wangu nisimamie katika hili jaribu niweze kulishinda, nakuomba ukaniepushe na fikra mbaya juu ya vifo vya watoto wangu."
Mzee Jerome aliendelea kusali kimya kimya huku machozi yakiendelea kumwagika.
"Mzee Jerome naomba urudi wodini muda wa mazoezi umeisha."
Alifika Nesi na kumtaka mzee Jerome kurejea ndani maana muda ambao alipewa kufanya mazoezi umeisha. Jessica alimuongoza mzee Jerome kuingia wodini, alimkongoja taratibu mpaka wodini na kumpa sapoti kupanda kitandani.
" Jessica mwanangu hali yangu kwa sasa si mbaya sana nikiamka salama kesho au keshokutwa niwazike wanangu."
"Sawa baba tutalifanyia kazi hilo naomba upumzike sasa."
Jessica alimuomba apumzike ili kuupa nguvu mwili ambao bado haujawa sawa. Na wakati huo huo Roberto aliingia mule wodini.
ROBERTO ANA TAARIFA GANI?
JACKLINE ATAFANIKIWA KUWANASA WAKINA SANTANA? KAA TAYARI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO