NITAKUUA MWENYEWE - 93
sultanuwezotz.blogspot.com
Baada ya kuangalia vizuri ni kweli kulikuwa na kivuli cha mtu upande wa nyuma wa gari hilo hivyo haraka sana waliondoka eneo hilo na kwenda kujificha kando kidogo ili kuweza kumuangalia mtu huyo anafanya nini hapo kwenye gari lao. Walijibana pale kwa muda lakini mtu yule aliendelea kukaa pale na pia hawakujua wafanye nini kwa mtu huyo.
"Mimi nina wazo jamani."
Jessica aliwaambia wenzake.
"Wazo gani hilo?"
Jackline alimuuliza Jessica juu ya kile alichokifikiria.
"Mnaonaje kama mmoja wetu akienda pale kwa staili ya kuviringika mpaka pale na kuingia uvunguni mwa gari na kumshambulia kutoka uvunguni kwani mpaka sasa hajaweza hajatuona kwani ingekuwa hivyo lazima angechukua hatua juu yetu."
Wazo lile la Jessica lilipitishwa bila pingamizi na haraka sana Roberto hakutaka kusubiri uchaguzi ufanywe nani aende yeye akajitosa kuelekea kwenye gari kwa staili ya kuviringika kama gurudumu. Baada ya kufika alijitosa uvunguni mwa gari na kutokea pale alipokuwa kasimama mtu yule ambaye hakufahamika ni nani na anasubiri nini pale.
Alipomfikia alimpiga mtama maridhawa uliompeleka chini yule mtu na kumfanya Roberto kumkalia juu yake bastola ikiwa kwenye paji la uso.
"Niambie wewe ni nani na umefuata nini hapa?"
"Wewe ni nani?"
"Nimekuuliza wewe ni nani na umefuata nini hapa sihitaji maswali bali majibu."
Roberto alimuuliza huku akiisugua bastola kwenye paji la uso wa yule mtu.
"Samahani kaka mimi naitwa Mahmoud ni dereva Taxi niliyekuwa nimemleta ndugu yenu pale hospitali."
"Dereva Taxi? Sasa umefuata nini hapa muda huu?"
Roberto alimuuliza swali baada ya kujua mtu huyo ni dereva Taxi ambaye alimbeba Jackline mchana.
"Toka nilipoachana naye sikutaka kumuacha peke yake kwani hakuwa sawa hivyo niliamua kumfuatilia nyuma kwa kila hatua yake mpaka anakwenda kumuua mzee yule kule bondeni ambaye ni kiongozi wa eneo lile nilikuwepo na sasa huku."
"Kwa hiyo wewe unatuchunguza sisi siyo?"
Roberto alimuuliza huku akimsindikiza na ngumi ya kichwani.
"Kaka hujui tu ndiyo maana unanipiga hivi."
"Roberto tunakwenda na muda mnaongea nini na huyo?"
Jackline alimkumbusha Roberto wakiwa wameshafika pale.
"Huyu ni yule dereva Taxi uliyekuwa naye mchana."
"Dereva Taxi? Kafuata nini huku au naye ni Kibaraka wa Santana?"
Jackline aliuliza.
"Tulipoachana muda ule niliondoka zangu lakini sikufika mbali nikawa nimekutana na Daktari Abbas akanisimamisha na kunipa kazi ya kukufuatilia kwa lengo la kukulinda bila wewe kujua hivyo niligeuza gari na kurudi mpaka pale nilipokuacha ndipo ulitoka na kuelekea kwa yule kiongozi nikiwa nyuma yako mpaka unafika na kufanya mauaji yale mimi nilikuwa dirishani kifupi ni hivyo tu na kule mlikokuwa mmeingia kulikuwa na walinzi wawili ambao walijificha mlipoingia tu walianza kuwavizia mimi nilicheza nao na kuwavutia pembeni bila ninyi kuona, na hapa ikawa hivyo hivyo njooni muone."
Alipoinuka huku akiwasimulia aliwaita kuwaelekea gizani ambako huko aliwaonesha miili ya watu watatu aliowaua.
" Hawa walikuwa nje ya geti mlipoingia ndani waliwasubiri hapa nje mkitoka tu wawashambulie lakini niliwamaliza."
"Mbona hatukusikia mlio wa risasi yoyote?"
Roberto alimuuliza.
"Bastola yangu ina kiwambo cha sauti hivyo huwezi sikia sauti."
Maelezo ya dereva Taxi yule yaliwachanganya kiasi cha kuwa na mashaka naye.
"Unatuchanganya Mahmoud kwa hiyo wewe ni dereva Taxi au nani? Tupe utambulisho wako."
Jackline alimuuliza.
"Mtanijua tu baadaye siyo sasa, mnaweza kuendelea na misheni yenu mimi nitakuwa nyuma yenu nikitekeleza wajibu wangu kwenu kama niliagizwa na bosi Abbas."
Hakuwa tayari kuwaeleza yeye ni nani kwa wakati huo na aliwaahidi kuwa watamfahamu hapo baadaye.
"Okay sawa."
Jackline alimjibu.
Waliondoka na kuelekea bandarini kwa ajili ya kumwagiwa Santana na watu wake. Kwa kuwa hapakuwa mbali waliweza kufika karibu na bandari hiyo ya Namport na kusimamisha gari.
"Jamani ndiyo tumefika eneo la mapambano si eneo zuri kwani linamilikiwa na serikali hivyo tukifanya kosa tunakamatwa na kama ambavyo niliwahi ambiwa huko nyuma wakati naichunguza hii bandari ni moja maeneo yanayolindwa sana serikali hivyo basi huko ndani tutaingia kwa staili ya panya hii staili ya kupenya popote pale hata pawe na ulinzi kiasi gani na tulifika huko ndani hatuwezi kutumia bastola zetu tutatumia visu tu."
Jackline alitoa maelezo.
" Sasa kama kuna ulinzi mkali tutapenyaje kuingia ndani?"
Jessica aliuliza.
" Kuhusu kuingia wala msijali nilishawahi fanya uchunguzi kwa kumtumia mfanyakazi wa humu ndani, kuna chemba moja ambayo tutaitumia hiyo kuingia ndani ni njia majitaka."
"Santana atakuwa alipitia wapi kuingia huko ndani?"
"Jamani tunapoteza muda andaeni vitendea kazi tuanze zoezi la kuingia ndani."
Walijiandaa wakashuka kwenye gari na kuanza kuufuata uchochoro ambao ulikuwa na hiyo chemba ya majitaka. Walifika kwenye hiyo chemba Jackline akatoa mfuniko na kuanza kuingia ndani, Roberto alikuwa wa mwisho hivyo akaurusha mfuniko kwa staili ya kuuweka kichwani kwake alivyoshuka chini wenyewe ulibaki sehemu yake huko chini ilikuwa ni visu mkononi. Walitembea na kutokea ndani sehemu ambayo ilikuwa ni kama barabara ya viberenge ya kupitishia mitambo na bidhaa mbalimbali kutoka kwenye Meli.
"Hapa tulipo kabla hatujaonwa tufichame sehemu tulivu ambayo hawawezi kutuona Jessica utaitraki namba ya Santana au ya Nafiwe tujue wako upande gani?"
"Sawa lakini hapa nina namba ya Santana tu."
"Siyo mbaya anza na hiyo asipoonekana nitakupa namba ya Nafiwe."
Jessica aliitoa simu yake na kuiingiza namba ya Santana kwenye mfumo na kama bahati ilikuwa hewani, walipoangalia vizuri umbali wakifurahi sana kwani wahusika hawakuwa mbali na pale walipo hivyo walianza kunyata kuufuata ukuta wa lile jengo. Na mwisho iliwaonesha sehemu walipo kwa usahihi na ndipo Jessica alipoizima simu huku Roberto akifanya kazi ya kuchungulia kila dirisha la chumba walichokuwa wanakifikia.
"Wanasema tuendelee kuwepo hapa kwani Meli hiyo itaondoka hapa mnamo saa nane usiku kwani bado wanamalizia kupakia mzigo."
"Ina maana tunaondoka na Meli ya mizigo?"
"Unataka tuondoke na boti ili tudakwe? Meli ya mizigo inahusika na uzuri wa hii Meli ni ya Kampuni ya jamaa yangu hivyo usalama ni asilimia mia moja."
Maongezi yale kutoka ndani ya chumba kimoja waliweza kuyasikia yaliyokuwa kati ya Santana na Nafiwe wakiwa na uhakika zoezi lilikuwa limekamilika kwa asilimia zote.
" Tunafanyaje hapa kuwavamia Jackline?"
Jessica aliuliza.
" Hapa tulipo ni moja ya mafanikio yetu hatuna haja ya kuwa na haraka, hapa kazi tunayoianza ni kuanza kuua mlinzi mmoja baada ya mwingine mpaka tuwafikie."
"Sawa sawa tuanzeni sasa."
Roberto aliwaharakisha wenzake, hivyo walianza kuwanyatia walinzi waliokuwa wanalinda jengo ambalo ndani yake ndiyo walikuwamo wakina Jasmine. Wakiwa wanaendelea kuvichunguza vyumba vile kupitia madirishani mara walikifikia chumba ambacho hicho waliweza kusikia watu wakiongea kwa taabu sana.
"Na..na..naom...ba wai...waite wani...ue nime....choka kwa mateso."
Sauti hiyo ilikuwa ni ya Titiana ikiongea kwa shida kwa ilivyoonesha walikuwa wameteswa sana mpaka kufikia hatua ya kukata tamaa. Kitendo hicho kiliamsha hasira za Roberto na kujikuta akiligonga dirisha lile ili waweze kusikia, na kweli walisikia kwani Jasmine aliyekuwa kafungwa kamba za kutosha kwenye kiti cha chuma aliweza kugeuka kutazama dirishani.
"Tumekuja kuwaokoa ndugu zetu msikate tamaa."
Jackline aliongea kwa sauti ya kunong'ona lakini iliyosikika mle ndani.
"Naomba sigara yako niwashe yangu."
Roberto aliambiwa na mlinzi aliyefika kuomba kuwasha sigara baada ya kumuona Roberto akivuta sigara akajua ni mlinzi mwenzake, Roberto aligeuka kumpa mkono wenye sigara kitendo cha kupokea ile sigara alimdaka na kumvutia kwake na kumpiga kichwa kilichomfanya apepesuke na kabla hajafanya chochote alimuwahi na kumkita kisu cha kifuani kisha kumvutia gizani na kusonga mbele. Visu viliendelea kutembea mle ndani mpaka alipoukaribia mlango wa kile chumba lakini akiwa anataka kugusa kitasa cha mlango huo mara mlango wa chumba cha pili ulifunguliwa haraka sana alikimbia na kujificha. Alimchungulia aliyetoka ni nani japo lilikuwa ni giza aliweza kumfahamu kutokana na mwanga wa simu ambayo mtu huyo alikuwa akiiangalia.
"Shiiiit si Nafiwe huyu?"
Roberto alijiuliza baada ya kumuona vizuri.
"Nakula naye sahani moja huyu kabla hajazima simu yake."
Alimfuata na nyuma nyuma mpaka alipoufungua mlango wa chumba cha wakina Jasmine huku ule mwanga wa simu ukimpa msaada kutokana na giza lililokuwa sehemu ile. Alipofungua tu mlango kabla hajafanya chochote Roberto alimfuata na kumuwekea bastola kichwani kwake.
"Nafiwe kuwa mpole tofauti na hapo ubongo wako halali yangu, naiomba simu yako."
Nafiwe hakuwa na jinsi alimkabidhi ile simu na kuweka mikono juu.
"Ingia ndani haraka."
Madam Nafiwe aliingia ndani ya kile chumba Roberto naye akafuata na kuufunga mlango kwa ndani.
Humo hakutaka kuchelewa aliona amlegeze kwanza ili asipate jeuri kuleta jeuri yake hivyo Roberto alianza kumshushia kichapo hasa baada ya kumuona mpenzi wake akiwa kwenye hali ile.
"Niko tayari kufanya chochote kile lakini usiniue."
Kichapo kilipokolea alianza kuomba msaada kutoka kwa Roberto ambaye muda huo hakuwa akiongea chochote zaidi ya kutoa kamba mfukoni na kuanza kumfunga Nafiwe karibu kabisa na Jasmine.
"Wala usihofu huwezi kufa saizi muda wako bado haujafika."
Alimjibu huku akiinuka na kumfuata Titiana ambaye muda huo alikuwa akikoroma tu hali ilikuwa tete.
"Mpenzi wangu usiniache nimefika kukuokoa."
Roberto alimwambia Titiana asimuache muda huo akimfungua kamba alizofungwa na baada ya kumaliza alimfuata Jasmine ambaye hali yake haikuwa mbaya sana zaidi ya maumivu ya bega ambalo lilipigwa tena pamoja na kichwa ambacho alikuwa akilalamika kutokana na kipigo cha kugongeshwa ukutani.
"Nafiwe utalipia na wenzako Ole wenu Titiana afe."
Jasmine alimwambia baada ya kufunguliwa pale. Na baada ya hapo mlango ulifunguliwa na kumtoa nje Titiana kisha wakamfungua kamba Nafiwe kumfunga kitambaa usoni kisha kamba za mikono na kuondoka naye. Zoezi likawa wanafikaje nje kwa kupitia kwenye ile chemba wakiwa na wagonjwa. Hivyo waliamua kumchukua Nafiwe na kutaka ataje njia ya kutokea nje.
"Taja njia ya kutokea nje ambayo ni salama."
Jackline alimuuliza huku akimchoma kisu cha kwenye paja.
"Nitawaambia tu msinifanyie hivyo mwenzenu."
"Nani mwenzako mshenzi wewe usiye na haya onesha njia haraka."
Roberto alimkatisha.
"Fuateni hayo makontena mpaka mwisho mtaikuta barabara hiyo ndiyo muifuate itawatoa nje bila kuonwa na walinzi."
Hapo hapo Roberto akambeba Titiana huku Jackline naye akimchukua Jasmine huku Jessica yeye akisalia nyuma kuangalia usalama.
NINI KINAKWENDA KUTOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
#SULTANUWEZO