NITAKUUA MWENYEWE - 91 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 91

sultanuwezotz.blogspot.com 


Wote waligeuka kumuangalia Mustapha aliyetoka humo chumbani akiwa anavuja damu puani na mdomoni na kutokana na kuvuja damu nyingine alipofika tu sebuleni alianguka chini na kuanza kukoroma. Wote walitazamana kwa kinachoendelea pale, mzee Jerome hakusubiri alimfuata mtoto wake pale chini na kuanza kumtingisha.

"Must.. Must... Mustaphaaaaa amka ulale kama ndugu yako."

Mzee Jerome alipiga kelele na kuanza kulia kwa sauti kubwa. Roberto alikwenda mpaka kwenye kiti kikubwa na kumlaza Victor pale kisha alimfuata mzee Jerome pale chini na kumuondoa, alimuangalia Mustapha kukagua mapigo ya moyo akayasikia kwa mbalii yakifanya kazi hivyo alimbeba na kutoka naye nje huko alikwenda naye moja kwa moja mpaka kwenye gari akampakia kisha akarudi ndani.

"Kwanini tuendelee kujikunyata kiasi hiki kuna kosa limefanyika tayari hatuna budi kuyaokoa maisha ya ambao bado wanapigania uhai wao."

Roberto aliongea hayo baada ya kuona kila mmoja mle ndani kama kapigwa shoti hivi wameduwaa tu, Jackline alikuwa kasimama karibu na dirishani akiangalia nje machozi yalimtoka mpaka yakakata yenyewe. Roberto alimuangalia kwa muda kisha akamfuata pale na kumshika bega lakini cha ajabu naye alikwenda chini na kuzimia, tendo hilo liliwachanganya hasa Roberto ambaye muda huo hakujua atoe msaada kwa nani? Ilibidi atoe simu mfukoni mwa Jackline na kuitafuta namba ya simu ya daktari Abbas wa 'THE KING'S MEDICARE CENTRE na kumpigia.

"Daktari huku mambo si yenyewe nyumba nzima imezima baada ya kuvamiwa na Santana aliyefanya mauaji na kuna wengine hatujui waliko, hivyo kama hutojali naomba gari la wagonjwa."

Roberto aliongea na daktari Abbas baada ya kupokea simu.

"Mmevamiwa na Santana? Mko wapi?"

Taarifa ile ilimshangaza sana daktari Abbas kiasi cha kujikuta akiuliza maswali ambayo hakuwa na uhakika wa kupata majibu kwani wakati anauliza hivyo tayari simu ilikuwa imekatwa. Baada ya kukata simu Roberto aliiweka mfukoni simu ya Jackline na kumbeba akamtoa nje na kumlaza kwenye kiunga ile apigwe upepo kisha alirudi ndani akamkongoja mzee Jerome aliyekuwa kama kachanganyikiwa kwa tukio lililofanyika nyumbani kwake huku Jessica yeye alikuwa hataki kuongea na yeyote mle ndani alikuwa kajikunja tu kwenye kiti.

"Jessica njoo ukae nje sehemu yenye hewa nzuri ili akili ikae sawa."

Roberto alimwambia Jessica huku akijaribu kumwinua pale kitini.

"Hebu niache huko unanipeleka wapi? Unanijua mimi wewe tena usiniguse Roberto."

Maneno yale yalimshangaza sana Roberto hakuamini kama yakitoka mdomoni kwa Jessica ama la.

"Jessica ina maana mi...." Kabla hajaimalizia sentensi yake Jessica alimkatisha.

"Naomba unisikilize kwa umakini mkubwa wewe panya, wewe na huyo mshenzi mwenzio Jackline nitawafanya kitu mbaya asipopatikana dada yangu Jasmine tena nitaua mtu kweupe."

"Lakini siyo sisi tuliofanya haya wewe mwenyewe unalijua hili na ukisema kuhusu Jasmine kumbuka mpenzi wangu mimi mwenyewe sijajua yuko wapi mpaka sasa hivyo ukisema hayo utakuwa unakosea Jessica."

"Narudia tena mimi sina undugu na ninyi hata kidogo ninachokihitaji hapa ni dada yangu na si vinginevyo zaidi zaidi nitaua mtu kwa mkono wangu mwenyewe."

Wakati Jessica akiongea hayo tayari Jackline alikuwa amerejewa na fahamu zake na aliinuka pale na kuja ndani lakini kabla hajakanyaga kizingiti cha mlango alisikia yaliyokuwa yanazungumzwa ndani hivyo ikabidi abane pale kusikiliza kinachoongelewa.

" Naomba tushirikiane pamoja kwani hata mimi najishangaa kwanini nitumikishwa na Jackline kwa manufaa yake? Kwani ukiangalia kama ni mama alishakufa haya mpenzi wangu naye ndiyo kama hivi......" Lakini kabla hajafikia mwisho wa maelezo yake mara kilisikika king'ora nje kuashiria kuwa gari la wagonjwa lilikuwa limeshafika tena hakukuwa moja yalikuwa mawili,haraka sana walitoka nje kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa Madaktari hao waliofika. Jackline alirudi alipokutana kalazwa na kujilaza vile vile kama awali baada ya kusikia kila kitu kilichokuwa kikizungumzwa na Roberto pamoja na Jessica hivyo akaamua atulie.

"Wagonjwa wako wapi Roberto?"

Daktari Abbas aliuliza akiwa anashuka kwenye gari lake binafsi.

"Mmoja yuko kwenye gari lile pale, Jackline yuko pale chini na mzee Jerome yule pale lakini pia ndani kuna mwili wa Victor."

Baada ya kuonesha Madaktari waliwabeba na kuwapakia kwenye magari yale mawili huku daktari Abbas yeye alimfuata Jackline na kumbeba na kumpakia kwenye gari lake.

" Roberto, ninyi njooni mpande huku."

Daktari Abbas aliwaita Roberto, Jessica na mzee Jerome ili wapande kwenye gari lake lakini cha ajabu wote walikataa kupanda gari lile wakapanda gari lao na kuondoka zao kufuatana na gari la wagonjwa. Daktari Abbas aliachana nao na kuingia kwenye gari lake na kuondoka, lakini akiwa anaendesha mara Jackline aliinuka.

"Daktari Abbas pole kwa usumbufu."

Jackline aliongea akikaa vizuri pale kitini kwani alilazwa kiti cha nyuma.

"Jackline umezinduka?"

Daktari Abbas alimuuliza huku akilipaki gari pembeni.

"Nimezinduka muda mrefu sana daktari ila kuna vitu ambavyo wenzangu walikuwa wanaongea vilinishtua kidogo ikanilazimu niigize kulala vile vile."

"Ulisikia nini? Hebu njoo ukae huku mbele."

"Nitakwambia wakati mwingine daktari ila ninachokiomba kutoka kwako ni kutonipeleka hospitali maana sihitaji kuonana nao kwa sasa."

"Sikuelewi Jackline unaongea nini au kichwa hakijakaa vizuri?"

"Hapana niko vizuri kabisa daktari Abbas ila kama hutojali naomba nipelekwe Makambi kwa daktari Hans Murray kikubwa ni kuwa mbali na hawa wenzangu."

"Sawa nimekuelewa, lakini wakitaka kujua nimekuacha wapi nitasemaje?"

"Ni rahisi sana wewe utawaambia kuwa nilizinduka na kutaka kushuka chini kupata haja ndogo ndipo nilipokimbia."

"Mhh sawa kumbe inabidi nikushushe hapa hapa nikukodie gari la kukupeleka huko."

"Sawa nashukuru."

Daktari Abbas alipaki gari pembeni na kumfungulia mlango baada ya kuteremka aliita taxi akampa maelekezo dereva huyo na kisha Jackline akapanda na kuondoka.

Safari iliendelea huku Jackline akiwa katika lindi kubwa la mawazo juu ya alichokisikia kutoka kwenye vinywa vya Jessica na Roberto kijana ambaye alimuamini katika harakati zake za kuipigania haki.

"Ni kweli mimi ndiyo chanzo cha haya yote lakini mbona wakina Jasmine nao waliapa kulipa kisasi kwa Santana pia Roberto aliungana nasi kutokana na historia mbaya iliyosababishwa na Santana kwa familia yake? Kwanini leo hii nionekane mimi ndiyo ninawapelekesha kwa ajili ya manufaa yangu? Siamini kwa kweli, pole sana mzee Jerome kwa familia yako kuingia kwenye matatizo kisa sisi ila nina imani Mungu atafanya jambo kwao na kuondokana na roho za kipepo zilizowaingia."

Alipofika hapo alianza kulia kwa kwikwi kitu kilichomfanya dereva Taxi kusimamisha gari pembeni.

" Dada vipi kuna tatizo?"

" Usihofu kaka yangu wewe tuendelee na safari haya ni masuala yangu binafsi."

"Ni kweli lakini kama hutojali unaweza kuniambia maana kama ni heri usingeanza kulia dada yangu."

"Uko sahihi kaka yangu lakini haya naomba uniachie mwenyewe nashukuru kwa moyo wako wa huruma."

Jackline alimjibu dereva Taxi akaona isiwe tabu akawasha gari na safari ikaendelea huku akiendelea kumuangalia kwa jicho la kuibia kwani Jackline hakuacha kulia.

" Nooo silii tena mzigo ni wa kwangu nitaubeba mwenyewe na si mtu mwingine hapa na kwanini niende mbali nao? Haiwezekani natakiwa nikawaambie ukweli ili mbele yangu waniambie hawako tayari kuendelea nami ili mwisho wa yote nijue la kufanya."

Wazo hili lenye nguvu lilivyotembea kichwani aliona haina haja ya kuendelea na safari hivyo akamuomba dereva Taxi ageuze gari kuelekea 'THE KING'S MEDICARE CENTRE'

" Samahani kaka yangu naomba ugeuze gari turudi tulikotoka."

"Kuna nini dada yangu si yule daktari alisema nikufikishe Makambi hospitali?"

"Ni kweli na mimi ndiye msafiri na nimeona hakuna haja ya kwenda huko natakiwa kurudi."

"Mhhh haya nimekuelewa."

Dereva hakuwa na la kufanya zaidi ya kugeuza gari kama mteja wake alivyoamuru.

"Natakiwa kuwarudisha mikononi mwangu Jasmine na Titiana, na ninaahidi kuwa Robinson nakurudia jiandae na utajuta kuungana na hao panya."

Alisema hayo huku akijifuta machozi yake kwa kiganja cha mkono wake.


****


Walifikishwa hospitali na mara moja matibabu yalianza kwa Mustapha na baba yake huku mwili wa Victor ulipelekwa kuhifadhiwa chumba maalum cha kuhifadhia maiti, Jessica yeye akipewa dawa za kutuliza maumivu ya kichwa.

"Unajisikiaje sasa?"

Daktari Abbas alimuuliza Jessica baada ya kumkuta akiwa anatembeatembea pale koridoni.

Jessica aligeuka kumuangalia daktari Abbas kama vile kuna swali alihitaji kumuuliza.

"Naendelea vizuri daktari vipi Jackline yuko wapi?"

Swali hilo halikumshtua daktari Abbas kwani alilitegemea, hivyo alichokifanya ilikuwa ni kumshika mkono Jessica na kutembea naye kuelekea nje huku Roberto akiwafuata nyuma.

"Hivi Jackline ni mtu wa namna gani?"

"Kwanini unauliza hivyo daktari?"

"Nauliza tu kwani wakati nikiwa naendesha alizinduka na kunitaka nisimame kwanza apate haja ndogo nikafanya hivyo lakini cha ajabu aliposhuka tu aliniambia safiri salama yeye akaanza kurudi tulikotoka."

"Kwa hiyo unataka kuniambia Jackline hujaja naye hapa?"

Jessica alimuuliza daktari Abbas.

"Kama uonavyo ndivyo ilivyo Jessica."

"Ana Mungu wake angetia miguu yake hapa angenitambua walahi."

"Jessica usiongee maneno hayo yaliyojaa laana, wewe ni binti mrembo sana hustahili kabisa maneno hayo, kumbuka kuwa mliamua kwa sauti moja kuungana kuisambaratisha Ngome ya adui yenu mpaka mwisho mkiwa hai au mmekufa,si ndiyo?"

"Ni kweli kabisa daktari."

Jessica alimjibu.

"Vizuri sasa iweje uibue mpasuko katikati ya vita ambayo hamjaimaliza? Najua unateseka na kutekwa kwa dada yako Jasmine pamoja na mpenzi wa Roberto lakini kwa kutengana na Jackline mtafanikiwa kuwakomboa?"

Daktari Abbas alipomaliza kuongea hayo alimgonga mgongoni Jessica na kuachana naye kisha akarejea ofisini kwake kuendelea na majukumu yake.

" Kasemaje daktari? "

Roberto alimuuliza Jessica baada ya kuona wameachana na daktari Abbas.

" Ni juu ya Jackline, inasemekana kuwa kashukia njiani haijulikani kaelekea wapi? Na pia kauliza kuwa mgawanyiko wetu katikati ya uwanja wa mapambano utaleta matokeo mazuri?"

" Kwa hiyo atakuwa kaenda wapi? Au kaamua kuwafuatilia wakina Robinson?"

"Hata sifahamu ndugu yangu ila maneno ya daktari yana kitu ndani yake? Kwanini tumemchukia Jackline ghafla kiasi hicho?"

"Wewe ndiye uliyemchukia mimi aka sijamchukia pale zilikuwa ni hasira baada ya kumuona Mustapha kwenye hali ile huku ndugu yake akiwa kafa."

Wakiwa wanaulizana maswali hayo mara kuna gari ndogo taxi iliingia mle ndani ya Hospitali na wakati wanaishangaa kwa mwendo iliyoingia nao mle mara mlango ulifunguliwa na ndipo walipomuona Jackline akishuka. Baada ya kushuka aliwafuata pale walipo.

" Najua mnionapo chuki yenu imeongezeka mara dufu, lakini niwaombe tu mnisamehe kwa yote mabaya niliyowafanyia mpaka kufikia hatua ya kunichukia kiasi hicho."

Jackline aliongea hayo huku akiwa anafuta machozi ambayo yalisheheni mashavuni na machoni.

"Jackline mbona hatukuelewi katika lipi?"

"Naomba mwenye simu yangu anipe kuna mtu nahitaji kuwasiliana naye."

Roberto aliitoa na kumkabidhi.

"Umesema tukusamehe kwa lipi dada Jackline?"

Roberto alimuuliza swali baada ya lile la Jessica kupotezewa.

"Niliwasikia yote mliyoyaongea muda ule kule nyumbani juu yangu na kweli mlikuwa na kila sababu ya kunitupia zigo la lawama na mimi nina waahidi kuwa nitahakikisha nairejesha furaha yenu."

Jackline aliwajibu huku akiendelea ofisini kwa daktari Abbas na kuwaacha na maswali wakina Jessica ambao waliduwaa baada ya kusikia kuwa aliwasikia ikiwa wao walijua kuwa kazirai. Baada ya muda kidogo alirejea kutoka ofisini kwa daktari Abbas na kuwaaga.

"Dada Jackline unachokifanya siyo kabisa, naomba usiondoke kwanza tulizungumze hili mbona ni suala dogo sana na linazingumzika."

Roberto aliongea huku akimfuata Jackline kwa nyuma huku Jessica akiwa ameduwaa mikono kichwani.

"Roberto narudi sasa hivi tutaongea tu ngoja nikafuate mzigo fulani hivi niliuacha nyumbani kwa mzee Jerome."

Jackline alimwambia Roberto huku akiwa kaufungua mlango tayari kwa kupanda.

"Basi tuongozane wote huko nyumbani."

"Hapana wewe baki tu umpe kampani Jessica."

Alimjibu na kuingia kwenye gari alilokuja nalo na kuondoka zake. Roberto na Jessica walitazamana kama vile kila mmoja alikuwa ana swali kwa mwenzake.

"Hivi ni kweli atakuwa anaelekea nyumbani?"

Jessica alimuuliza Roberto.

"Wewe na mimi hatujui anaelekea wapi tumeyakoroga wenyewe Jessica hasira hasara."

"Ni kweli kabisa Roberto hata sijui itakuwaje siku dada akirudi na kuambiwa kuwa tulifanya ujinga kama huu."

Alikuja daktari aliyekuwa akiwashughulikia wakina Mustapha na baba yake mzee Jerome na kuwapa taarifa kuwa wagonjwa wao wanaendelea vizuri na mzee Jerome keshapata fahamu tayari ila Mustapha atatakiwa kuachwa apumzike mpaka kesho.

" Lakini naye atazinduka daktari?"

Jessica alimuuliza daktari.

"Ndiyo na ataendelea kubakia chumba maalum lakini mzee Jerome mnaweza kwenda kumuona."

Daktari aliwaelekeza na kuachana nao wakielekea kumuona huku naye daktari akielekea ofisini kwa daktari Abbas kupeleka taarifa ya wagonjwa wake.

Jackline alifika nyumbani kwa mzee Jerome akashuka getini na kumshukuru yule dereva Taxi na kuachana naye kisha yeye akaingia ndani ambako alienda mpaka ndani akachukua kila kilicho chake na kupakia kwenye moja ya gari ambayo walichukua kwa yule kijana aliyeuawa na Robinson, lakini kabla hajaondoka alichukua kisu chake pamoja na bastola yake akatoka zake na kuelekea nyumbani kwa mwenyekiti na kwa kuwa alikuwa hapajui aliweza kumuuliza mama mmoja aliyekuwa akiuza maandazi mtaani pale.

"Mwenyekiti wa mtaa wetu anaishi kwenye nyumba ile pale yenye geti la kijivu."

"Nashukuru mama."

Alimshukuru na kuongoza mpaka kwenye nyumba ile aliyoelekezwa na mama muuza maandazi na kugonga geti. Alipoona kimya aligonga tena lakini hali ilivyobaki vile vile aliona apige kengele ambayo ilipelekea mlango mdogo wa geti kufunguliwa.

"Karibu binti pita ndani."

Alikaribishwa na mama mmoja wa makamo ambaye bila shaka alikuwa ni mke wa mwenyekiti.

"Asante mama, mimi si mkaaji ninahitaji kuonana na mwenyekiti."

Alimjibu baada ya kuingia ndani.

"Wewe ni nani? Mbona sura yako ni ngeni machoni pangu."

"Ni kweli lakini hata nikikaa kuanza kukuelezea mimi ni nani huwezi kunifahamu, naomba uniitie mwenyekiti au unahisi na mimi ni mke mwenzako?"

Jackline alimjibu jeuri.

Mama huyo hakujibu kitu zaidi ya kuingia chumbani kwake.


JACKLINE KAFUATA NINI KWA MWENYEKITI?

NA VIPI KUHUSU VITA MPYA BAINA YA JACKLINE NA WENZAKE ITAKUWAJE NA WAKINA JASMINE WATAPATIKANA?


USIKOSE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA KUJUA KILICHOJIRI.


        #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post