NITAKUUA MWENYEWE - 90 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 90

sultanuwezotz.blogspot.com 


Mustapha na Victor wao walipita upande mwingine wa nyumba yao na kumuacha Roberto naye akipita upande wake lengo likiwa ni kuwashtukiza waliokuwa eneo la getini bastola ikiwa mkononi Roberto aliendelea kuambaa na ukuta ule kulisogelea geti kule wakina Mustapha nao wakiwa makini vipande vya nondo mkononi nao waliendelea kusogea mpaka karibu na geti. Cha kushangaza baada ya kufika pale getini hawakuweza kumuona mtu yeyote wala ule mwanga tena kiza kilitanda. Walikagua geti vizuri na kukuta liko salama na kisha pale chini ili kuona kama wanaweza kuona makanyagio ya miguu au viatu au chochote cha kuwasaidia lakini hawakuona kitu.

"Ilikuwa ni nini sasa?"

Akiwa kashikilia kiuno chake Roberto aliwauliza wenzake.

"Maajabu kaka, kwa mwanga kama ule uliashiria kabisa kuna watu wenye nia fulani walikuwa nje ya nyumba sasa iweje?"

Victor alimjibu Roberto baada ya kutoona chochote pale, ndani ya geti Jackline alisogea mpaka karibu ya geti na kuchungulia nje kupitia nafasi za geti na kuwaona wakina Roberto wakiwa wanaongea ndipo naye akaufungua mlango mdogo wa pembeni na kutoka nje akiwa na mzee Jerome pamoja na Jessica.

"Imekuwaje?"

Mzee Jerome aliwauliza baada ya kuwakuta wakiwa wanajadiliana juu ya lililotokea.

"Wala hatuelewi baba hatujakuta mtu yeyote yule hapa."

Mustapha alimjibu huku akijaribu kuangaza maeneo ya jirani kama anaweza kuwang'aza.

"Basi watakuwa wamekimbia na kujificha tu, kwanini watoweke ghafla hivi? Kuna sehemu wapo hawa."

Jackline aliwaambia wenzake kuwa lazima wamejificha sehemu na katika kutaka kulihakikisha hilo alisogea pembeni na kuanza kuchunguza mazingira yale.

"Wakina nani ninyi hapo?"

Ilisikika sauti kutoka gizani ambayo iliongea kwa kujiamini sana.

Walikaa kimya kumsikilizia aliyewauliza swali hilo, na kwa kuwa Jessica alikuwa na tochi alimulika kule lilikotoka swali.

"Mbona mnanimulika pasipo kujibu swali langu?"

Aliuliza swali tena baada ya kumulikwa mwanga usoni, ule mwanga ulimfanya mzee Jerome kumtambua mtu yule na hakuwa peke yake alikuwa kaongozana na vijana wengine kama watano hivi.

"Mzee mwenzangu kwema kweli? Umenishtua sana unajua."

"Ni mzee Jerome?"

"Ndiye mwenyekiti karibu."

"Asante mzee Jerome, unajua nini tulikuja hapa kutaka kukujulisha kuwa usiku wa leo unatakiwa kutupa msaada kwenye ulinzi wa mtaa wetu kwani mzee mwenzetu Changalawe kapata tatizo la msiba huko kijijini leo ni siku ya tano lakini tulivyoona kengele haitupi mrejesho tukaona tuondoke zetu."

"Pole sana mwenyekiti mwanga tumeuona tukahisi labda ni Majambazi wametuvamia tena si unakumbuka walionivamia siku ngapi hizi."

"Nakumbuka vizuri sana mzee Jerome sasa hapo sijui tufanyaje?"

Mwenyekiti alimuuliza mzee Jerome juu ya suala la Ulinzi.

"Kwanza nikupe pole kwa msiba wa bwana Changalawe lakini pia kwa leo nitaungana nanyi kwenye zoezi hili la Ulinzi kwani nina ugeni hapa ndani lakini pamoja na ugonjwa hivyo niombe mimi nitafanya hivyo tu kwenye zamu yangu na kingine kabla sijasahau mwenyekiti waambie vijana kuwa hata huku ulinzi ni muhimu vile vile siyo wawe kule kwenye mataa kwani kuwa na silaha siyo ulinzi umoja wetu ndiyo silaha si ulishuhudia mwenyewe nilichofanyiwa siku ile laiti kama ulinzi ungekuwa kwenye maeneo yote ingekuwa vile?"

Mzee Jerome alimfafanulia mwenyekiti wa eneo lile kile kilicho moyoni mwake.

" Mzee mwenzangu nimekuelewa katika hilo na ndiyo maana nimewapa utaratibu mpya ambao utaanza kufanya kazi wiki ijayo kwa kipindi hiki nilishawaelekeza maeneo yanayotakiwa kushughulikiwa kiulinzi."

"Iwe hivyo mwenyekiti si unajua tena dunia hii si kama ile ya wakati wetu."

"Ni kweli kabisa, kumbe mzee Jerome mimi nimekuelewa wacha sisi tuendelee na kibarua hiki ambacho natakiwa kuichukua nafasi hii ya bwana Changalawe."

Wakashikana mikono kuagana lakini Jackline aliwasogelea na kutaka kuongea na mwenyekiti.

"Samahani mwenyekiti mimi ninaweza kusaidia ulinzi lakini ngoja kuna mambo fulani hivi nayakamilisha yakiwa tayari nitaungana nanyi."

Jackline aliongea na mwenyekiti huku akimshikisha hela mkononi kitu kilichomfanya mwenyekiti kufurahi sana.

"Binti wala usijali sana sisi tuko kamili lakini pia huku sisi suala la Ulinzi halifanywi na wanawake."

Alimjibu huku akitupia hela ile mfukoni mwake.

"Basi tunashukuru na tuwatakie majukumu mema."

Jackline aliwatakia kazi njema huku wao wakiingia ndani na kufunga geti.

"Yaani nilikuwa nina mzuka wangekuwa ni wale panya ningewachezesha Samba ambalo wasingelisahau aslani."

Victor alijigamba huku akimpigapiga Mustapha mgongoni.

"Taratibu sasa mgongo wa mtu huo."

Jibu hilo liliwafanya wote kucheka wakiwa pale varandani.

"Hivi dada Jackline hatuwafuati wakina Nafiwe?"

Mustapha alimuuliza Jackline wakiwa pale pale nje varandani.

"Si hawa wametuchanganya? Lakini kama kawaida vamio liko pale pale usiku huu huu na kwa kuwa kila kitu kiko tayari nafikiri tuianze safari."

Jackline aliwaeleza.

"Ila mimi ningeomba wakina Mustapha wangesalia na Jasmine hapa pamoja na Titiana sisi wengine ndiyo tuelekee huko."

Jessica alitoa pendekezo.

"Dada Jessica una....."

Mustapha kabla hajamalizia kauli yake ilikatishwa na Jackline.

"Sikiliza Mustapha siyo kwamba tumewadharau la hasha kubaki hapa pia ni kazi, hebu fikiria tukipishana nao wakaja huku ni nani wa kuwadhibiti?"

"Kwa hapo tumewaelewa dada, kazi na ianze."

Victor alimjibu. Hapo kila mmoja alichukua zana yake tayari kwa kwenda kwa madam Nafiwe kufanya shambulizi. Lakini wakiwa ndiyo wanatoka na kuelekea kwenye gari ambalo alikabidhiwa ufunguo mzee Jerome mara simu ya Jackline iliingia ujumbe, aliichukua na kuufungua ujumbe huo.

"NASHUKURU MMEUGUSA MOYO WANGU KWA KUWAANGAMIZA WAPENDWA WANGU LAKINI NATAKA KUWAHAKIKISHIA KUWA USIKU MMOJA UTATOSHA KULIPA KILE MLICHOKIFANYA KWANGU JIANDAENI."

Jackline aliusoma ujumbe ule na kuubeza akaiweka simu yake mfukoni na kuingia garini, safari ikaanza. Mzee Jerome kwa kuwa mitaa anaijua vizuri alitumia muda mfupi sana kufika kwenye mtaa liliko Kasri la Madam Nafiwe hapo aliegesha gari kando ya barabara kwenye kiuchochoro ambacho kipo mita kadhaa kutoka kwenye jumba hilo. Hapo waliacha gari na kila mmoja alichukua zana yake kisha wakapeana majukumu ya namna ya kuingia ndani ya jengo lile na kwa kuwa Jackline na Roberto waliingia kwenye jengo mwanzo haikuwa ngumu kwao hivyo waliwaelekeza wenzao namna ya kukaa kwenye tageti.

"Jessica wewe utapitia mlangoni kwa mbinu yoyote ile kwani pale getini hukaa mlinzi mmoja tu, mzee Jerome wewe utasalia hapa hapa kwenye gari kazi yako ni kuliangalia geti na kuchukua hatua stahiki. Roberto utapita njia yako ile ile na mimi kule kule ila kabla ya kila kitu kufanywa mmoja wetu anatakiwa afike pale afanye doria kwanza maana hawa kwa sasa hatujui wamejiandaaje? "

Jackline alihitimisha kugawa majukumu kwa wakina Jessica.

" Nakwenda mimi kuangalia naleta majibu muda si mrefu."

Roberto alimjibu akiondoka kwa mwendo wa kunyatia kuelekea upande wa nyuma wa jengo lile na baada ya kulifikia aliupanda ukuta na kuchungulia ndani, aliangaza huku na kule lakini hakuona hata kivuli cha mtu japokuwa kulikuwa na mwezi muda huo.

" Watakuwa wamekaa upande gani? Mbona kimya kiasi hiki? Au wako ndani hebu ngoja kwanza."

Alijiuliza maswali bila majibu na mwisho akaona ateremke pale juu na kuangukia ndani ambako alitua kwa staili ya kuviringika kisha akajiinua na kupiga goti kisha akachomoa kisu na kuirudisha bastola sehemu yake. Kisu kikiwa mkononi alianza kutembea kusonga mbele akiwa kainama, alifika mpaka kwenye ukuta wa jumba lile na kulifikia dirisha ambalo lilionekana lina taa iliyokuwa inawaka, alifika akainuka kwa kuibia na kuchungulia ndani lakini hakuona mtu yoyote ndani yake. Aliondoka na kulifuata dirisha la upande mwingine nako alichungulia ndani lakini hali ilikuwa ni ile ile.

"Washenzi hawa watakuwa wapi?"

Alijiuliza tena baada ya kuangukia pua. Ikabidi arudi nyuma na kuuendea mlango wa kuingilia ndani kwa mwendo wa kunyata alifika mlangoni ambapo alinyonga kitasa kikakubali akaingia ndani ambako huko alikagua kila chumba na kona zote lakini hakuambulia kitu chochote. Alitoka nje na kuurudisha mlango kama ulivyokuwa na kuondoka akalifuata jengo dogo lililokuwa upande wa kulia kwake na kuanza kulinyatia kama kawaida kwenye madirisha ambako alichungulia ndani lakini hakuweza kuona mtu.

"Buu shiiiit.....!! Watakuwa wapi hawa au wametuchezea picha nini?"

Alipojiuliza swali hili akajikuta mwili kama unapata ubaridi hivi, vipele vya baridi vikamtoka mwili mzima hapo kengele ya hatari ikamgonga kichwani.

"Mhh kwanini hivi, noo hapa kuna mchezo tumechezewa."

Aliondoka eneo lile na kwenda kuuparamia ukuta haraka na kurukia nje na kutoka mbio kuwafuata wakina Jackline.

"Tumechezewa mchezo hapa ndugu zangu jengo liko kimya sana hata panya tu hachezi humo ndani na katika kujiridhisha nimeingia mpaka ndani lakini hali ni ile ile."

Maneno ya Roberto yakawa kama yameongea na ubongo wa kumbukumbu wa Jackline ambaye aliukumbuka ujumbe wa Santana, na hapo hapo akamtaka mzee Jerome ageuze haraka gari na kurudi nyumbani.

" Umehisi nini mwanangu? "

Mzee Jerome aliuliza huku akigeuza gari.

"Hapana ila ni kama nahisi wale washenzi wameelekea nyumbani."

Jackline alimjibu mzee Jerome.

"Hata mimi nahisi hivyo hivyo na kwanza nina mashaka hata na yule mwenyekiti anaweza kuwa alitumiwa tu bila kujua na Santana."

Roberto alionesha hisia zake kwenye hilo.

"Acheni basi kubashiri mambo tusubiri kwanza tufike mengine yatajulikana huko huko."

Jessica aliona awakatishe maongezi yao kwani hawakujua ni namna gani alikuwa akiumia juu ya dada yake kumkuta salama au la. Huku Jackline naye aliendelea kujiuliza juu ya ule ujumbe aliotumiwa ulitoka kwa nani maana haukuwa na jina la mtumaji na hapo akaitoa simu na kuuangalia tena ujumbe ule lakini ilikuwa vile vile namba iliyotumika ilikuwa ngeni, hivyo akaona haina haja ya kuendelea kuwa nao akaufuta na hakutaka kumwambia mtu yeyote mle kwenye gari akaiacha ibakie siri yake. Walipoukaribia mtaa wao kama nyumba ya nne hivi nyuma walisimama na kila mmoja silaha mkononi na kuanza kuelekea nyumbani.

"Jamani nyumba kila mmoja anaifahamu ilivyo hivyo cha kufanya ni kupita pande mbili tu yaani kulia na kushoto. Roberto na Jessica piteni kulia halafu mimi na mzee hapa tutapita kushoto."

Jackline alitoa maelekezo kwa wenzake kisha minyatio ikaanza. Walitembea mpaka karibu na nyumba kwa kila watu upande wao na kuufikia ukuta ambao kwa tahadhari kubwa waliupanda na kuingia ndani. Na baada ya kutua walikwenda moja kwa moja mpaka kwenye madirisha kuchungulia ndani lakini kwa upande wa Jessica na Roberto wao baada ya kuingia ndani walikwenda kupitia kwenye maua ambako walikutana na mshangao baada ya kukutana na mwili wa Victor ukiwa karibu na ukuta wa nyumba ukiwa umeshambuliwa na visu vya kutosha.

"Mungu wangu Victor kashambuliwa tayari na hawa Wendawazimu?"

Aliongea Jessica ambaye hakutaka kupoteza muda alikimbilia ndani akipiga kelele za kumuita dada yake hakujali wameondoka au bado wapo yeye akili zake zikawa kwa dada yake.

Aliingia ndani na kukutana na wakina Jackline wakiendelea kuwatafuta baada ya kukuta vitu vimevurugwa si mchezo.

"Victor yuko huko nyuma kalalia midamu kibao!!!"

Jessica aliongea bila kujali kama kuna mtu ataumizwa na kauli yake.

"Unasemaje Jessica?"

Mzee Jerome alimgeukia Jessica na kumuuliza swali ambalo kabla hajajibiwa alitokea Roberto akiwa kambeba Victor ambaye alikuwa amelegea kuashiria kuwa amekufa huku Roberto akilia. Kila mmoja alimfuata ili kuhakikisha kama ni kweli. Wakiwa bado wanamshangaa Victor kwa namna alivyouawa mara mlango wa chumba cha mzee Jerome ulifunguliwa.


JE NI NANI KAFUNGUA MLANGO WA CHUMBANI KWA MZEE JEROME?


JASMINE, TITIANA NA MUSTAPHA WAKO WAPI?


MAJIBU YA MASWALI HAYA NI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA USIKOSE.


        #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post