NITAKUUA MWENYEWE - 84
sultanuwezotz.blogspot.com
Nafiwe alimuangalia Santana kisha akacheka kicheko cha dharau, akimkaribisha kiti daktari.
"Karibu mtaalam, mgonjwa ndiyo huyu lakini kama tulivyoongea ya humu ndani yabakie humu humu na si vinginevyo."
Nafiwe alimsisitizia daktari kwa yale ambayo waliongea kabla ya kufika pale.
"Wala usijali Madam shughuli kama hizi nimezifanya sana hivyo muwe na amani juu yangu."
Daktari alimjibu Nafiwe.
"Mnasemaga hivyo hivyo lakini dakika tatu mbele mlishabadilika."
Santana aliongea huku alikaa karibu na daktari kumpa nafasi ya kukiangalia kidonda chake.
"Hao ni wengine ila siyo kwangu mimi, naijua mipaka yangu ya kazi kwa hali zote lakini kabla sijaanza kazi mnaweza kuongea chochote kile kama nianze au niache na kuondoka maana ni kama vile mna wasiwasi na mimi."
Daktari aliona aoneshe msimamo wake mbele ya miamba hiyo.
" Unasemaje wewe? Uondoke kwenda wapi? Kama haukuwa tayari kwanini ulikubali kuja au ndiyo ulikuja kutuchunguza kisha upeleke ripoti huko siyo?"
Santana alisimama na kumkunja daktari ambaye alijua anaongea na watu wa kawaida hivyo kuweka utani wake.
"Brother ndiyo nini sasa tunakunjana namna hii wewe ni mtu wa namna gani usiyeujua utani?"
Daktari aliongea akiwa kasimamia ncha za viatu angekuwa peku tungesema kasimamia kucha kutokana na kabali ambayo alikuwa kakunjwa na Santana.
"Unasikia wewe daktari mimi siyo binadamu wa kawaida ni mtu hatari sana hivyo jiangalie na maneno yako? Utaokotwa mtaani ukiwa marehemu shauri yako."
Aliongea hayo na kumuachia, kitendo kile kilimfanya daktari kutokwa na jasho huku kikohozi kikiwa kimemkamata cha bila kutarajia.
" Nisamehe kaka sikujua kama vitu vidogo kama hivi vingetufikisha huku."
"Unanishangaa nini sasa tukiwa njiani nilikwambia nini? Na wewe umefanya nini? Nimekwambia kabisa kuwa mgonjwa wangu kavurugwa hivyo ukifika pale fanya kazi yako basi kujuana juana achana nako lakini wewe kichwa maji umekutana na kubwa yako, anza kazi bwana."
Nafiwe naye badala ya kumsaidia akaendelea kumsakama na maneno ya maudhi kitendo kilichozidi kumkwaza daktari.
" Okay sawa lakini laiti kama ningejua kuwa nitapatwa na haya wala nisingeingiza mguu humu kwenu."
Daktari aliongea huku akitoa vitendea kazi kwenye kibegi chake.
"Na wewe muda mwingine uwe unakuwa mstaarabu bwana mambo gani hayo sasa, kwani daktari alikutuma kwenda huko bila kampani ya kutosha?"
Madam Nafiwe alitupa shambulizi kwa Santana.
"Kwa hiyo unanisema siyo?"
"Siyo hivyo mimi nakuambia ukweli Big mambo yako siyo bwana."
"Haya bwana umeshinda wewe."
Aliongea hayo huku akiwa kakunja sura kutokana na vifaa vya daktari kuanza kazi yake ya kukisafisha kidonda bila shaka alikuwa akifidia aliyofanyiwa na Santana. Wakati matibabu yakianza Nafiwe aliwaita watu wake na kutoka nao nje kupanga yao na huku wakitoa nafasi kwa daktari kufanya kazi yake kwa uhuru.
"Kama mnavyoona hali si shwari hawa watu wametufikia kila kona, tusipochukua hatua za haraka tutaaibika nadhani ninyi wenyewe mnaona kila tukishambuliwa lazima mtu wetu apoteze maisha kitu ambacho siyo kizuri hata kidogo."
Madam Nafiwe hakutaka kuficha hisia zake juu ya kinachoendelea kati yao na wakina Jackline.
" Ni kweli kabisa Madam lakini bado tuna muda wa kufanya marekebisho na kuwarudi."
Robinson aliongeza.
" Halafu mimi nina mashaka na Robinson kwenye oparesheni hii, hivi ukikutana na Jackline uso kwa uso unaweza kumkabili kweli?"
Madam Nafiwe alimuuliza swali Robinson.
" Kuhusu hilo ondoa shaka kabisa kwa tumeshamfanyia majaribio mengi sana kwenye hilo baada ya kuwa na wasiwasi naye."
Mzee Bruno alimtoa wasiwasi Madam Nafiwe juu ya Robinson.
" Halafu kingine Madam unachotakiwa kukijua kwa sasa ni kwamba mtu huyo si mpenzi wangu na mbaya zaidi aliwaongoza wenzake kuwateka wazazi wangu na kuwatesa hivyo bado nina hasira nao sana."
Robinson alimfungukia Madam Nafiwe katika kuhakikishia kuwa hana mpango nao zaidi ya hasira nao.
" Okay vizuri kama uyasemayo ni ya kweli. Kumbe tunatakiwa kuchunguza uwepo wao kwenye maeneo matatu kisha tuwafanyie shambulizi, na maeneo hayo ni ile Hoteli ya The Camel ambayo mara nyingi wameonekana hapo, pili ni nyumbani kwa yule mzee walikoshambuliwa wenzetu nako wanaweza kuwa wameweka makazi yao na mwisho ni kwenye mahospitali wanaweza kuwa huko kwa matibabu ya mgonjwa wao hivyo tunatakiwa kutuma watu wetu kufanya uchunguzi mara moja kuanzia asubuhi."
"Bila shaka binti yangu mimi pia nitakuwa sambamba nanyi katika hili."
Mzee Bruno alijitoa kuungana nao kwenye mpango wao huu mpya ambao wanahisi unaweza kuwaletea matokeo chanya.
"Kumbe itakuwa vizuri mzee wangu, sasa Robinson na Malaika mtakwenda King's Medicare na Makambi hospitali kuwatafuta huko na pia mimi nitakuwa na mzee wangu kule The Camel Hotel na nyumbani kwa mzee Jerome na ninyi hapa Paul na wenzako mtakuwa na Santana kuilinda ngome sawa jamani?"
Alihitimisha Madam Nafiwe kwa swali la msisitizo ambalo mara nyingi jibu lake huwa ni ndiyo.
" Umeeleweka mwanangu hapo kila watu wajiandae kwa shughuli kama walivyopangwa."
Mzee Bruno aliungana na Madam Nafiwe katika hilo kisha daktari alitoka ndani akiwa na mkoba wake kuashilia kuwa kazi yake imekamilika na nyuma yake alikuwa Santana akiwa na sigara mdomoni.
" Kazi yangu imekwisha madam naomba mimi niende."
Daktari alitoa taarifa ya kazi yake.
"Okay sawa mtaalam wangu ingia tu kwenye gari nikukimbize mara moja."
Madam aliongea hayo huku akiifuata gari yake tayari kwa kumpeleka daktari.
"Vipi mambo yamekwenda vizuri?"
Mzee Bruno alimuuliza Santana.
"Yuko vizuri sema tu ujingajinga wake ndiyo sijaufurahia hata kidogo."
"Kijana wangu tulichokuwa tunakihitaji ni hicho tu hayo mengine unataka undugu kwake?"
"Yaishe mzee."
Santana aliona ahitimishe baada ya kuona mzee Bruno naye ni kama alikuwa amekwazika na yale ambayo alimfanyia daktari.
****
Jackline na Roberto walitoka pale hospitali na kuwaacha Jessica, Titiana na mzee Jerome kuendelea kumuangalia Jasmine. Safari yao muda ule ilikuwa ni kule uswahilini kwenye ile gereji ambayo walitoa oda ya gari mbili aina ya Suzuki 56 kwa ajili ya oparesheni maalum ambayo walikuwa wameipania hivyo waliamini wakipata magari hayo itakuwa poa sana. Hivyo kabla waliamua kwanza watie kwenye ile kampuni ambayo walikodi ile gari ili kuirudisha hivyo tairi ziliongoza huko na baada ya taratibu zote za kimalipo kukamilika walitoka na kuchukua Bajaj kuelekea kule gereji. Walifika na kumkuta kipanga wao ambaye waliongea naye na kwa kuwa kila kitu kilienda sawa walikabidhiwa kila mmoja yake kilichofuata hapo lilikuwa ni vumbi tu maana gari hizo zilikuwa vizuri barabarani. Breki ya kwanza ilikuwa ni Hotelini ambako waliingia ndani na kuchukua kila kilicho chao na kupakia kwenye magari yao rasmi ya kazi tayari kwa kuondoka.
"Tunakwenda wapi sasa maana na wewe dada yangu maamuzi yako yanakuwaga ya ghafla kama mganga wa kienyeji vile."
Roberto alimuuliza Jackline baada ya kuona wamepakia kila kitu chao kwenye magari huku akiunganishia na kiutani ndani yake.
"Nimehisi kuwa eneo hili litakuwa si rafiki kwetu kwa sasa maana nina imani baada ya tukio hili lazima wataanza kutuwinda tu."
"Ni kweli dada katika hili hata mimi nilikuwa nina hofu hiyo ilmradi umelibaini ni vyema kutokomea hapa. Sasa makazi mapya yatakuwa wapi?"
Roberto alimuuliza Jackline wakati huo akifunga buti la gari.
"Kuna sehemu moja nimeipata nasikia ni nzuri sana iko karibu kabisa bahari, hoteli hiyo inaitwa Flamingo Villas Boutique Hoteli naambiwa ni miongoni mwa hoteli ghali hapa Namibia."
"Kama umeipenda wewe basi na sisi tumeipenda vile vile tuanze safari."
"Poa."
Kila mmoja aliingia kwenye gari lake na safari ilianza mara moja, hoteli hii iko pembeni mwa Namport kwa kilometa za kutosha hivyo spidi za magari zilihusika. Wakiwa tayari nje ya mji wakingua msitu huu wenye hali Ujangwa mara Roberto aliyekuwa nyuma aliweza kuiona gari ndogo kupitia site mirror zake hivyo akawa amepata kazi mpya ya kuichunguza gari hiyo kama inawafuatilia au ina safari zake. Akamtumia ujumbe Jackline.
"Kuna mbwa ananusa mapito yetu huku nyuma."
Jackline alipousoma ujumbe ule akayapeleka macho kwenye site mirror ili kuiangalia gari hiyo lakini hakuweza kuiona kutokana na umbali kati yao hivyo ilibidi apunguze mwendo kwanza.
"Tusimame kwanza tuone uelekeo wao au ni bendera fuata upepo. Kama ni bendera lazima wapoteze mwelekeo."
Roberto alipoupata ujumbe huo ikabidi amuangalie Jackline atasimama sehemu gani ili naye afanye hivyo hivyo na baada ya mwendo kidogo walitia nanga. Walishuka na Roberto akatoa triangle zake na kuziweka kuashiria gari limepata tatizo kisha akaliegemea huku Jackline akiwa ng'ambo ya barabara akiongea na simu. Ile gari ilikuja na kuwapita kwa kasi na walivyoiangalia waliibaini ni gari ya kukodi si ya mtu binafsi hivyo wakawa wamebaini kitu, wakapeana ishara ya kuanza kuifuata nyuma gari hiyo. Roberto alitoa alama zake kisha kwenye gari safari ikaanza upya na safari hii ikiwa ni kasi kidogo kuhakikisha hawaipotezi ile gari.
"Kwa vyovyote vile lazima watatafuta uchochoro wa kujificha ili watutangulize mbele kama ni wenyewe hivyo hakikisha tunawaweka kati."
Roberto alimpigia simu Jackline kumuelekeza hilo.
"Hapa wamekosea njia lazima wagawane vipande vya ardhi na hapo ndipo watajuta kutufutilia."
Jackline alimjibu Roberto na kukata simu kisha kuelekea kukanyaga mafuta.
Baada ya mwendo mrefu gari ile iliacha barabara kuu na kuchepuka na kuwafanya wakina Jackline kuendelea na safari yao hilo halikuwasumbua kwani walijua ni janja tu hiyo hivyo hawakuweza kupunguza mwendo bali waliongeza mwendo kuwazuga. Na kama waliotea vile kwani walipofika kitongoji fulani cha wafugaji waliweza kuiona tena ile gari ikija nyuma yao kwa mwendo ule ule Jackline akamtumia ujumbe Roberto.
"Andaa mashine yako tukifika kwenye msitu ulio mbele yetu tunawasimamisha watuambie wanaelekea wapi?"
"Bila shaka, huwa haichezi mbali." Roberto alimjibu.
Na kweli walipofika tu kwenye kimsitu kile Jackline aliipeleka gari yake kulia na kuisimamisha huku Roberto kutokea kushoto aliikata barabara akasimama kisha wote kwa pamoja walishuka bunduki zao mkononi na kusimama katikati ya barabara na kuzielekeza kwenye ile gari iliyokuwa inawafuata, na katika kuwatia hofu maadui Roberto alipiga za juu futi chache kutoka sehemu ya juu ya gari hilo.
Jackline naye hakutaka kusubiri yeye alizichapa tairi zote mbili za mbele kama kawaida yake na kuifanya gari hiyo kuanza kuyumbayumba na kupoteza mwelekeo.
JE, UNAFIKIRI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.
#SULTANUWEZO