NITAKUUA MWENYEWE - 83
sultanuwezotz.blogspot.com
Waliingia mpaka ndani ya KING'S MEDICARE CENTRE baada ya geti kufunguliwa na gari liliposimama wahudumu wa kupokea wagonjwa walifika na wheel chair na kumchukua Jasmine na kuingia naye kitengo maalum huku nyuma yao Jackline akiwa sambamba nao. Wakati wakiingia ndani Jessica na Titiana walisalia nje kusikilizia kitakachoendelea huko ndani na baada ya dakika chache Jackline alitoka nje kuungana na wenzake na kuwaeleza kinachoendelea.
"Kila kitu kinakwenda vizuri wameshaingia naye chumba cha upasuaji."
Jackline aliwataarifu wenzake akikaa kwenye kiti.
"Mungu ampiganie dada yangu apone."
Jessica aliongea huku chozi likimtoka, Titiana alimfuata na kumtuliza.
Wakiwa pale mara alifika Daktari Abbas Mukesh na kushuka garini, aliongoza ofisini kwake huku akiitazama saa yake kwani kwa namna ambavyo alivyokuwa akitembea kwa kasi kidogo ni dhahiri kabisa alikuwa amechelewa. Lakini alipowakaribia wakina Jackline pale walipokaa aliwaangalia kidogo na kwa kutaka kupata uhakika zaidi alishusha miwani yake.
"Ni macho yangu au ni kweli ninachokiona?"
"Daktari Abbas wala huna sababu ya kujiuliza mara kumi kumi uko sahihi kabisa macho yako hayajakudanganya sisi ndiyo wale wale uliojaribu kuokoa uhai wao."
"Yes, Jackline?"
Daktari Abbas Mukesh aliuliza kwa hamaki kidogo.
"Ndiye mwenyewe mimi na pembeni yangu hapa ni Jessica pamoja na friendmate wetu Titiana."
Jackline alitoa utambulisho.
"Wao nafurahi kuwaona mkiwa katika nyuso za furaha kiasi hicho, bila shaka kuna jambo mpaka mko hapa kwetu?"
"Ni kweli daktari tumepata tatizo."
"Hebu nifuate ofisini kwangu tukaongelee hilo tatizo lako tafadhali."
Daktari Abbas alimtaka Jackline aongozane naye ofisini kwake ili akajuzwe hicho kilichowaleta pale. Hivyo alinyanyuka na kuongozana naye.
"Karibu Jackline, kulikoni huko?"
Daktari Abbas Mukesh alimkaribisha Jackline na kutaka amweleze kilichomleta King's Medicare Centre.
"Kama ujuavyo majanga yaliyo nyuma yetu."
"Ndiyo nafahamu."
"Basi jana lile kundi linalotuwinda lilifika nyumbani kwa mzee Jerome kwa kutaka kufanya umafia wao lakini kwa bahati nzuri tukawa tumewawahi na kutokea majibishano ya risasi yaliyopelekea Jasmine kupigwa risasi."
"Jasmine kapigwa risasi? Ya wapi? Na vipi hali yake?"
Daktari Abbas alijikuta akitokwa na maswali mfululizo ambayo hayakusubiri majibu.
"Tumekuja naye yuko chumba cha upasuaji kwani alipigwa ya begani ambayo hatujui imemuadhiri kiasi gani?"
"Okay hebu ngoja kwanza."
Daktari Abbas alimwambia Jackline asubiri kwanza alichukua simu na kupiga kitengo cha upasuaji ili kujua nini kinaendelea kwa mgonjwa wanayemfanyia upasuaji.
"Enhh vipi upasuaji unaendeleaje kwa huyo binti."
"Mkuu ndiyo tunamalizia haikuwa mbaya sana kwani ilikuwa ni begani na tumefanikiwa kuitoa risasi moja na hapa ndiyo tunammalizia kumshona."
Daktari mkuu wa kitengo cha upasuaji alimweleza mkuu wake kinachoendelea muda huo.
"Poleni sana Jackline kwa majanga mnayopitia, Jasmine yu buheri wa afya na upasuaji umekwenda vizuri ametolewa risasi moja begani."
"Mungu mkubwa, lakini haya yote yatapita na maisha mengine yataendelea. Kikubwa tufahamishane kinachoendelea kwani wale watu siyo wazuri najua watataka kufanya mauaji kwa wote walio karibu na sisi."
Jackline alitoa tahadhari kwa daktari kutokana na kilichotokea kwa mzee Jerome Whistle hakutaka kitokee kwa wengine.
" Usijali Jackline toka tulipolijua hilo tulichukua tahadhari zote lakini ni vyema kukumbushana hili."
"Sawa sawa na pia nakushukuru kwa msaada wako uliotufanyia kwa kushirikiana na daktari Hans Murray wa Makambi hospitali kule Windhoek hakika ninyi ni wa thamani sana kwetu na Mungu aendelee kuwapa uhai zaidi ili msaada mliotufanyia sisi mfanye na kwa wengine pia."
Jackline hakusita kutoa pongezi zake kwa daktari Abbas.
" Jackline usijali kabisa katika hilo kwani ni jukumu letu kufanya hivyo maana ndiyo taaluma yetu."
Daktari Abbas alipokea pongezi hizo na kumuahidi kuwa watafanya zaidi ya hayo kwa kuwa ndiyo shughuli yao. Wakiwa wanaendelea na mazungumzo mara aliingia mzee Jerome Whistle akiwa kaongozana na Roberto.
" Karibu mzee Jerome, vipi na wewe ulikuwepo pale nje?"
Daktari Abbas alimuuliza mzee Jerome kwani hakumbuki kama alimuona pale nje.
"Hapana daktari mimi ndiyo nimeingia muda huu na nilipokuulizia pale nje nikaambiwa uko ofisini hivyo nikaona si vibaya kama nikiungana nanyi."
"Karibu sana mzee wangu."
"Asante sana daktari vipi mgonjwa wetu anaendeleaje?"
Mzee Jerome alimuuliza daktari.
"La kumshukuru Mungu ni kuwa Jasmine anaendelea vizuri na oparesheni imeenda vizuri na kwa sasa bila shaka atakuwa yuko wodini."
"Da afadhali maana kwa namna tukio lilivyotokea lilimchanganya kila mmoja ila zuri kwetu ni kwamba yule ambaye alimchapa risasi amekufa na kwa ushirikiano na kijana wangu hapa tumemchukua na kwenda kumtelekeza mtaani huko."
Mzee Jerome alitoa maelezo ya kilichotokea.
" Vipi mliweza kumjua ni nani huyo?"
Jackline aliwauliza kama wamemtambua mtu huyo.
" Hapana ila sura yake si ngeni ni kama mtu wa Santana hivi."
Roberto alijibu huku akiitoa simu mfukoni ili awaoneshe picha ambayo alimpiga mtu huyo.
"Ni kweli Santana yuko nchini kwani huyu ndiye kijana wake wa karibu kuliko wote kwenye timu yake hivyo kama kafa huyu lazima kachanganyikiwa na hivyo anaweza kufanya jambo baya lolote lile. Huyu anaitwa Chude."
"Na ukumbuke pia aliyekuwa naye naye ana jeraha la risasi mkononi hivyo ni kuendelea kufanya uchunguzi kaenda kutibiwa hospitali gani?"
Roberto aliongeza. Baada ya maongezi yao waliongozana kuelekea chumba alikuwa Jasmine ili kujua hali yake na ikiwezekana awekwe chumba maalum chini ya uangalizi mkali kama hali yake itakuwa si nzuri kwa kuhofia kuingiliwa na mtu wa Santana.
" Baba dada Jasmine anaendeleaje?"
Ulikuwa ni ujumbe wa Mustapha akitaka kujua hali ya Jasmine.
Mzee Jerome hakusita kumjibu mtoto wake.
"Keshafanyiwa upasuaji anaendelea vizuri kwa sasa."
Waliwakuta wakina Jessica pale nje na kisha kuongozana nao mpaka wodini alikolazwa Jasmine baada ya upasuaji.
"Dada unajisikiaje kwa sasa?"
Lilikuwa ni swali la Jessica baada ya kuingia tu wodini na kumkuta akiwa kajilaza.
"Namshukuru Mungu, Madaktari na ninyi kwa kunipigania kwani kwa maelezo ya Madaktari ni kuwa kama ningecheleweshwa basi kama siyo kuupoteza mkono ingekuwa ni kupooza kutokana na risasi ilipokuwa imekaa."
Jasmine aliwaeleza kile alichoambiwa na Madaktari waliomfanyia oparesheni.
" Pole sana Jasmine, nakuahidi utakuwa poa muda si mrefu na utarudi kwenye majukumu yako."
Daktari Abbas alimhakikishia kuwa sawa muda si mrefu.
" Nashukuru sana daktari Abbas Mukesh natami hata iwe leo kwani baada ya kumuua Chude nilipigwa risasi hii na Santana baada ya kunifahamu na tayari nilikuwa nimemtageti hivyo hata alivyonipiga alikuwa anajihami tu kwani kitendo cha Chude kwenda chini kilimshtua hakukitarajia hata kidogo."
Jina la Santana kuhusika na kumpiga Jasmine liliwachanganya wote mle wodini kwani hawakutegemea kama angekuwa ni yeye wao walijua ni miongoni mwa vijana wao.
" Bad news' kama Santana ameingia mzigoni yeye mwenyewe basi ni habari nyingine hiyo tunatakiwa kupanga mkakati mpya wa kupambana nao."
Jackline aliongea baada ya kujua Santana ndiye aliyehusika na tukio lile.
"Ni kweli Jackline wakati Jasmine anaendelea na matibabu yake, tunatakiwa kuendelea na maandalizi ya shughuli mpya iliyo mbele yetu."
Roberto aliongea hayo naye baada ya kusikia kuwa Santana kaingia mzigoni.
****
Mzee Bruno Gautier na Robinson na kundi la walifanikiwa kumkuta Santana akiwa anatembea taratibu kwenye kibarabara cha vumbi huku akiwa hajui anaelekea wapi kwani hata watu aliokuwa anakutana nao njiani alishindwa hata kuwauliza uelekeo wake kwani alikuwa hajui chochote.
"Pole mkuu kwa majanga yaliyokukuta."
Robinson alimpa pole baada ya kukutana naye.
"Asante Robbie hali si nzuri kwetu kwani maadui wetu wamejizatiti vilivyo kila unayekutana naye si mzembe hivyo tuna kazi ya ziada ya kufanya."
Santana kwa mara ya kwanza alikiri udhaifu wao mbele ya wakina Jackline.
"Aisee inabidi tukuwahishe kwenye tiba kijana wangu kabla sumu haijatembea zaidi mwilini. Na Chude yuko wapi na gari?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana baada ya kuona yuko pekee yake.
"Mzee wangu kwa hali hii unapata picha gani juu ya swali lako? Kifupi ni kwamba Jasmine kamuua Chude na mbaya zaidi alitaka kuniua na mimi nikamuwahi na ndipo nikapata upenyo wa kukimbia ile nafika nje nikakutana na chuma kilichocheza na mkono wangu, nilijikuta napotea mpaka gari ilipo."
"Pole sana kijana wangu kwa janga lililokukuta, kwa hiyo ndiyo kusema Chude hatuko naye tena?"
Mzee Bruno Gautier alijikuta akiuliza swali tena.
"Ndiyo hivyo mzee wangu."
"Kumbe tulifuate gari mlipoliacha na kisha tuufate mwili wake...."
Kabla Robinson hajamaliza maneno yake alikatishwa na Santana.
"Unasemaje Robinson? Mrudi kule nilikotolewa nduki mimi mnafikiri kuna usalama huko? La muhimu nimepona tuondokeni vyuma vinanunuliwa lakini si uhai."
Hakukuwa na la kufanya zaidi ya kuondoka eneo hilo kutokana na Santana kutoa tahadhari. Lakini wakiwa wanaiacha barabara ya vumbi na kuingia barabara ya lami waliweza kuiona gari kwa mbele mita kadhaa inayofanana na ya kwao ikiwa kando ya barabara.
" Hee mbona gari liko huku tena?"
Santana alijikuta akiuliza swali baada ya kuliona gari likiwa eneo tofauti na kule ambako aliliacha.
"Labda limefanana tu mkuu inawezekana siyo lenyewe."
Robinson alimjibu Santana.
"No, ni lenyewe si unaona namba yake pale ni ile ile niliimaki 'N... 0'
Santana aliwaambia hiyo gari ni yenyewe na si kwamba labda giza limemchanganya la hasha hivyo walipolisogelea aliagiza kijana mmoja waliyekuwa naye aende kwa tahadhari akaliangalie.
Baada ya kulifikia na kukuta hakuna pingamizi lolote aliwapa ishara ya usalama hivyo nao walisogea mpaka pale na kuteremka.
"Shiiiiiiii... t !!! Si unaona hawafai wale Chude wamemuweka humo na kuyashuti matairi yote."
Santana alifoka baada ya kumuona Chude akiwa kalalia usukani huku matairi yakiwa hayana upepo.
"Mshusheni huyo humo mpakieni kule, Robinson lete waya tulifunge na kulivuta mpaka nyumbani hakiwezi kubaki hapa."
Mzee Bruno Gautier aliagiza hayo baada ya kuona kiongozi wake kama kachanganyikiwa vile akiwa anaongea peke yake.
Walifanya hivyo kisha Robinson aliingia kwenye gari bovu na mzee Bruno akaingia kwenye ile aliyokuwa akiiendesha, safari ikaanza.
Waliwasili kambini na haraka sana Santana aliingizwa ndani kwa matibabu huku mwili wa Chude ukitolewa na kupelekwa chumba maalum.
"Santana pole sana kwa kilichokukuta."
Nafiwe alimpa pole Santana kwa hali ambayo alikuwa nayo huku akitafuta namba ya daktari wake mwingine baada ya yule wa awali kuuawa na Jackline.
"Nakuona unavyochekelea mwanamke?"
Santana aliongea huku akivua koti na shati lake.
"Una maanisha nini Santana?"
Madam Nafiwe alimgeukia kumuuliza Santana baada ya kuikata simu ya daktari.
"Kwani siioni sura yako ilivyo?"
Santana alimjibu.
"Shida yako Santana hakuna jema ambalo umewahi kuniambia na sina uhakika iwapo kama kuna kijana wako yeyote umewahi kukubali kile anachokifanya."
Nafiwe alimfungukia Santana baada ya kuona kuwa imekuwa 'too much' kwa maneno yake ya shombo.
"Hebu tuachane na hizo mambo zako hebu mwambie huyo daktari afanye haraka maumivu yameanza."
Ilibidi Santana abadilishe mada ili kuepusha mgongano baina yao. Madam Nafiwe alitoka nje kwa hasira na kumuacha ndani Santana na kuingia kwenye gari ili kwenda kumchukua daktari ambaye alidai usafiri wake uko matengenezo.
" Punguza maneno, si unaona umemkwaza tayari Nafiwe kitu ambacho si kizuri kuwa nacho kipindi hiki cha matatizo."
Mzee Bruno Gautier alimtahadharisha Santana kwa mambo yake ambayo huyafanya pasipo kuangalia nyakati.
" Achana naye mzee wangu, huyo ni mwanamke tu siwezi kumnyenyekea hata mara moja wewe mwenyewe unakumbuka kipindi kile namnyenyekea Jasmine lakini leo hii si huyu kanikosakosa risasi."
"Ni kweli lakini angalia huyo naye unayemsema ana hasira na wewe kwa mambo uliyomfanyia unafikiri itakuwaje siku ukikutana naye face to face?"
"Mzee wangu kwa hiyo unanitisha na wewe?"
Santana aligeuka na kuwa mkali.
"Si hivyo nakuambia tu kuna wakati unatakiwa kubadilika kijana wangu nyakati zinabadilika."
"Aaaaghhh, unanipanda kichwani unaacha kuangalia kile kilichotuleta huku gizani mzee wangu unageuka babu mshauri au unamtaka Nafiwe?"
Santana aliongea hayo huku akiitoa bastola yake kiunoni akitaka kumshuti mzee Bruno lakini hiyo ilionwa na Robinson ambaye aliuwahi mkono ule.
" Mkuu unataka kufanya nini sasa hujionei huruma kwa hali yako? Kufanya hivyo hujui unatoa ushindi kwa mpinzani?"
Alimnyang'anya bastola hiyo na kumpiga maswali ambayo badala ya kujibu Santana alianza kulia kwa kwikwi.
"Robinson ume..ume....kua ee mpaka una...unachukua bast..."
Kabla hajamalizia maneno yake aliyokuwa akiyaongea kwa kuyakatakata kutokana na hasira zake aliingia Nafiwe akiwa kaongozana na mtu mmoja ambaye bila shaka ndiye Daktari aliyefuatwa kwa ajili ya kumtibu Santana.
JE, NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI YETU.
#SULTANUWEZO