NITAKUUA MWENYEWE - 82 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 82

sultanuwezotz.blogspot.com 


Wakiwa bado njiani Jackline akapata wazo la kumpigia simu mzee Jerome Whistle kujua yuko wapi ili ampe angalizo juu ya wageni wasio rasmi. Simu iliita na kisha aliipokea.

"Mwanangu vipi mlifika salama? Na mnaendekeaje lakini."

Mzee Jerome alianza baada ya kupokea simu.

"Tulifika salama na tuko salama mzee wangu, uko wapi muda huu?"

Jackline alimtupia swali mzee Jerome.

"Niko nyumbani hapa kuna kikazi nakifanya si unajua tena wadogo zako wako kwenye shughuli zao na leo walijihimu bandarini kuangalia mzigo kwa tuliowakabidhi boti hivyo nafuafua vinguo maana vimechafuka sana."

Mzee Jerome alimwambia Jackline akiwa na furaha zote akiwa hajui nini lengo la kupigiwa simu.

" Okay pole sana baba yangu, ila nikuombe rudisha nguo ndani na kisha hapo nyumbani ondoka na jifiche nyumba ya jirani uwe unaangalia getini kwako nahisi kuna watu wanakuja kwako si watu wazuri na sisi tuko njiani kuja huko, sijui umenielewa mzee wangu?"

"Kweli huu ni mwaka wa shetani, hivi wananitaka nini mimi lakini? Nimewalia nini ambacho kinawakosesha amani kiasi hicho? Sawa mwanangu ngoja nijikusanye haraka."

Mzee Jerome alikata simu na Jackline aliiweka simu mfukoni baada ya kuhakikisha kila kitu kiko vizuri.

Safari iliendelea lakini kwa spidi yote hiyo hawakuweza kuwaona hiyo ikatoa picha kuwa wamedhamiria si kwa mwendo huo.

" Hawa jamaa kiboko yaani kwa mwendo wangu huu sijawaona hata vumbi lao?"

Roberto ilibidi aongee baada ya kuona hakuna dalili ya kuwakuta wala kuwaona.

"Tufanye hima tutawakuta wamefika au tunaweza kuwaona mbele."

Jasmine alimtia moyo Roberto aliyekuwa kakitolea macho kioo cha mbele ya gari kama vile atoke awe mbele kabisa kwani alihisi ni kama vile haikimbii.Wakiwa umbali wa kama mita mia tano hivi kutoka kwenye nyumba ya mzee Jerome waliweza kuiona ile gari ikiwa imepaki mita chache kutoka getini kwa mzee Jerome.

"Ni kweli aisee gari lile pale tunafanyaje hapa?"

Roberto aliongea baada ya kuiona ile gari pale nje.

"Sogea mbele kidogo kisha paki pembeni tujue tunafanyaje, hofu yangu ni kama wamemkuta ndani."

Jackline alimuelekeza apaki kwani kwa kuiona ile gari tayari hakuna jema ndani ya nyumba ya mzee Jerome.

Jackline aliipiga namba ya mzee Jerome iliita lakini haikupokelewa, akaipiga tena lakini mwendo ni ule ule iliendelea kuita tu bila kupokelewa. Hisia ziliwaijia kuwa tayari mzee Jerome kapatwa na tatizo.

"Kuna shida ndugu zangu simu yake inaita tu bila kupokewa sijui ikoje?"

Jackline aliwaambia wenzake huku akiiangalia simu yake kama vile kuna kitu anakitarajia kukipata muda mfupi ujao kutoka kwenye simu hiyo.

Jasmine na Roberto walishuka na kuanza kutembea kuielekea nyumba ya mzee Jerome kupitia sehemu nyingine ili wasishtukiwe na walioko pale. Jackline naye akaona kwanini asalie kwenye gari akaona hapana akashuka na kujiweka sawa na kisha akaanza kuifuata barabara kwa maana ya kulifuata geti pasipo kujifichaficha kama wakina Jasmine ila tu kwa namna alivyokuwa kajifunga mwenyewe ingekuwa ni kazi kwa yeyote kumtambua kwa haraka. Aligeuka na kuwapa ishara wakina Jessica na Titiana kubaki garini.

"Tumeufikia ukuta lakini kuna milio ya risasi kutoka ndani."

Roberto alimtumia ujumbe Jackline.

"Kupitia huo ukuta tafuteni tageti haraka muwakabili kutokea nje."

Jackline alimjibu na kisha kuiweka simu mfukoni.

Muda huo Jasmine alikuwa kesha jiongeza na kulifikia eneo lilikuwa na urembo fensi ambazo ni ruvazi na kuchungulia ndani, kwa bahati aliweza kuona kinachoendelea mle ndani.

" Roberto njoo haraka uone kule."

Jasmine alimwita Roberto aliyekuwa akiiweka simu yake mfukoni.

Alisogea na kuchungulia ndani ambako waliwaona watu wawili wakipambana kuuvunja mlango wa kuingia ndani.

"Tunafanyaje hapa?"

Jasmine alimuuliza Roberto ambaye alikuwa bado akiendelea kuchungulia ndani wala hakuweza kumsikia Jasmine anazungumza nini. Jasmine aliona anachelewa alichokifanya alichukua bastola yake na kuilengesha kwenye kitundu kile na kuiseti vizuri kuwaelekea walipo wale watu kisha akaachia risasi mbili mfululizo. Kwa bahati mbaya hazikuwapata walishtuka na kuangalia huku na kule wakiwa wanakimbia kujificha.

"Sister vipi tena?"

Roberto alimuuliza Jasmine ambaye alikuwa anaitoa bastola pale huku akitukana.

"Wana Mungu wao washenzi wale, halafu nimeiona sura ya Chude pale."

Jasmine alimjibu Roberto huku akiondoka eneo lile kutafuta sehemu nyingine ambayo anaweza kufanya jambo.

"Baki hapo hapo endelea kuwacheki pale walipojificha wanafanya nini?"

Jasmine alimwelekeza Roberto huku yeye akiendelea kuizunguka nyumba kuufuata upande waliojificha.

"Mko wapi wanangu huku mambo si mazuri waliniwahi kabla sijatoka."

Mzee Jerome alimpigia simu Jackline kumweleza kinachoendelea.

"Hawajakudhuru mzee wangu?"

"Hapana bado wanapambana kuuvunja mlango wa kuingia ndani na mimi nimejificha stoo kwenye yaliko magunia ya nafaka na siyo kizembe niko na sub-machine gun yangu ambayo huitumia nikiwa kwenye uvuvi."

"Vizuri huko usitoke sisi tayari tuko nje tunajaribu kuwadhibiti."

"Sawa binti yangu, nawaaminia sana."

Jackline aliikata simu na kumpigia Jasmine ili kujua kinachoendelea, lakini badala ya kupokea simu Jasmine aliikata kitendo kilichotafsiriwa na Jackline kuwa kazi inakaribia kuiva haraka sana na yeye akalifuata gari la wale wabaya wao bastola ikiwa mkononi na kuipiga risasi za kwenye matairi ya mbele kisha akatulia akiwa katikati ya barabara kuona kama kuna anayeweza kujitokeza akaona kimya ndipo alipolisogelea na kufungua mlango na kuingia sijui alilifanya nini humo ndani lakini alitoka na kupiga tairi za nyuma na kujificha nyuma ya mti uliokuwa karibu na pale. Akiwa pale alisikia milio ya risasi kutoka ndani hivyo akaona atoke pale na kuufuata ukuta ili aupande lakini mara alisikia geti likigongwa kisha akatoka mtu akiwa kama kachanganyikiwa, Jackline akauachia ukuta na kuivuta bastola yake na kumtageti mtu yule ambaye alimpa mgongo.

Lakini kabla hajafanya lolote ashtukia jamaa akitoa ukelele huku akilishika bega lake na kutokomea ng'ambo ya barabara na kukimbia na kuliacha gari. Jackline alianza kumfukuzia yule mtu kule alikokimbilia.

"Hee nini kimetokea huko ndani?"

Jackline aliuliza baada ya kukutana na Roberto akiwa na anahema kwa nguvu huku kainama na kujishika magoti.

"Achana na huyo mshenzi kimbilia ndani kampe msaada Jasmine."

Jackline kusikia hivyo hakutaka kungojea maelezo mengi alitimua mbio ndani kuona kilichotokea. Baada ya kuingia alishangazwa kumkuta Jasmine akiwa chini anatapatapa kwa maumivu huku damu nyingi zikimtoka kwenye bega lake la kulia.

Haraka sana Jackline alimwinua na kumbeba kuelekea iliko gari yao ambayo inakaa kwa mzee Jerome, lakini akakumbuka kuwa funguo ziko ndani akatoa simu na kumpigia mzee Jerome.

"Toka na funguo ya gari haraka mzee huku nje Jasmine kajeruhiwa na risasi."

Akakata simu na kumshika vizuri Jasmine lakini wakati huo huo tayari wakina Jessica wakawa wameshafika na gari hivyo ikabidi wampakie baada ya kuona mzee Jerome anachelewa.

"Mshikilieni hivyo hivyo."

Jackline aliongea huku akiuendea usukani na kwa kasi ya ajabu aligeuza gari na kutimua vumbi.

Mzee Jerome anatoka anaambulia vumbi tu akatembea kulifuata geti lakini sijui nini kikamwambia geuka nyuma alipogeuka akamuona mtu kalala chini upande wa maua, akaangaza huku na kule kuona kama kuna yeyote alipoona hakuna alimfuata na kumuangalia. Muda huo huo akaingia Roberto akiwa na ile gari iliyoachwa pale nje.

"Mzee vipi uko salama? Hofu yetu ilikuwa ni kwako wewe."

Alimuuliza huku akishuka kwenye gari na kumfuata pale alipo.

"Huyo kachapwa risasi na Jasmine akiwa anashuka kwenye ukuta kabla hajaotewa na risasi iliyomjeruhi lakini nashukuru Mungu nilimshtua na risasi yangu iliyompata sijui ni mkono au bega maana alitoka mbio akiwa kashika sehemu ya mkono nimemkimbiza akawa kanizidi mbio."

"Mimi nilikimbilia ndani baada ya kusikia geti linavunjwa na kwenda kujificha stoo."

Mzee Jerome alimjibu huku akiendelea kumchunguza aliyelala kama bado anapumua.

"Mungu wangu huyu si ni mtu wa Santana?"

Roberto aliongea baada ya kumuona vizuri sura mtu yule.

"Vipi unafahamiana naye?"

Mzee Jerome alimuuliza baada ya butwaa la Roberto kutokea.

"Hapana lakini tumekutana mara nyingi kwenye mipambano kipindi wakina Jackline wako huku."

"Kwa hiyo unataka kuniambia wamekuja kufanya wanayoyafanya kwetu?"

"Mzee wangu unavyomuona huyu jua hata kiongozi wao asiyekubaligi kushindwa yuko hapa Namibia pia."

Roberto alimjibu mzee Jerome Whistle huku akimuinua na kumpakia kwenye gari lao lililotelekezwa na kisha kutoka naye wakiwa na mzee Jerome.

"Tunaelekea wapi kijana wangu?"

"Huu mwili tunatakiwa kuuacha nje na makazi yako kwa usalama zaidi na vile hatuwezi kujua iwapo gari hili ni lao au ni la wizi hivyo maiti na gari tunakwenda kuviacha huko."

Roberto aliongea huku akipambana na gari ambalo matairi yake hayana upepo hivyo kumvuta huku na kule barabarani lakini aliweza kuliwini. Baada ya kufika mbali kidogo alilipaki kando ya barabara na kumchukua marehemu na kumuweka siti ya dereva na kumuegesha kwenye usukani na kisha kufunga milango na kuondoka zao na kwa wakati huo hakuna watu waliokuwa wakitumia njia hiyo hivyo kuwa rahisi kwao kufanikisha zoezi lao. Mzee Jerome alitoa simu na kumtumia ujumbe mtoto wake Mustapha.

"Nyumbani tulivamiwa leo hivi ninavyowatumia ujumbe huu tuko barabarani tunataka kuelekea hospitali alikopelekwa dada yenu Jasmine kaumizwa vibaya na risasi."

Alipohakikisha ujumbe umemfikia mhusika aliiangalia namba ya Jackline na kuipiga.

"Mwanangu mmeelekea hospitali gani?"

"Tuko njiani kuelekea KING'S MEDICARE CENTRE."

"Okay na sisi tuko njiani kuja huko."

Alimjibu na kukata simu kisha akamgeukia Roberto na kumuelekeza walikoenda wakina Jackline.

"Safari ni KING'S MEDICARE."

Mzee Jerome aliongea kwa kifupi akiwa anaiweka simu mfukoni.

"Tuwahi tukachukue gari tuwawahi huko."

"Bila shaka kijana wangu."

Mzee Jerome alimjibu huku akiitoa simu mfukoni iliyokuwa inaita.

"Unasemaje Mustapha?"

Aliuliza baada ya kupokea simu.

"Hakuna mwingine aliyeumia baba?"

"Hakuna mwanangu ila tu tulifanikiwa kumuua mmoja wa Majambazi na mwenzake tulimjeruhi akakimbia. Si unanijua baba yako kwa shabaha."

Mzee Jerome alitumia nafasi kujivika kitambaa ya ustaa akimdanganya mtoto wake kuwa yeye ndiye aliyemuua jambazi.

"Baba umeanza uongo wako sasa ni nani asiyekufahamu kwa uongo wako. Ninaye kufahamu wewe kwa uoga wako kama hukujificha chooni."

Mzee Jerome alivyoona kashtukiwa na mtoto wake akamkatia simu. Lakini Mustapha akapiga tena.

"Ukweli mchungu eee? Tuache hayo dada kalazwa hospitali gani niende?"

"Ninyi rudini nyumbani mfanye usafi huko idadi yetu inatosha sana. Sawa kijana wangu? Ila uwe na adabu kwa baba yako."

"Sawa baba nimekuelewa."

Alikata simu na kuchukua funguo ya gari iliyokuwa mfukoni na kumkabidhi Roberto aliyekuwa akilikagua gari mara baada ya kulifikia lilipokuwa mle ndani.

Aliliwasha na kuondoka zao kuwafuata wakina Jackline hospitali


***


"Unasemaje mkuu wangu?"

Lilikuwa ni swali la Nafiwe kutoka kwa Santana baada ya kupokea simu aliyopigiwa.

"Acha maswali mwanamke wewe nimesema nifuateni sijui niko sehemu gani hapa na giza hili."

"Mbona sikuelewi tukufuate kivipi wakati mna gari?"

"Mpaka nasema hivyo ujue mambo hayako sawa huku hata kidogo."

"Kivipi au mlipotea njia?"

"Unaonaje kama ukinifuata ujue nikoje kuliko kuendelea kunitwisha maswali yako bibie?"

Santana aliona amkatishe Nafiwe baada ya kuona maswali yamezidi.

"Nimekuelewa mkuu jitahidi usizime simu ili anayekufuata aweze kuitraki."

"Najua bwana."

Santana alijibu kwa ukali na kukata simu.

Nafiwe alimgeukia mzee Bruno na kumjulisha alichoambiwa na Santana.

"Mzee wangu nahisi Santana kapatwa huko naona anaongea kwa ukali tu mara kapotea na yuko sehemu gani yeye ni mgeni."

"Inawezekana waliwazidi au hawakufika kutokana na ugeni wake."

Mzee Bruno Gautier aliongea alichokihisi.

"Inawezekana ikawa hivyo, lakini shida ya Santana ni ubishi si unakumbuka nilimwambia aongozane na mwenyeji akatuchamba kuwa sisi ni timu ya washindwa atakwenda na Chude kwa kutumia GPS yako wapi sasa hawajafika na GPS yao wamepotea na sasa timu ya washindwa inakwenda kumpa msaada."

Nafiwe aliyakumbuka maneno aliyoambiwa na Santana kabla ya kuondoka.

" Msamehe tu bila shaka kapata somo kikubwa wafuatwe huko maana giza limeanza kukolea hili."

"Ni kweli kabisa mzee wangu, Robinson jiandaeni mkafuate bosi wenu huko aliko sijui ni wapi lakini najua njia pekee ni kuitraki simu yake."

"Sawa mkuu."

Walijibu na kuliendea gari na kuwasha lakini mzee Bruno akaomba kuongozana nao huko hivyo hakukuwa na pingamizi lolote wakaondoka kuelekea huko.


JE NI NINI KITAENDELEA HUKO?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA KUJUA KILICHOJIRI.


          #SULTANUWEZO

      

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post