NITAKUUA MWENYEWE
Sehemu:05
sultanuwezotz.blogspot.com
Mzee Jonathan Ubao ni mfanyabiashara maarufu sana kwa Kanda ya kati, Magharibi na Kanda ya Ziwa.
Umaarufu huu uliongezeka zaidi mara baada ya kuongeza mara dufu miradi mingine ambayo ilikuwa chini ya kampuni aliyoianzisha iliyofahamika kwa jina la UBAO INTERNATIONAL TRADE.
Kampuni hii inahusika na uagizaji wa vipuri, mitambo na magari kutoka nje ya nchi.
Pia kampuni hii inasafirisha Maua kwenye nchi za Kanada na India hizo ni kimataifa na kwa upande wa ndani ya nchi inahusika na uandaaji wa mchele na kuupaki kwenye uzito tofauti tofauti na kupeleka mikoa ya Dar na Arusha.
Pamoja na yote hayo kitu pekee ambacho kilikuwa kinamuumiza kichwa ilikuwa ni juu ya familia ya mzee Joachim yaani mzee Fikirini na Jackline.
Aliumiza kichwa chake usiku na mchana, na Kiukweli alikuwa nchini katika mkoa wa Mwanza na si nchini China kama ambavyo alimwambia Jackline alidanganya lengo likiwa ni kujiweka mbali na mtoto huyo ambaye asilimia kubwa ya mtaji wote wa kampuni yake umetokana na mali za marehemu mzee Joachim na sasa Jackline alikuwa kahitimu Masomo yake nchini SA hivyo kurudi kwake tafsiri ni kuwa anakuja kuchukua mali za mzee wake ili azisimamie mwenyewe kwa ushirikiano mkubwa na baba yake aliyebaki mzee Fikirini.
Hili hakuwa tayari kuona linatokea mbele yake na alikuwa tayari kumwaga damu za Watu watakaoonesha dalili za kumfuatilia na ndiyo maana kitu cha kwanza kukifanya ilikuwa ni kuuza makazi yake na kuhamisha makazi yake na kutimkia sehemu ambayo Jackline ingemchukua karne na karne kujua na ndiyo maana alibadilisha na jina kabisa la kampuni.
Baada ya kutafakari kwa muda akamkumbuka rafiki yake ambaye miaka kadhaa nyuma alikuwa nyuma ya nondo pale gereza kuu la Dodoma.
Huyu jamaa issue zake ni kukodiwa kwa shughuli mbalimbali iwe kuteka, kuua na kadhalika, hivyo akaona amtafute kwenye namba yake ya zamani ili kujua kama alishatoka ili amshawishi kwenye mpango wake mpya.
"Griiii, Griiii, Griiii, kumbe yupo hewani alitoka nini gerezani?" Aliwaza mzee Ubao.
"Halooo." Iliita upande wa pili.
"Naongea na Abuu Surambaya."
"Ndo mwenyewe kaka upo Ndugu yangu."
"Niende wapi bwana, ila Kwa sasa naishi mkoani Mwanza."
"Ulinitenga kabisa kaka, hata kunitembelea pale gerezani?"
"Ndugu yangu kwanza naomba unisamehe kwa hilo lakini nadhani unafahamu maisha niliyoyapitia."
"Wewe tena, nakufahamu kama njaa. Lete mpya lakini."
"Mambo yako vipi bado unaendelea au umeacha?"
"Kaka nilikunywa damu ya kiapo hiyo ni mpaka kaburini, wewe kama una kazi Nambie."
Mzee Jonathan Ubao alimueleza kila kit rafiki yake huyo Abuu Surambaya. Na kumueleza nini lengo lake.
Abuu alimuelewa mzee Jonathan na kumwambia kuwa kuna vitu anavihitaji kwa muda huo navyo ni picha za wahusika, eneo wanakopatikana na mkwanja wa awali kama milioni hamsini.
Mzee Ubao alifurahi kusikia hivyo akiamini tayari wabaya wake mzee Fikirini na Jackline wanakwenda kulamba mchanga na kumuacha yeye akiendelea kutanua maisha na kushamiri zaidi kwenye biashara zake.
"Wamekwisha hawa." Aliwaza mzee Jonathan.
Alifanya maandalizi ya fedha alizohitaji Surambaya Pamoja na picha zao hivyo vyote alivituma Kupitia simu janja yake ya MACX, simu anayoipenda kupita kiasi, Hivyo Alifanya miamala yote kwa njia ya APPLICATION YA BENKI Fulani nchini. Baada ya kukamilika alitumiwa ujumbe.
"Nimepata, subiri majibu ndani ya siku tatu kaka." Aliandika Abuu.
******
Mji mzima wa Lupa ulizizima kwa vilio, kila kona ya mji safari ilikuwa ni moja tu nyumbani kwa mzee Fikirini ambaye alizua taharuki kwa kifo chake cha kujinyonga.
Na kilichopelekea watu kuacha shughuli zao na Kuelekea kwenye mji huu haikuwa tu kujinyonga kwa mzee Fikirini la hasha bali ni pamoja na kifo cha mke wake, mama Shamimu ambaye alikutwa na umauti baada ya kukuta mume wake kaning'inia chooni akiwa tayari kafariki hali iliyomkuta ni mshangao mkubwa uliomuangusha chini na kupelekea umauti wake.
Hivyo kwenye mji huu kulikuwa na misiba miwili ya hawa wazee.
Na kila aliyefika kwenye msiba huu alitokwa na machozi kutokana na namna ambavyo hawa mabinti wawili walikuwa wakilia kwa NGUVU kupelekea Sauti zao kukauka.
Vijana wengi walikuwa na kazi kubwa ya kumnyamazisha kijana mwenzao Robinson ambaye kwa wakati huu alikuwa ni familia moja na hii ya mzee Fikirini.
Na wengi walijua huyu Robinson alikuwa tayari ni mchumba wa Jackline.
Wanafunzi wa Sekondari ya Lupa, walifurika kwenye msiba huu kumpa Moyo mwenzao Shamimu.
Wakina mama wengi waliokuwa kwenye huu msiba walilia sana kutokana na kumpoteza mzee Fikirini aliyekuwa mcheshi zaidi popote pale ambapo alikuwepo lakini swali lilikuwa ni kwa nini wamejitoa uhai hawa wazee?
Mzee Kaaya na wazee wenzake waliandaa mazingira ya namna ya kuisitiri miili ya marehemu hawa wawili.
"Da, hili toto kweli limeumbika aise cheki linavyolia, Pamoja na kulia kote huko lakini bado litamu. Robinson analifaidi kweli." Yalikuwa ni maneno ya dogo mmoja fundi pikipiki.
"Robinson si bure, hapa kizizi kimetumika hawes mtoto mwenye sifa zote, mzuri, tajiri na msomi lakini kaangukia kwa kijana Fukara lakini handsome asiyekuwa na matunzo. Ina maana hakuwaona vijana na wazee wenye mtonyo hapa kati?" Alijibu kijana mmoja aliyejulikana kwa Jina la Chawa.
Wakati Utitiri huu ukiendelea kumiminika kwenye mji huu wa mzee Fikirini. Kati yao ni mtu mmoja ambaye aliungana na Watu wengine kwenye msiba huu.
Kila mmoja alikuwa akimtazama sana mtu huyu kwani alifika hapo akiwa na pikipiki aina ya XR450-KAWASAKI alifika hapo akiwa na begi lake mgongoni na akiwa na full black clothes (rainclothes).
Aliungana na wengine kwenye hatua zote za kusitiri miili ya hawa wazee.
"Huu msiba umebeba Watu wengi sana wanaojulikana na wasiojulikana mfano huyo jamaa hapo ni mgeni kabisa halafu cheki huo mpikipiki wake sasa." Aliongea kijana mmoja aliyekuwa pembeni ya mgeni huyo.
Baada ya mazishi kufanyika kila mmoja alitawanyika kurudi kwake kutokana na tangazo la mwenyekiti wa kijiji kuwa kutokana na msiba huu kuondokewa na wazazi wote wawili na kubaki na watoto tu tena mabinti, hivyo hakuna msiba utakaoendelea hapo na kuwaacha hawa watoto kutafakari juu ya misiba hii.
"Hivi Robinson huyu mtoto umewahi kummega?" Aliuliza rafiki yake Awadh.
"Awadh, maswali gani unayouliza hapa, unafikiri ni mahali Sahihi kwa swali lako?"
"Sorry boy, samahani bwana ilikuwa ni joke tu."
Mzee Kaaya alimfuata mtoto wake Robinson na kumnong'oneza kitu sikioni. Kitendo kilichomfanya Robinson kuinuka na kumfuata Jackline ndani.
"Pole Jack."
"Asante Robinson, ndo hivyo tena wazazi wametuacha wakiwa."
"Baba na Mama wanakupa pole sana na wanasema msijione wapweke kwani kwa wema uliotenda kwetu amedai Wapo kwa ajili yenu."
"Waambie nawapenda sana wazazi wako maana wao ndiyo wazaa chema, nakupenda sana Robinson ungana na mimi kwenye kipindi hiki kigumu nimeona nikueleze ukweli muda huu wa majonzi."
Jackline aliamua kueleza ukweli toka moyoni kwake namna ambavyo anampenda Robinson. Na Robinson alivyoambiwa hayo alibaki mdomo wazi japo hakuonesha wazi.
" Nakupenda pia Jack, nakuahidi sitakuumiza milele. "
Alijitahidi kuongea Robinson.
" Nashukuru sana Robinson, kuna mpango ambao baada ya siku nne tunatakiwa kuufanya."
Bila shaka.
Pamoja na kuwa kwenye majonzi lakini Jackline alikuwa bado kwenye mkakati ya kuhakikisha anamnasa mzee Jonathan akiwa Hai au amekufa.
Aliamini msiba huo ni zao la utapeli wa mzee huyu.
Baada ya kuondoka kwenye msiba huu, Abuu Surambaya alipaki pikipiki lake eneo la kijiji cha Upendo na kutoa simu yake.
"Boss...."
"Nakusikia Abuu.". "
"" Hawa watu nimewakuta tayari wanakoishi, lakini yule mzee Fikirini na mke wake wamekufa kicho cha ghafla, ambapo mzee Fikirini alijinyonga sababu haijulikani na mke wake alikufa kwa mshtuko wa kifo cha mume wake."
"Duuu, inakuwaje sasa!"
"Kale kabinti nimekakuta kapo pale."
"Lini unakapoteza hako maana ndiyo kamwiba."
"Ngoja kwanza msiba huu umalizike kwanza then nitaleta mshtuko mwingine kwenye familia hii na hivi sasa niko njiani naelekea jijini Mbeya kukutana na mchizi wangu Hasara niliyekuwa naye gerezani Dodoma."
"Mimi nakutegemea wewe Abuu."
"Bila shaka kaka."
Kisha akakata simu yake Na kuiweka mfukoni mwake na kuiwasha pikipiki yake na kuendelea na safari yake.
*******
Jackline alifika mapema Shuleni kwa Shamimu pale Lupa Sekondari kwa lengo la kwenda kumuaga.
Hii ilikuwa ni lazima aondoke kijijini hapo na kusafiri Kuelekea mkoani Dodoma kuanza maisha mapya lakini kichwani aliamini hii ni sehemu muhimu sana ya kufanikisha mpango wake wa kumnasa mzee Jonathan Ubao.
Na ambacho kilimvutia zaidi ni kuweza kumnasa Robinson kijana ambaye alimpenda mara baada ya kufika tu Lupa na hali hii ilimshangaza sana kwani kwa kipindi chote alichokuwa masomoni Afrika ya Kusini hakuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi zaidi ya kuwa na urafiki tu na kijana mmoja kutoka nchini Botswana waliyekuwa darasa moja.
Na kitu ambacho kilimvutia kutoka kwa kijana huyu wa Kiswana si kingine bali ilikuwa ni mazoezi na mapigano ya karate na judo ambayo aliyamudu sana chuoni hapo na kupelekea Jackline kupenda michezo hiyo na hivyo ikawa ni suala la kumuomba Simbozya amfundishe michezo hiyo.
Simbozya hakuwa mjivuni alikubali kumfundisha hivyo Jackline aliungana na wasichana wengine wanne kwenye mafunzo hayo ambayo waliweza kuyamudu vilivyo na kupelekea kukiwakilisha chuo kwenye mashindano mbalimbali ya Olympics duniani.
Miongoni mwa mashindano ambayo alifanya vizuri Jackline yalikuwa ni yale yaliyokwenda kwa jina la SOWETO INTERNATIONAL OLYMPICS 006 ambayo alishinda kwa kumpiga mwanadada wa Afrika Kusini aliyefahamika kwa jina la Malosa na kupeleka medali ya dhahabu chuoni hapo.
Hivyo katika suala la mapenzi alijikuta akiangukia mikononi mwa shamba boy (Robinson) ambaye naye hakulaza damu juu yake.
Alifika Shuleni na kumkuta mwalimu mmoja anaongea na simu akatulia pembeni kumsubiri amalize kwanza ndipo amweleze shida yake.
Mwalimu alipoona kuna mtu pembeni yake ilibidi akatishe maongezi yake kwenye simu.
"Naomba kukusaidia binti."
"Naitwa Jack." Alijitambulisha.
"Naitwa mwalimu Costantine, naomba nikusaidie Jack."
"Samahani mwalimu, ninamomba Shamimu."
"Uhusiano naye."
"Ni mdogo wangu."
"Ooh, wewe ndo yule mwenye ile Honda?"
"Haujakosea mwalimu."
"OK, ngoja nikakuitie mdogo wako."
Mwalimu Costantine aliondoka Kuelekea madarasani kumfuata Shamimu na dakika kadhaa akaja akiwa kaongozana naye.
"Jack mdogo wako huyo ila maongezi yawe mafupi nimemtoa kwenye kipindi."
"Dakika chache mwalimu." Jackline alijibu akimvuta Shamimu pembeni ambapo aliongea naye mambo kadhaa ikiwemo kukazania masomo zaidi ya chochote pia ilikuwa ni kumuachia fedha kidogo ambazo zingemsaidia kipindi ambacho yeye Jackline atakuwa mbali na mdogo wake huyo ambaye kwa muda huu ndiye mlezi wake.
"Dada nitakumis sana na sijui kwenye masomo kama nitafanya vizuri."
"Usiseme hivyo mdogo wangu mimi ninaimani utafanya vizuri sana kikubwa amini kuwa nitarudi baada ya kufanikisha suala nililokueleza ambalo itakuwa ndiyo dira yetu." Jackline alimfafanulia mdogo wake.
"Vipi kuhusu Robinson amekubali kukusindikiza?"
"Mdogo wangu hii siyo sehemu muafaka kwa mazungumzo haya, rudi darasani kaendeleze kitabu."
"Ila mimi bado nina kinyongo na kaka yangu kwanini afanye vile dada?"
"Mdogo wangu msamehe bure tu kuna siku ataelewa maana, mwache aendelee na maisha yake anayoamini ndiyo kila kitu kwake."
"Sawa dada nikutakie safari njema na mkafanikiwe na kurudi salama kuungana nami."
"Bila shaka mdogo wangu najua mpaka likizo ifike tutakuwa tumerudi."
Baada ya mazungumzo ya dakika kadhaa waliweza kurudi pale kwa mwalimu na kumkabidhi.
"Nashukuru mwalimu nimemaliza na naomba niwaache muendelee na kazi."
"OK, karibu tena Jack." Alijibu mwalimu Costantine.
Jackline aliondoka taratibu na kumuacha mwalimu Costantine akiyashibisha macho yake kwa nyuma kukitolea macho kichuguu ambacho alikifungasha Jack kwa nyuma. Ni kweli Jackline kaumbika kiasi cha kumtoa mate mwanaume yeyote ambaye ni lijali. Jackline aliondoka zake pale shuleni na kurudi zake nyumbani kwa ajili ya kuianza safari.
Tukutane katika sehemu inayofuata ya Hadithi hii. Lakini pia usisahau kuacha ujumbe wako juu ya simulizi hii.