HADITHI: NITAKUUA MWENYEWE - 06 (Mtunzi:Sultan Uwezo)


 NITAKUUA MWENYEWE 

Sehemu: 06

sultanuwezotz.blogspot.com


"Hallow boss."

"Lete habari mpya Abuu."

"Unahitaji habari mpya?"

"Abuu unauliza nini tena?"

"Boss hapa ninapoongea niko ndani ya shimo hapa porini, sisimizi wamezingira hili eneo wananitafuta."

"Buuu shiiiit! Umefanya nini sasa na hapo ni wapi?"

"Nilipofika hapa Makongolosi, nilitulia sehemu moja hivi nikamfuata pusha mmoja hivi kununua kitu cha Jamaica ili kuweka Sawa akili na wakati pusha yule ananishughulikia wewe ndo ulipiga tena kujua nitalala wapi si ndo nikajichanganya kuanza kukupa mchakato mzima na namna ya kuongeza vijana watatu kwa zoezi Zima. Kisha nikapewa changu nikalipa na kusepa nikilenga kulala sehemu moja inaitwa Matundasi. Nikiwa spidi kwa nyuma si nikaona kuna pikipiki kama tatu zikija kwa kasi."

"Kwa hiyo walikukamata?"

"Hapana boss ila nikiwa nakanyaga mafuta zaidi ghafla dude likazima kucheki nyuma jamaa hawa hapa ikabidi nichumpe pembeni na kutokomea porini na kuiacha pikipiki hapo, hivyo jamaa wameichukua na kulizingira eneo hili sijui kama nasalimika. Ila nikipona tu kutoka salama eneo hili lazima nirudi pale kati na kumsaka yule pusha hanijui mimi ni nani Mchawi yule."

Wakati Abuu Surambaya akiwa anawasiliana na mzee Jonathan juu ya janga lililomkuta katika eneo la Manyanya, ghafla akasikia sauti kwa juu ikitoa amri.

"Washa moto eneo lote hili kwanini tupoteze muda kwa mtu mmoja mpumbavu kama huyu ilmradi tumepata pikipiki lake na hili begi lake tukalikague tujue kuna nini ndani yake na haya ndo Majambazi yanayokimbia huko na Kuja kujificha huku machimboni."

"Sawa Afande."

Kweli moto uliwashwa eneo lote lile na moto ulikubali sheria, kwani ulisambaa kila eneo na kwa moto ule sidhani kama hata sisimizi watapona.

Kiufupi kila kitu kiliteketea kwenye msitu ule na mpaka kuleta hofu karibu na makazi ya Watu kwenye kijiji kile cha Manyanya.

Baada ya kuona moto umekolea vilivyo wale Askari Doria waliondoka eneo lile na kurudi kituoni wakiamini mtuhumiwa wao wameshamuangamiza pale.


***


"Huyu mshenzi mbona hapatikani hewani?" Aliwaza mzee Jonathan baada ya kupiga simu ya Abuu karibu mara sita pasipo kumpata hewani.

"Mume wangu mbona unaongea peke yako, kulikoni?" Aliuliza mke wake.

"Si mshenzi huyu hapatikani hewani?"

"Kwanini sasa."

"Dakika kadhaa nyuma aliniambia kajificha shimoni jamaa wametanda kila kona wanamsaka na pikipiki imenaswa baada ya kuzima wakifukuzana, sasa sijui wamemkamata?"

"Tutafanya nini sasa Mume wangu, nilikuonya lakini kuwa achana na mali za udhulumaji unaona sasa tumekuwa Wakimbizi ndani ya nchi yetu."

"Keleleeee....... Nitausambaza ubongo wako wewe, unafikiri akikamatwa kwa uzembe wake na mimi nitakamatwa la hasha zaidi nitaingia mtaani mwenyewe mpaka nimtie mkononi Jackline hawezi ishi katika dunia hii labda dunia nyingine pambafuuuu toka hapa."

Alimfokea mke wake akiwa kauma meno yake kuonesha kachukia sana na haitaji kusikia lolote tofauti na alivyopanga yeye.

Anachokiamini yeye ni kuuondoa uhai wa Jackline na ili apate fursa ya kuikuza kampuni yake Kupitia mihela ya marehemu rafiki yake mzee Joachim.

Aliumiza kichwa usiku huu pasi na kupata jibu zaidi ya kuona jasho likiendelea kumtiririka Mwilini wakati kwa muda huu jiji la Mwanza lilikuwa na baridi kali sana lakini mwili wa mzee Jonathan haukuliona.

"Au huyu mtoto ni mchawi nini?"

Aliwaza mzee Jonathan huku akijipiga piga kichwani kwa kutumia Mkono wa kisu chake.

"Griiiiiiiiiii, griiiiiiiii, griiiiiiiii."

Simu yake mzee Jonathan iliita na haraka sana akaitoa simu mfukoni na kuipokea haraka pasipo kuangalia ni nani mpigaji.

"Hivi wewe una akili zote kwanini bado umeuweka hapo si uwakimbie hao Askari wewe." Aliongea mzee Jonathan.

"Unasemaje shemeji mbona sikuelewi?"

Alijibu Mwanaheri, huyu ni mdogo wa mke wake akiwa Dodoma chuo cha Mipango aliamua kumpigia shemeji yake kumjulia hali lakini alichokutana nacho ni janga.

"Mhh, shabashi........." Alipoangalia kioo cha simu yake akagundua amechanganya madensa baada ya kugundua ni shemeji yake ndiye aliyempigia kabla ya kumjibu alikata simu hiyo haraka na kuzima simu yake.


****


"Niwashukuru sana wazee wangu kwa kukubali kukaa mdogo wangu kwa kipindi chote cha Masomo yake."

"Bila shaka Jackline ninyi ni wanangu ni jukumu letu kuhakikisha mnazifikia ndoto zenu pasipo kuathiriwa na Matatizo yaliyopita." Alijibu mzee Kaaya

"Nashukuru sana tena sana." Aliongeza Jackline huku akitokwa na machozi.

"Baby, punguza kulia hapa ni kwetu kila kitu kitakuwa vizuri pasi na shaka kabisa."

 Robinson Alimbembeleza Jackline.

"Nimekuekewa baby, ila roho inaumaa, naumia mimi........"

Huku akilia kwa kwikwi.

Robinson ilibidi atumie akili ya ziada kumbembeleza mpenzi wake. 

Huu ulikuwa ni muda wa Jackline kuondoka na mpenzi wake Robinson kuelekea jijini Dodoma kwa ajili ya kuanza maisha lakini tageti kubwa ilikuwa ni kuwatafuta marafiki wa karibu na mzee Jonathan ili wampe ukweli aliko baba yake huyo mlezi japo alijua itakuwa ni ngumu, alijipa matumaini ya kumpata popote pale iwe ni huko China au kwingineko. Na kilichokuwa kina muumiza kichwa ilikuwa kwanini asipatikane hewani? Na kwanini hakufika hata kwenye msiba wa walezi wake? Na kwanini huyu kaka Athuman afanye kitendo kile mbele ya watu? Ni maswali ambayo alijiuliza Jackline bila majibu yoyote. Athuman mtoto wa kwanza wa mzee Fikirini anaishi Mbeya akifanya biashara ya mitumba na baada ya kufika kijijini kuwazika wazazi wake alitoa ya mpya ya mwaka baada ya kuwatuhumu majirani zao kuwa wamewatoa kafara wazazi wake ili wakatumike kwenye mashamba ya tumbaku kitu ambacho kiliwaudhi sana wale majirani na laiti kama ingekuwa siyo busara za Jackline kumuombea msamaha kaka yao huyo bila shaka majirani wangeondoka lakini walibaki kutokana na busara za mtoto wa kike. Baada ya mazishi kukamilika Athuman hakusubiri kukamilisha taratibu zote za msiba aliondoka siku ile ile tena bila kuaga kitendo kilichotafsiriwa kuwa alimaanisha maneno yake. 

Safari ya kuelekea Dodoma ilianza kwa kupitia barabara ya Singida na hii ilikuwa ni baada ya kupata baraka zote za wazazi wa Robinson na ambao walichukua jukumu la kuishi na mdogo wake Jackline kwa kipindi chote ambacho wao hawatakuwepo. 

Wakiwa njiani maeneo ya Rungwa kuitafuta Singida Jackline aliona ampigie simu rafiki yake Simbozya kuomba ushauri katika hili. 

Kama utakumbuka huyu ni Mbotswana ambaye walisoma pamoja kule Afrika kusini na huyu ndiye aliyekuwa mwalimu wake wa mapigano ambayo yalipelekea kujizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya chuo chao kwa kushinda kwenye michuano mbalimbali. 

"Jackline hili si jambo dogo rafiki yangu na si la kuliendea kichwa kichwa huwezi jua mpaka kafanya hivyo kajiandaaje." Simbozya alimtahadharisha Jackline juu ya kukabiliana na mzee Jonathan. 

"Nifanyaje sasa, naomba ushauri wako mwamba." 

"Kama hutojali fanya maandalizi ya kuja huku BONDENI kisha tufanye mpango wa kukutana na yule rafiki yangu ambaye alikuwa ananitumia vipande vya video za mafunzo ya mapigano bwana Santana." 

"Yupi huyo mbona kama nimemsahau vile?" 

"Jackline, umemsahau Santana ambaye nilikutana naye kwenye mtandao wa Instagram?" 

"Okay, nimemkumbuka mshikaji wangu." 

"Ndiyo huyo sasa najua baada ya kujifua vilivyo ndipo tutamtafuta popote pale duniani huyo mzee na kisha kumuonesha namna dunia inavyotaka tuishi." 

Maongezi yake na Simbozya yalimwingia zaidi Jackline na hapo akawa amepata wazo jipya la kufika Dodoma na kuanza maandalizi mapya ya safari ya kuelekea Afrika ya kusini. 

"Itakuwaje sasa Jackline hili jambo mbona ni la ghafla sana." Robinson alimuuliza Jackline baada ya kuambiwa wanatakiwa kuelekea nchini Afrika Kusini kuongeza ujuzi wa mapigano ili kuja kumkabili mzee Jonathan ambaye inasemekana yuko nchini China. 

"Kivipi Robinson?" 

"Si kama hivyo unavyosema tunatakiwa kuelekea nje ya nchi ilhali wazazi wangu na mdogo wako wanajua tunakwenda Dodoma." 

"Ni kweli mpenzi lakini tambua kuwa katika hili tukisema tukaombe ridhaa yao hawatakubali hata kidogo hivyo unaonaje kama tukiondoka kimya kimya bila kuwapa taarifa na mpaka waje wajue ukweli tutakuwa tumerudi na zoezi litakuwa limekwisha." 

"Hapana Jackline haiwezekani hata kidogo, yaani niende nje ya nchi bila ridhaa ya wazazi?"

"Kwa hiyo unasemaje katika hili?"

"Mimi siwezi kwenda huko Jackline."

"Okay sawa, basi wewe itabidi ushukie Manyoni kwa kuwa tunakaribia kufika kisha utarudi nyumbani na mimi nitaendelea na safari yangu kamwe siwezi kurudi nyuma."

Na kweli baada ya kufika Manyoni Jackline alishuka na kwenda kumkatia tiketi Robinson ya kurudi Chunya, alirudi akiwa na tiketi mkononi lakini ajabu ni kwamba Robinson alibadili mawazo yake na kuigomea tiketi ile na kumsihi airudishe ile tiketi hata kwa kuiuza kwa nusu bei. Kwa namna ambavyo Jackline alifurahi alimwambia Robinson haina haja ya kuirudisha itabaki kwenye kumbukumbu zetu tuondoke zetu mpenzi, na safari ikaanza.



Nini kitatokea? Tukutane katika sehemu ya saba ya kigongo hiki.

Kwa maoni na ushauri dondosha komenti yako hapa chini tafadhali. 


       #SULTANUWEZO



Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post